ANELKA AFUKUZWA WEST BROM
By Israel Saria on March 15, 2014
West Bromwich Albion wamekata shauri la kumfukuza mchezaji mkongwe,
Nicolas Anelka kwa utovu mkubwa wa nidhamu, baada ya mpachika mabao huyo
kutangaza kwamba anaondoka Hawthorns.
West
Brom walishamuonya Anelka, kumsimamisha kucheza mechi tano, ambapo
Chama cha Soka (FA) kilimtoza faini ya £80,000 kwa kuonesha ishara ya
‘quenelle’ ambayo inatafsiriwa kuwa ni ya Kinazi.
Klabu
imedhamiria kumfuta Anelka mwenye umri wa miaka 35 kwenye orodha ya
wachezaji wake kwa kosa hilo na pia kwa kupayuka kwenye vyombo vya
habari bila ruhusa, na wamempa notisi ya siku 14 kama kanuni zinavyotaka
kabla ya kutengua mkataba wake.
Ishara
hiyo hufanywa kwa kunyoosha mkono mmoja chini pamoja na vidole kando ya
mguu wa upande huo huo, huku mkono mwingine ukiwekwa mbele kwenye bega
la mkono ulioshushwa. Ilibuniwa na mwigizaji wa Ufaransa, anakotoka,
Anelka, Dieudonne M’bala M’bala na inasemwa kwamba ni ishara ya kupinga
mamlaka halali.
Anelka
alitumia mtandao wa jamii kuandikia kwamba alikuwa anaondoka klabuni
hapo mara moja kwa madai wameshindwa kufikia mwafaka na klabu, kwa kuwa
amewekewa masharti ambayo hawezi kuyakubali na anataka kutunza heshima
yake na hivyo amekatisha mkataba wake.
West
Brom wanasema usitishaji wa mkataba anaodaiwa kufanya Anelka si wa
kweli na ni batili kwa sababu haujafuata taratibu za kisheria
zinazotakiwa. Masharti klabu iliyotoa ni kwa Anelka kuomba radhi klabu,
washabiki, wadhamini na jamii nzima kwa athari za ishara aliyoitoa
Desemba 28 mwaka jana na kasha akubali faini aliyotozwa.
Mkataba
wa Anelka ambaye amechezea klabu nyingi ulikuwa umalizike mwishoni mwa
msimu huu. Anelka ameichezea Timu ya Taifa ya Ufaransa tangu 1997 hadi
2010 na huko aliwahi kupata masahibu pia.
Katika ngazi ya klabu, Anelka alianzia kwenye timu za vijana za Trappes Saint-Quentin, Clairefontaine na Paris Saint-Germain. Katika
ngazi za wakubwa, kati ya 1996–1997 alikuwa Paris Saint-Germain, kisha
akaenda Arsenal hadi 1999 alipohamia Real Madrid kabla ya kurudi Paris
Saint-Germain mwaka 2000 lakini hakudumu kwani 2001 alipelekwa Liverpool
kwa mkopo hadi 2002.
Anelka
alijiunga na Manchester City 2002 alikocheza hadi 2005 akaenda
Fenerbahçe kwa mwaka mmoja hadi 2006 alipohamia Bolton Wanderers
akacheza hadi 2008 akasajiliwa Chelsea alikokaa hadi 2012 akaenda China
kuchezea Shanghai Shenhua. Hakukaa sana kwa sababu mwaka uliofuata
alikwenda Juventus kwa mkopo na mwaka jana akajiunga West Bromwich
Albion ambao sasa wanamtema.
ANELKA AFUKUZWA WEST BROM
Reviewed by crispaseve
on
03:19
Rating:
Post a Comment