Rais Jakaya Kikwete na Mama Salma Kikwete Watoa Pole Kwa Mjane na Familia Ya Mwanadiplomasia na Mwanasiasa Mkongwe, Balozi Isack Sepetu
Rais Jakaya
Mrisho Kikwete akiweka saini katika kitabu cha maombolezo ya msiba wa
Balozi Isaac Sepetu alipokwenda nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar
es salaam, kutoa pole. Marehemu Sepetu aliyefariki jana katika jijini
Dar es salaam.
Mama
Salma Kikwete akiweka saini katika kitabu cha maombolezo ya msiba wa
Balozi Isaac Sepetu nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam.
. Marehemu Sepetu aliyefariki jana katika jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji
mjane wa Balozi Isaac Sepetu, Mama Miriam Sepetu, alipokwenda na Mama
Salma nyumbani kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole kwa
mjane huyo na familia ya Marehemu Sepetu aliyefariki jana jijini Dar es
salaam.
Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete
akimfariji mjane wa Balozi Isaac Sepetu alipokwenda nyumbani kwa
marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole kufuatia msiba Marehemu
Sepetu aliyefariki jana katika jijini Dar es salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitoa pole kwa
wanafamilia wa Balozi Isaac Sepetu alipokwenda na Mama Salma nyumbani
kwa marehemu Sinza Mori, Dar es salaam, kutoa pole kufuatia
msiba Marehemu Sepetu aliyefariki jana jijini Dar es salaam.Picha na IKULU
-----
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe kufuatia
kifo cha Mwanadiplomasia na Mwanasiasa Mkongwe, Balozi Isack Sepetu aliyefariki
dunia tarehe 27 Oktoba, 2013 katika Hospitali ya TMJ ya Jijini Dar es Salaam
alikopelekwa kwa matibabu ya ugonjwa wa Kisukari na Kiharusi.
Marehemu Balozi Isack Sepetu, enzi za uhai wake,
aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za juu Serikalini kuanzia miaka ya Sabini
ambapo aliwahi kuteuliwa kuwa Naibu
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Waziri wa
Habari, Utangazaji na Utalii katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Katika miaka ya Tisini, aliteuliwa
kuwa Waziri wa Nchi, Mipango na Uchumi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
iliyoongozwa na Dr. Salmin Amour. Akiwa
Balozi wa Tanzania, Marehemu aliiwakilisha nchi katika Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Congo (DRC) na uliokuwa Muungano
wa Nchi za Kisovieti za Kisoshalisti za Urusi (USSR) ambayo kwa sasa ni Russia.
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa
taarifa za kifo cha Mwanasiasa na Mwanadiplomasia Mashuhuri, Balozi Mstaafu,
Mheshimiwa Isack Sepetu aliyefariki dunia katika Hospitali ya TMJ Jijini Dar es
Salaam alikopelekwa kwa matibabu ya ugonjwa wa Kisukari na Kiharusi tarehe 27
Oktoba, 2013”, amesema Rais Kikwete
katika Salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Balozi
Isack Sepetu, enzi za uhai wake, kama Mwanasiasa na Kiongozi mwenye bidii na
uwezo mkubwa wa uongozi ambaye alidhihirisha uaminifu na uadilifu wake katika nyadhifa mbalimbali alizowahi
kushikilia katika Awamu zote za Uongozi Tanzania Bara na Zanzibar. Balozi Sepetu aliwahi pia kuwa Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nafasi ya kuteuliwa na
Mwenyekiti wa Chama, na kukitumikia Chama kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
“Natambua hata baada ya kustaafu, Marehemu
Balozi Isack Sepetu aliendelea kuaminiwa katika utumishi wake, na hivyo
kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar
(ZIPA) katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt.
Ali Mohamed Shein, na pia Mjumbe wa Bunge la Afrika Mashariki hadi mauti
yalipomkuta”, amesema Rais Kikwete,
na kuongeza,
“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe Salamu
zangu za Rambirambi kwa kumpoteza Mwanadiplomasia na mmoja wa Viongozi shupavu
katika nchi yetu, Marehemu Balozi Isack Sepetu”.
“Kupitia kwako, naomba pia Salamu zangu za
Rambirambi na pole nyingi ziwafikie Wanafamilia ya Marehemu kwa kumpoteza
Kiongozi na Mhimili Madhubuti wa Familia.
Nawaomba wote wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki
kigumu cha maombolezo kwani yote ni mapenzi yake Mola”.
Rais Kikwete amewahakikishia Wanafamilia ya
Marehemu Balozi Isack Sepetu kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha
majonzi kufuatia kifo cha mpendwa wao.
Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema
Peponi Roho ya Marehemu Balozi Isack Sepetu, Amina.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
28 Oktoba, 2013
Reviewed by crispaseve
on
02:38
Rating:
Post a Comment