Header AD

CCM YAZOA KATA ZAIDI YA ASILIMIA 72, UCHAGUZI MDOGO WA UDIWANI ULIOFANYIKA JANA

*Yalaani tukio la bomu kwenye kampeni za Chadema
*Nape adai lilipangwa na Chadema wenyewe
DAR ES SALAAM, Tanzania
Matokeo ya Uchaguzi mdogo wa udiwani  uliofanyika  jana, Juni 16, 2013  yanaonyesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepata kata 16 kati ya Kata 22 ulikofanyika uchaguzi huo.

Kata hizo 22 zilizofanya uchaguzi ni Kati ya 26 zilizotangazwa kufanya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi zilizokuwa zimeachwa wazi kutokana na sababu mbalimbali.

Kata nne zilizoko Arusha uchaguzi wake ulisitishwa na Tume ya Uchaguzi kufuatia mlipuko wa mabomu kwenye mkutano wa kampeni za Chadema, ambao uliosababisha vifo vya watu wawili na wengiene kadhaa kujeruhiwa siku moja kabla ya uchaguzi.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye imesema matokeo hayo ambayo imeyakusanya CCM kutoka kwenye maeneo yaliyofanya uchaguzi huo yanaonyesha kuwa ushindi wa CCM ni asilimia  72.72% na vyama vingine hasa Chadema vimepata 27.28%.

"Tunawashukuru sana kote walikoonyesha imani yao kubwa kwa Chama chetu kwa kutupa dhamana ya kuendelea kuwatumikia. CCM inawaahidi utumishi uliotukuka. Hata wale 27.28% walioamua kuwajaribu wenzetu, tunawatakia kila lakheri, kwani wametumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua wanaodhani watawasaidia kufikia malengo yao ya kimaendeleo. Uchaguzi kwenye kata hizi zote umeisha sasa tuwatumikie wananchi", alisema Nape katika taarifa hiyo na kuongeza;

"CCM tunalaani tukio la mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa kampeni wa Chadema mjini Arusha tarehe 15/06/2013, na matukio yanayofanana na hayo katika nchi yetu. Tunawapa pole wale wote walioathirika na tukio hilo".

Alisema ni vizuri serikali ikalichunguza tukio hilo kwa kutumia muda mfupi na kuhakikisha waliohusika wanapatikana na kuchukuliwa hatua zinazostahili.

Pamoja na kulaani na kuitaka serikali kukomesha vitendo hivyo nchini,  Nape amesema ni wakati muafaka kwa vyama vya siasa nchini kujitazama upya kwani kuna kila dalili kuwa tukio hili kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwa ni la kupangwa, inawezekana limepangwa na Chadema wenyewe.

"Hali ya kisiasa jijini Arusha kuelekea uchaguzi huo ilikuwa wazi kuwa wana Arusha walishaamua kuzirudisha kata hizo nne kwa CCM, hasa baada ya kuchoshwa na maandamano na vurugu za kila siku jijini Arusha. Aidha kauli za kukata tamaa za viongozi wa Chadema na vitendo vyao ni dalili tosha kuwa tukio hili lilipangwa na Chadema wenyewe", alisema Nape.

Alisema CCM wanaendelea kusisitiza na kulaani juhudi za wenzao (Chadema) kujaribu kujenga umaarufu wa chama chao juu ya damu za Watanzania na kwamba juhudi hizo zinapaswa kulaaniwa na wazalendo wote ndani na nje ya nchi.

"Tukumbuke asiyekubali kushindwa, si mshindani. Si busara wala uungwana na ni kinyume na utu kutumia majanga ya kutengeneza kama mtaji wa kisiasa", alisema Nape.

Nape alisema CCM pia inalaani kitendo cha viongozi wa Chadema kujaribu kutumia baadhi ya misiba na majeruhi wa tukio hilo la mabomu  kujinufaisha kisiasa na baadaye kuwatelekeza hospitali baadhi yao baada ya kuwaahidi kubeba gharama zote za matibabu na mazishi.

"CCM tunaipongeza serikali kwa kuingilia kati na kuwasaidia waathirika hawa na kuhakikisha wanapata huduma inayostahili", alisema Nape na kuongeza;

"CCM inarudia kueleza masikitiko yake kwa waathirika wa tukio hili la kinyama na kikatili lisilostahili kuvumiliwa hata kidogo. Kama Chama tumeguswa sana na tukio hili pamoja na kulilaani, tunawasihi watanzania tushindane na kutofautiana bila kupigana na kuvunja tunu ya nchi yetu ya amani na utulivu. Katika demokrasia ya vyama vingi swala la kuvumiliana ni swala la msingi sana katika kufikia ukomavu wa demokrasia hiyo".
Reviewed by crispaseve on 03:24 Rating: 5

No comments

Post AD