Header AD

Swali la Mlata, jibu la Pinda, hotuba ya JK na kutekwa Dk Ulimboka


ALHAMISI wiki iliyopita, Mbunge wa Viti maalum (CCM) Martha Mlata alitaka kauli ya serikali kutoka kwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusu madai ya kuwapo watu wanaochochea mgomo huo kwa kuwahonga fedha madaktari ili nchi isitawalike.
Bila tahadhari wala kupima athari na uzito wa swali hilo, Waziri Mkuu Pinda alitoa jibu ambalo hadi sasa naamini analijutia kutokana na tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa msitu wa Pande lililomkuta kinara wa mgomo huo, Dk Stephen Ulimboka usiku wa siku hiyo hiyo.
Katika jibu lake ambalo pia halikupima madhara yanayoweza kufuata, Waziri Mkuu alisema Serikali imepata taarifa za kuwapo wanaochochea mgomo huo na tayari imeviagiza vyombo vya dola kuchunguza kujua ukweli ili hatua stahiki zichukuliwe.
Kwa kauli hii, Pinda amejikuta akijiingiza kwenye mtego ambao utamchukua kipindi kirefu kujinasua baada ya tukio la Dk Ulimboka kutekwa kuhusishwa na agizo la Serikali la kuchunguza walio nyuma ya mgomo, hasa baada ya watekaji kudaiwa kumhoji Ulimboka nani anawatuma kugoma?
Kwa kauli yake aliyoitoa kwa shida mara baada ya kuokotwa na wasamaria wema, Dk Ulimboka alidai pamoja na mambo mengine waliomeka anaoamini walitumwa na serikali walimtaka kueleza iwapo kuna watu wanawatumia madaktari kupitia mgomo ili kuiyumbisha Serikali.
Kuna maswali mengi ya msingi yanajitokeza hapa:- Mosi, je, Mlata alitumika kuuliza swali bungeni ili kumpa fursa Waziri Mkuu kutuma ujumbe kuwa tayari Serikali imegundua mbinu, hila na mkakati ya wapinzani wake kutaka nchi isitawalike?
Pili, watekaji walikuwa wakitekeleza agizo la Waziri Mkuu, Rais au kiongozi yeyote Serikali, dola au chama tawala la kuchunguza na kuwatambua waliowatuma madaktari kugoma?
Hisia za Serikali kuhusika kwenye tukio la Dk Ulimboka zimezidishwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Jumapili iliyopita pale alipojaribu kuiepusha Serikali yake na tuhuma hizo bila mafanikio kwa kukiri kuwa miongoni mwa wasaidizi wake, wamo waliokuwa hawamtaki daktari huyo hata kuwemo kwenye timu ya majadiliano kati ya madaktari na Serikali.
Kwa kauli yake, Rais Dk Kikwete alisema yeye ndiye aliyezima juhudi za kumuengua Dk Ulimboka zilizokuwa zikifanywa na wasaidizi wake pale alipoamuru kinara huyo wa mgomo aachwe awemo kwenye timu a madaktari iwapo kada hiyo inamwamini kuwa ndiye anayeweza kusimamia na kutetea maslahi yao.
Rais amesisitiza kuwa Serikali haina, haitakuwa nayo wala haiwezi kupanga njama za kumdhuru Dk Ulimboka kwa sababu ya mgomo wa madaktari kwa sababu ni moja ya nguzo na daraja muhimu kati ya serikali na madaktari katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro kati ya pande hizo.
Bila kumung’unya maneno, kauli hii inadhihirisha kuwa ndani serikali, wapo maafisa ambao kwao Dk Ulimboka alikuwa ni tatizo kuhusu suala la madaktari na hawa siyo ajabu wakaunda njama za kumdhuru kama ilivyotokea baada ya juhudi zao za kumuengua kwenye kamati kuzimwa na Rais.
Kwa uzoefu wa kawaida uliozoeleka miongoni mwa watumishi wa serikali wanaoshindwa kutimiza wajibu na majukumu yao, ni rahisi kwao kutumia njia ya mkato ya kumdhuru na hata kumtoa roho anayewafanya waonekane hawafai mbele ya mteule wao na jamii kwa ujumla.
Inawezekana waliomteka Dk Ulimboka walitumwa kufanya kazi halali ya dola ya kuchunguza matukio yanayohatarisha usalama wa taifa kama lilivyo mgomo unaoendelea lakini waliowatuma hawakuwapa mbinu wala maelekezo ya kutekeleza jukumu hilo ndiyo maana wao wakachagua utekaji nyara, kutesa na kutupa baada ya kuhisi wameua.
Kama ndivyo, basi serikali iwachukulie hatua za kisheria kwa kuwafikisha mahakamani waliotumwa kuchunguza swala hilo kwa kwenda mbali zaidi katika uchunguzi wao kwa kutumia njia ya utekaji, kutesa (kwa lengo la kuua), badala ya njia ya kawaida na za kitaamu za kuhoji na kuchimbua yaliyofichika wanayofundishwa wapelelezi wetu.
Ili kufikia hapo, serikali kwanza ijisafishe kwa kuunda tume huru kama ile ya Jaji Musa Kipenka iliyochunguza mauaji ya wafanyabiashara wa madini Mahenge waliodaiwa kuuawa na polisi.
Wajumbe wa tume hiyo wawe madaktari wanaoaminiwa na wenzao, viongozi wa dini, wanasheria waliobomea, wapelelezi huru na Serikali yenyewe.
Tume ya polisi wanaotuhumiwa kwa tukio hilo haiwezi kupata ufanisi kwa sababu siyo tu kwamba haikubaliki kwa wadau lakini pia haina mamlaka ya kimaadili baada ya kiongozi wake, Ahmed Msangi ambaye ni Mkuu wa kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai, Kanda Maalum ya Dar es Salaam kudaiwa kutambuliwa na Dk Ulimboka kuwa mmoja wa watekaji wake.
Hata kama Msangi hahusiki kama ambavyo tayari ametetewa na kamanda wa operesheni wa jeshi hilo, Paul Chagonja, bado dhamira yake haitakuwa huru kutekeleza wajibu na majukumu yake katika tume hiyo.
Kama alivyokonga nyoyo za Watanzania alipounda Tume ya Jaji Kipenka baada ya polisi kama kawaida yao kukimbilia kujikosha kutohusika na mauaji ya wafanyabiashara hao (kama ilivyofanya sasa), Rais Dk Kikwete aunde tume huru kuchunguza tukio la Dk Ulimboka.
Kinyume chake, madaktari, wanaharakati na umma wote wa Watanzania utaendelea kuamini kuwa kuna mkono wa Serikali kwenye tukio hili la Dk Ulimboka kwa sababu bado kuna mawe mengi yameachwa bila kugeuzwa kuangalia kilichojificha chini yake.
Utata wa swali la mbunge Mlata, jibu la Waziri Mkuu Pinda na hotuba ya Rais Dk Kikwete kuna maswali mengi ambayo majibu yake ya haraka ni kuwa serikali inahusika na tukio la Dk Ulimboka hadi pale uchunguzi huru na wa kina utakapofanyika kujua wahusika bila kujali wanatoka serikalini au ni wahalifu kama wahalifu wengine.
Muhimu zaidi kwa taifa letu ni kwamba kamwe tusiruhusu jamii yetu iwe ya watu wenye kuanza kujenga tabia ya kutekana, kuumizana na hata kuuana pale makundi mawili yanapopishana kiimani, itikadi, misimamo na kimaslahi katika jambo lolote.

Lakini lililo dhahiri ni kuwa hata Serikali ikijitetea, ushahidi wa kimazingira kuhusu swali la mbunge Mlata, jibu la Pinda na hotuba ya Rais Dk Kikwete vinaizamisha Serikali kwenye tope la tuhuma za kuhusika na tukio la Dk Ulimboka na njia pekee ya kujinasua ni uchunguzi huru ambao hauwezi kufanywa na polisi ambao katika hili ni watuhumiwa
Reviewed by crispaseve on 11:24 Rating: 5

No comments

Post AD