Header AD

Wakali wa Epiq BSS Lindi waanikwa


Jaji Mkuu wa EBSS 2012 Ritha Paulsen akimfariji mshiriki mmoja wa washiriki wa shindano hilo  aliyekosa nafasi ya  kuchaguliwa.
Mwanadada ahuyu alikuwa mmoja kati ya waliojitokeza kushiriki katika kinyang’anyiro cha kuwatafuta wakali wa Lindi.

Na Mwandishi Wetu
PAZIA la shindano la Epiq Bongo Star Search (EBSS 2012) mkoa wa Lindi limefungwa ambapo washindi watano tayari wamepatikana.
Msako huo wa vipaji mkoani hapa ulifanyika kwa siku mbili mfululizo ambapo vijana wengi walijitokeza kuonesha vipaji vyao kiasi cha kuwapelekea majaji kuwa na wakati mgumu kupata wawakilishi.
Akizungumzia mchakato wa Lindi Jaji Mkuu wa EBSS 2012 Ritha Paulsen alisema kuwa ikiwa ni mara ya kwanza kuanza kwa shindano hilo mkoani hapa ameridhishwa na idadi ya watu waliojitokeza.
Alisema kuwa EBSS 2012 ilifanya uamuzi wa kutafuta vipaji mkoani Lindi ili kuwapatia nafasi washiriki wa Lindi kuonesha uwezo wao wa kuimba aina mbalimbali za nyimbo.
“Mkoa wa Lindi ninaamini kuwa ni kati ya mikoa ambayo kuna vipaji vingi vilivyojificha hivyo EBSS kazi yetu ni kuwatengenezea njia ya kufikia mafanikio yao, sasa tukipata vipaji hivi kitakachobakia ni wao kuonesha uwezo wao”alisema Ritha.
Naye Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wa kampuni ya simu ya Zantel ambao ni wadhamini wa EBSS 2012, Awaichi Mawalla mbali na kuridhishwa na idadi ya watu waliojitokeza alielezea umuhimu wa sanaa katika kuinua uchumi wa mkoa wa Lindi.
“Hii ni nafasi ya kipekee kwa wakazi wa mkoa huu kujitengenezea ajira kupitia muziki, kama inavyofahamika kuwa Zantel imejikita katika kurahisisha maisha ya watu wote sasa kwa kuona umuhimu wa muziki katika kukuza ajira imeamua kujikita katika muziki kwa maendeleo ya vijana” alisema Awaichi.

Shindano hilo lishapita mikoa mitatu tayari kati ya nane litakayoifikia mwaka huu, na wiki hii litakuwa mkoani Arusha kusaka vipaji.
Reviewed by crispaseve on 11:36 Rating: 5

No comments

Post AD