Header AD

WATHAMINI MADINI VITO WAASWA KUWA WABUNIFU

 Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), Archard Kalugendo (Kulia), akimwongoza Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Mhandisi Ngosi Mwihava kuingia Ukumbi wa Semina ya Wathamini Madini ya Vito na Almasi nchini, iliyofanyika Agosti 12 na 13 katika Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza.
 Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT) Archard Kalugendo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara Mhandisi Ngosi Mwihava, Kaimu Kamishna wa Madini nchini Mhandisi Ally Samaje na Mkurugenzi wa Utawala na RasilimaliWatu Mrimia Mchomvu, wakijadili jambo muda mfupi kabla ya kuanza kwa Semina ya Wathamini Madini ya Vito na Almasi nchini, iliyofanyika Agosti 12 na 13, 2015 katika Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza.
Meza Kuu – wakiwa katika Semina ya Wathamini Madini ya Vito na Almasi nchini. Semina ilifanyika Agosti 12 na 13, 2015 katika Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza. Kutoka Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), Archard Kalugendo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara Mhandisi Ngosi Mwihava, Kaimu Kamishna wa Madini Ally Samaje na Mkurugenzi wa Utawala na RasilimaliWatu Mrimia Mchomvu.

WATHAMINI MADINI VITO WAASWA KUWA WABUNIFU
Na Veronica Simba - Mwanza

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava amewataka Wathamini Madini ya Vito na Almasi nchini kuendelea kuwa wabunifu ili kutafuta majibu na suluhisho kwa changamoto zinazoikabili tasnia ya vito nchini.

Aliyasema hayo alipokuwa akifungua Semina ya Nne ya Wathamini Madini ya Vito na Almasi nchini iliyofanyika Agosti 12 na 13, mwaka huu katika Ukumbi wa Hoteli ya Gold Crest, jijini Mwanza.

Mwihava alisema kuwa changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia hiyo zitaweza kuondolewa endapo watumishi katika kada hiyo watajituma kufanya kazi kwa uaminifu, weledi na ubunifu wa hali juu. “Napenda kuwakumbusha kwamba Watanzania wanataka kuona faida stahiki kutoka katika sekta ya madini hasa itokanayo na almasi na vito vingine; kadhalika hata mimi nataka kuona matokeo yanayopimika na malengo hayo kutimia na hata kuzidi viwango wanavyotarajia,” alisema Kaimu Katibu Mkuu.

Akifafanua zaidi, Mwihava aliongeza kuwa angependa kuona Soko la uhakika kwa Madini yanayopatikana nchini hususan Almasi na Vito ili Watanzania wanaojishughulisha na biashara hiyo wajue utaratibu wote.

Alisema kuwa angependa kuona wataalam hao wakitumia ipasavyo mitandao iliyopo katika kuwavutia wafanyabiashara na wakataji wa vito kuja nchini kununua na kuwekeza katika tasnia husika.

Aidha, Mwihava aliongeza kuwa angependa kuona wataalamu hao wa Madini ya vito na almasi wakitumia ujuzi wao katika kuwasaidia wadau wa tasnia husika kupata tafsiri sahihi na kuzingatia Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na Kanuni zake.

“Nawaagiza mzingatie maadili na miongozo ya kazi katika utekelezaji wa majukumu yenu; msome na kuzingatia Sera ya Madini ya mwaka 2009, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na kanuni zake na Mkataba wa Huduma kwa Mteja,” alisisitiza Mwihava.

Vilevile, Kaimu Katibu Mkuu alitahadharisha kuwa yeyote atakayefanya kazi kinyume na matarajio, kwa kupokea rushwa, wizi au kufanya jambo jingine lolote kinyume na maadili ya utumishi wa Umma na kusababisha kuathiri juhudi zinazofanywa na Wizara, hatavumiliwa.

Akizungumzia mchango wa Serikali katika kuinua tasnia ya Madini ya vito na almasi, Mwihava alisema Wizara imeahidi kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya madini ili kuongeza uwezo kwa Serikali kujitegemea katika bajeti yake.

“Endapo azma hii itafanikiwa, uchumi wetu kama Taifa utakua, fursa za ajira zitaongezeka na kipato cha Watumishi kitaboreshwa. Aidha, wananchi watapata huduma stahiki, muingiliano wa biashara utakua na hivyo kuchochea ufikiaji wa malengo ya Dira ya Taifa, yaani kuwa nchi yenye kipato cha kati ifikapo 2025.”

Alisisitiza kuwa suala muhimu zaidi ni kuhakikisha Watanzania wanaridhishwa na utendaji kazi wa watumishi wa Serikali hususan walioko katika kada husika na kuwaonyesha Watanzania kwamba wana uwezo wa kusimamia sekta husika kwa niaba yao na pia wananchi waone kwa maneno na vitendo kwamba kazi hiyo inafanyika vizuri.

Mwihava alihitimisha kwa kuwataka washiriki wa semina hiyo kuitumia kama fursa muhimu ya kujitathmini, kubadilishana uzoefu, kupeana mbinu za utendaji bora, kutafuta majibu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili na kukumbushana maadili mema ya kazi na utumishi wa umma.

Alitoa changamoto kuwa anatarajia baada ya semina husika, wataalam hao wa sekta ya Madini vito na almasi watakuja na mkakati wa kuboresha ukusanyaji mapato ya Serikali kutoka katika tasnia ya almasi na vito, ili kuisadia Wizara kufikia malengo ya makusanyo na kuboresha utendaji wao.
WATHAMINI MADINI VITO WAASWA KUWA WABUNIFU WATHAMINI MADINI VITO WAASWA KUWA WABUNIFU Reviewed by crispaseve on 11:46 Rating: 5

No comments

Post AD