Header AD

NBC YAZINDUA KAMPENI YA HAJJ KWA AJILI YA WATEJA WAKE WA HUDUMA ZA KIBENKI ZA KIISLAMU.

 Mkuu wa Idara ya Huduma za Kibenki kwa kufuata Sheria za Kiislamu wa Benki ya NBC, Yassir Masoud (katikati) akionyesha kadi ya ATM ya akaunti ya kiislamu ya benki hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni ambayo wateja wawili wa akaunti hiyo watajishindi tiketi mbili kila mmoja zitakawawezesha kusafiri kwenda kuhiji Makka mwezi Oktoba. Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam leo.  Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha na kulia ni Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Suleiman Lolila.

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) leo imezindua kampeni ya miezi miwili kwa ajili ya wateja wake wa huduma za kibenki zinazofuata sheria za kiislamu, ili kubaini washindi watakaoshinda Safari ya wawili iliyolipiwa kila kitu kwenda kuhiji Makka mwezi Oktoba 2012.

Kampeni hiyo ambayo ilizinduliwa katika Ofisi za Makao Makuu ya NBC ni sehemu ya sherehe za miaka 45 za benki ya NBC kutoa huduma za kibenki. Sherehe hizi zitawezesha wateja kushinda zawadi mbalimbali zilizotayarishwa kwa ajili yao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Idara ya kutoa huduma za kibenki kwa kufuata Sheria za Kiislamu wa NBC, Yassir Masoud alisema,"Kampeni hii siyo tu kwa ajili ya kusherehekea miaka 45 ya kutoa huduma bora za benki kwa wateja wetu lakini pia kusherehekea miaka miwili ya kutoa Huduma za kibenki zenye kufuata sheria za Kiislamu".

"Hii ni mara ya kwanza kwa kampeni ya aina hii kufanyika nchini na tunawakaribisha wateja wetu wote na yeyote mwenye nia ya kushiriki, washiriki kikamilifu ili kupata nafasi ya kushinda zawadi hii ya kipekee" alisema Bwana Masoud.

NBC ilianza kutoa huduma za benki zinazofuata Sheria za Kiislamu tangu mwezi Mei 2010. Hivi sasa huduma inayotolewa ni pamoja na Akaunti za Akiba za Kiislamu na Akaunti za Hundi. Hivi karibuni pia benki ilizindua ya Akaunti za Biashara za Kiislamu na akaunti za Kiislamu kwa Mashirika. Huduma hizo zinatolewa bila riba, na kwa kufuata Sheria za Kiislamu, pia ni wazi kwa wateja wote bila kujali imani zao.

Kampeni iliyozinduliwa leo itaisha Septemba 13, 2012, ambapo washindi watachaguliwa kwa njia ya droo. Washindi watajishindia safari iliyolipiwa kila kitu kwa ajili ya watu wawili kwenda Kuhiji. Zawadi ni pamoja na tiketi za ndege, malazi na fedha za matumizi wakati wa safari hiyo ya kwenda Makkah.

Kwa Wahariri;  NBC ni kampuni ya kutoa huduma za kifedha inayojali wateja. Tunashirikiana na wadau wetu wote ili kujenga mafanikio kwa mbinu zinazotizama maslahi ya mteja, ubunifu na utofauti wa bidhaa

 Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha (kushoto) akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampuni ambayo wateja wawili wa akaunti ya kiislamu ya NBC watajishindia tiketi mbili kila mmoja zitakazowawezesha kusafiri kwenda kuhiji Makka kwa gharama za NBC Mwezi Oktoba. Uzinduzi ulifanyika jijini Dar es Salaam leo. Katikati ni Mkuu wa Idara ya Huduma za Kibenki kwa kufuata Sheria za Kiislamu wa Benki ya NBC, Yassir Masoud na kulia ni Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Suleiman Lolila.

Daima Karibu Nawe

Kwa Taarifa Zaidi Wasiliana na;

 Mshauri wa Mahusiano ya Umma wa NBC, Eddie Mhina, eddie.mhina@nbctz.com
Reviewed by crispaseve on 08:26 Rating: 5

No comments

Post AD