Header AD

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjOHH5shDbK0teTxfPCXyfZ2Kc7JflqSz_fjG1ykqSVN8G-SkVq8XfKyCLT87wJCvhD3qTvmfrTDuakIaxr5mtL-ZcmNVk112EifrI3TwsKvx5hcUO3cJ38A3YlD1GckxJY_OztOBs0b1Aw/s1600/EDO%252B.jpg 
MBIO za urais wa mwaka 2015 ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinazidi kuchukua sura mpya baada ya kundi linalodaiwa kumuunga mkono Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kumeguka huku baadhi ya washir
ika wake wa Kanda ya Ziwa wakimwibua William Ngeleja.


Ngeleja ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, ni mmoja wa wanasiasa vijana wanaotajwa kuwa wafuasi wa kundi la Lowassa, jambo ambalo linazua hofu kuwa huenda kambi hiyo ikatikisika ikiwa juhudi hizo zitafanikiwa.


Tanzania Daima limedokezwa kuwa vigogo kadhaa waandamizi wa CCM wakiwemo wabunge na mawaziri kutoka Kanda ya Ziwa ambao ni wafuasi wa kundi la Lowassa, wameingia kwenye msuguano wakitaka mgombea urais 2015 atoke kanda hiyo.


Chanzo chetu, kinaeleza kuwa msigano huo ulizua mtafaruku huku baadhi ya wajumbe wakidai kanda hiyo tayari ilikwishampata Rais Julius Nyerere ambaye aliongoza Serikali ya Awamu ya Kwanza na wengine wakisisitiza kuwa ni lazima rais ajaye atoke kanda hiyo.


“Ni katika mikakati mizito hiyo, wajumbe walimpendekeza Ngeleja kuwa mpeperusha bendera hiyo, ingawa yuko na waziri mmoja ambaye anaonekana anatamani nafasi hiyo,” kilisema chanzo chetu.


Ngeleja ambaye pia ni mbunge wa Sengerema, anatajwa kuhudhuria kikao cha siri kilichofanyika eneo la Nyegezi jijini Mwanza hivi karibuni, ambako mjadala mkubwa uliongozwa na wazee maarufu wa Kanda ya Ziwa ukimtaka akubali kuomba kuwa mgombea wa CCM.


Mikakati ya kumwandaa mbunge huyo, inaelezwa kuwa imeanza kwa kumwandalia hafla mbalimbali za kushiriki harambee kwenye nyumba za ibada kama wanavyofanya baadhi ya makada maarufu wa CCM wanaotajwa kuutaka urais, akiwemo Lowassa mwenyewe.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu suala hilo, Ngeleja alisema huu sio muda muafaka kwake kuzungumzia kama atagombea urais au hapana.


Akijibu swali hilo muda mfupi baada ya kumaliza kuhutubia mahafali ya tatu ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lilian, jijini Dar es Salaam juzi ambako alikuwa mgeni rasmi, Ngeleja alisema: “Kuhusu suala la urais bado ni mapema sana kulisemea, kuna taratibu, maadili na kanuni za chama. Tusubiri muda ukifika tutajua nini cha kusema, sijaanza mbio zozote za kuwania nafasi hiyo kubwa.


“Mimi bado nina wajibu wa kuwatumikia wananchi wangu wa Sengerema kama mwakilishi wao, bado nina wajibu wa kutekeleza kazi za kibunge, hivyo kwa sasa kuzungumzia suala la urais bado ni mapema sana.


“Ni kinyume cha kanuni na maadili ya CCM, wakati ukifika kanuni zipo wazi, na maadili yanajulikana kwa wanachama wote, tutajua wakati huo, ndiyo tutasema kama tunagombea au la, ila kuanza kulisemea sasa ni kujiongezea majukumu ambayo hayana tija kwa sasa,” alisema Ngeleja.


Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa endapo kundi hilo litashikilia msimamo wake wa kumpigia debe Ngeleja, litakuwa limedhohofisha nguvu ya Lowassa Kanda ya Ziwa, kwani eneo hilo ni muhimu kutokana na wingi wa kura.


Majina mengi ya vigogo wa CCM yanatajwa kugombea nafasi hiyo nyeti, huku msukumo mkubwa ukiwa upande wa Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya na Spika aliyepita, Samuel Sitta.


Duru za siasa zinadokeza kuwa kundi la Membe linafanya kila jahudi ili kumshawishi Sitta asigombee waweze kuunda nguvu ya pamoja kwa kuwashirikisha pia Prof. Mwandosya, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.


Mei 26 mwaka huu, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akiwa mkoani Iringa, alisisitiza kwamba chama kitamwadhibu bila huruma mwanachama yeyote anayejipitisha katika maeneo mbalimbali na kufanya kampeni za kuwania urais kabla ya wakati.


Makundi hayo, yameleta hofu ya rushwa ndani ya chama, hatua ambayo Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete ameikemea vikali akisema inaweza kuikosesha CCM ushindi mwaka 2015.


Akifunga mafunzo ya makatibu na wenyeviti wa wilaya na mikoa mjini Dodoma juzi, Rais Kikwete alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameanza kujipitisha kwa viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili ya kuwapigia debe ili wawachague katika nafasi mbalimbali za urais ama ubunge.


Alisema kuwa kimsingi kwa sasa wapo watu ambao wameishaanza kuzunguka na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali za kugombea, huku wakipenyeza rushwa jambo ambalo linaendelea kukishushia hadhi chama hicho.


“Kama hatutabadilika katika suala la rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana, na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani.


“Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea sh laki mbili za ‘airtime’ (muda wa mawasiliano), ndugu zangu hatutafika ama wengine watavuka na wengine kukwama,” alisema.

Alisema tatizo la rushwa kwa viongozi wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku hali ambayo inawapotezea imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.

“Viongozi wa chama ndio mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu, nawaombeni tubadilike. Kama tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali, nawaambieni,” alisema. TANZANIA DAIMA.
Reviewed by crispaseve on 23:51 Rating: 5

No comments

Post AD