WAZIRI MKUU AONYA MATUMIZI YA RUSHWA UCHAGUZI MKUU
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewaonya Watanzania kuwa makini na watu wanaotumia
rushwa ili kupata nafasi za uongozi na hasa kwenye uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2015.
Ametoa
onyo hilo leo mchana (Jumapili, Julai 27, 2014) wakati akizungumza na
mamia ya waumini na viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya uzinduzi
wa dayosisi mpya ya Ruvuma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT) na kuwekwa wakfu Askofu Amon Mwenda aliyeteuliwa kuongoza
dayosisi hiyo.
“Ninawasihi
wananchi wawe makini na viongozi wanaopenda kutoa rushwa hasa katika
kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu. Kama mtu ana nia ya
kweli ya kuongoza ni kwa nini atumie fedha ili kupata nafasi ya
uongozi?,” alihoji.
“Tatizo
ni kwamba hata wananchi hivi sasa wanakubali kupokea kile kinachotolewa
na wagombea. Atakuja huyu atakupa hiki na mwingine naye atakupa kile,
lakini ujue akiingia madarakani anaanza kurudisha haraka vile
alivyowagawia,” alisema.
Aliwaonya
wananchi kuwa makini ili wasije wakageuzwa mtaji wa kuwanufaisha watu
binafsi. “Tukikubali kutumika ni sawa tutapata viongozi wakati wa
uchaguzi, lakini watakuwa ni wale wasio na hofu ya Mungu, wenye kujali
maslahi yao kuliko ya wananchi waliowachagua,” aliongeza.
Aliwaomba
viongozi wote wa dini waliohudhuria sherehe hizo pamoja na waumini wote
waendelee kuliombea Taifa ili Mungu aliepushe na janga hilo la watu
kupenda rushwa. Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wazidi kuuombea
mchakato wa kupata Katiba mpya ili wabunge wote warejee ndani ya Bunge
na kuikamilisha kazi waliyoianza.
Alimuomba
Askofu huyo mpya apokee jukumu hilo kwa mikono miwili na kumuahidi kuwa
kama Serikali watakuwa naye bega kwa bega kuwaongoza Watanzania walioko
kwenye dayosisi yake. Dayosisi hiyo mpya inahusisha mkoa wote wa Ruvuma
na wilaya ya Ludewa eneo ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba
72,630. Kati ya hizo km. za mraba 64,233 ni za mkoa wa Ruvuma na km. za
mraba 8,397 ni za wilaya ya Ludewa.
Mapema,
akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kusimikwa rasmi, Askofu
Mwenda alisema dayosisi mpya ya Ruvuma imezaliwa katika kipindi chenye
changamoto nyingi za kidunia na utandawazi ukiwemo mmomonyoko mkubwa wa
maadili.
Hata
hivyo, akiainisha malengo ya dayosisi hiyo ambayo anakuwa Askofu wake wa
kwanza, Askofu Mwenda alisema mbali ya kufundisha neno la Mungu,
dayosisi hiyo itahimiza ufanyaji kazi ili wakazi wake wawe na akiba ya
chakula cha kutosha.
Alisema
watashirikiana na Serikali na wadau wa ndani najje katika kutoa huduma
za kijamii hasa elimu na afya. Aidha alisema atakabiliana na changamoto
za sasa ambazo alizitaja kuwa ni mmomonyoko wa maadili, rushwa, mauaji
ya albino, unajisi wa watoto na ubakaji wa wanawake.
Akitoa
shukrani kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk.
Alex Malasusa alisema Kanisa lingependa kupata viongozi ambao ni wacha
Mungu.
Akirejea
mahubiri yake, Askofu Malasusa alisema inashangaza kuona kuna baadhi ya
watu wanagombea nafasi za uongozi lakini hawana mapenzi na Mungu
aliyewaumba watu anaotaka kuwaongoza. “Bila kujali imani ya mtu,
tunatamani tungepata kiongozi ambaye anamcha Mungu. Awe anapenda
kuhudhuria ibada. Awe anampenda Mungu ndipo atawapenda watu
anaowaongoza,” alisisitiza.
WAZIRI MKUU AONYA MATUMIZI YA RUSHWA UCHAGUZI MKUU
Reviewed by crispaseve
on
07:11
Rating:
Post a Comment