Sekta ya Elimu yapokea Bil. 203 kutoka Benki ya Dunia
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dk. Servacius B. Likwelile akizungumza na waandishi
wa habari (hawapo pichani) wakati wa kusaini mkataba wa kupokea mkopo nafuu kutoka Benki
ya Dunia kwa ajili ya kusaidia sekta ya Elimu, kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia
Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Philippe Dongier.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Sifuni Mchome akifafanua jambo wakati wa hafla
fupi ya kusaini mkataba wa kupokea mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia kuisaidia sekta ya
Elimu nchini, katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dk. Servacius B. Likwelile na kulia ni
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Philippe Dongier.
Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dk. Deo Mtasiwa akichangia wakati wa hafla fupi ya
kusaini mkataba wa kupokea mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kusaidia sekta ya
Elimu, kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Sifuni Mchome.
Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dk. Deo Mtasiwa (kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya
Elimu Prof. Sifuni Mchome (wapili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dk. Servacius B.
Likwelile (wapili kulia) na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Uganda na Burundi
Bw. Philippe Dongier (kulia) wakijadiliana wakati wa kusaini mkataba wa kupokea mkopo
nafuu kutoka Benki ya Dunia kuisaidia sekta yaElimu leo jijini Dar es Salaam.
Picha na Genofeva Matemu – Afisa Mawasiliano Serikalini - WHVUM
Na Rose Masaka - MAELEZO
Serikali ya Tanzania imesaini mkataba wa kupokea mkopo nafuu wa shilingi bilioni 203 kutoka
Benki ya Dunia kwa ajili ya kuendeleza sekta ya elimu katika mpango wake wa matokeo
makubwa sasa(BRN).
Mkataba huo umesainiwa na Katibu mkuu wa wizara ya fedha Dk. Servacus Likwelile huku
ukiwashirikisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elinu na Naibu Katibu Mkuu kutoka TAMISEMI
leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ya kusaini mkataba Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
Dk. Servacus Likwelile ameishukuru Benki ya Dunia kutoa mchango huo kusaidia sekta ya
elimu nchini na kuwataka TAMISEMI na Wizara ya Elimu kusimamia vizuri pesa hizo ili kuleta
mafanikio zaidi kufikia malengo ya matokeo makubwa sasa.
Aidha Dk. Likwelile amewataka waajiri wote katika sekta ya elimu kutoa kipaumbele kwa
walimu ili waweze kuboresha elimu nchini na kuwataka kupeleka majina na akaunti namba za
walimu wote Hazina ili Hazina iweze kuwawekea mishahara yao katika akaunti zao kwa wakati.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Prof. Sifuni Mchome amesema kuwa Wizara ya Elimu
kwa sasa imepiga hatua kubwa katika kufanikisha lengo la matokeo makubwa sasa linalolenga
kukuza na kuendeleza elimu katika ngazi ya shule za msingi na sekondari hivyo fedha hizo
zinatumika kutatua matatizo katika sekta ya elimu ambapo kwa sasa shule nyingi zimeanza
kuonesha matokeo mazuri.
Akitoa mchango wake wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania,
Uganda na Burundi Bw. Philippe Dongier amesema kuwa Benki ya Dunia imeona kuna
umuhimu wa kuisaidia Tanzania katika sekta ya elimu ili kuleta ujuzi na kuvumbua vipaji kwa
vijana wadogo watakaosaidia kuleta maendeleo hapo baadae.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI Dk. Deo Mtasiwa ameahidi kusimamia fedha hizo
kwa ufanisi na kuhakikisha kuwa zinawafikia walengwa wote hadi ngazi ya chini waweze
kufaidika na pesa hizo.
Sekta ya Elimu yapokea Bil. 203 kutoka Benki ya Dunia
Reviewed by crispaseve
on
14:19
Rating:
Post a Comment