HOSPITALI KUU YA NANJING NCHINI CHINA YAANZISHA MAFUNZO YA MIAKA MITATU KWA MADAKTARI NA WAUGUZI 12 WA ZANZIBAR
Mkurugenzi
wa Idara ya Elimu na Daktari Mkuu wa Hospitali ya Nanjing Dkt. Zhou
Yujie akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi mmoja vitabu
vitakavyotumika kuendesha mafunzo ya madaktari na wauguzi wa Zanzibar.
Dkt.
Zhou Yujie ambae ni Mkurugenzi na Daktari Mkuu wa Hospitali ya Nanjing
akizungumza na madaktari na wauguzi watakaoshiriki mafunzo ya miaka
mitatu nchini China na Zanzibar wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo
uliofanyika Hospitali ya Mnazi mmoja.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi mmoja Dkt. Ali Salum Ali akizindua
mafunzo ya madaktari na wauguzi yatakayofanyika katika Hospitali ya
Nanjing na Hospitali kuu ya Mnazi mmoja Mjini Zanzibar, (kushoto) ni
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Daktari Mkuu wa Hospitali kuu ya Jimbo
la Nanjing
Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar
…………………………………………………………………………….
Jimbo
la Nanjing Nchini China limeongeza ushirikiano mpya na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha mpango maalumu wa mafunzo ya miaka
mitatu kwa madaktari na wauguzi wa Hospitali kuu ya Mnazi mmoja.
Mafunzo
hayo yatakayofanyika kwa zamu katika Hospitali ya Mnazi mmoja na
Hospitali ya Nanjing yatawashirikisha madaktari sita na wauguzi sita
kutoka sehemu ya wazazi.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi mmoja Dkt. Ali Salum Ali ameyazindua
rasmi mafunzo hayo na kueleza kuwa wamejiandaa vizuri ili kuhakikisha
mafunzo hayo yanafanyika kwa ufanisi.
Amesema
mafunzo hayo yanatarajiwa kuwaongezea uwezo madaktari wazalendo na
wauguzi katika kukabiliana na vifo vya mama wajawazito wakati wa
kujifungua na watoto wachanga.
Dkt.
Ali Salum amesema katika mpango huo, madaktari bingwa kutoka Hospitali
ya Nanjing watakaoendesha mafunzo hayo wataambatana na wanafunzi wao kwa
awamu katika hospitali ya Jimbo hilo na Hospitali ya Mnazi mmoja.
Ameongeza
lengo la kuendesha mafunzo hayo katika vituo viwili tofauti, China na
Zanzibar, ni kuwapa fursa madaktari na wauguzi kujifunza kwa kutumia
mazingira ya nyumbani na mazingira ya kigeni ambapo yatakuwa na ufanisi
zaidi.
“Mara
nyingi vijana wetu wanapokwenda nje ya nchi kwa mafunzo hutumia
teknolojia ya huko na wanaporudi wanatumia teknolojia ya kwetu hivyo
baadhi ya wakati wanajikuta wapo njia panda,” aliongeza Mkurugenzi
Mtendaji.
Amesisitiza
kwamba mpango huo mpya wa mafunzo utatoa fursa kwa madaktari na
wauguzi wengi kutoka Zanzibar kupata mafunzo kwa wakati mmoja na
utapunguza gharama za kuwasafirisha watu wachache kwa gharama kubwa.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi mmoja alisema baada ya madaktari na
wauguzi hao kumaliza mafunzo yao watasaidia kutoa huduma katika
Hospitali na vituo vyengine vya afya vya Zanzibar.
Mkurugenzi
wa Idara ya Elimu ambae pia ni daktari mkuu wa Hospitali ya Nanjing
Dkt. Zhou Yujie amesema tayari wameandaa mtaala na kufanya uteuzi wa
madaktari 20 watakaosimamia mafunzo hayo.
Katika
uzinduzi wa mafunzo hayo uliofanyika Hospitali ya Mnazi mmoja, Dkt.
Zhou alimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji vitabu vitakavyotumika katika
kuendesha mafunzo hayo.
Alisema
katika mafunzo hayo wakufunzi kutoka Hospitali ya Nanjing
watashirikiana na wanafunzi wao kuwafanyia matibabu ya kawaida na
upasua wagonjwa ikiwa ni miongoni mwa mafunzo yao.
Amekumbusha
kuwa uhusiano wa sekta ya afya kati ya Jimbo la Nanjing na Zanzibar
ulianza tokea mwaka 1964 kwa kuleta madaktari katika Hospitali ya Mnazi
mmoja na Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani na mpango wa sasa wa mafunzo
ya miaka mitatu ni muendelezo wa historia hiyo.
HOSPITALI KUU YA NANJING NCHINI CHINA YAANZISHA MAFUNZO YA MIAKA MITATU KWA MADAKTARI NA WAUGUZI 12 WA ZANZIBAR
Reviewed by crispaseve
on
01:27
Rating:
Reviewed by crispaseve
on
01:27
Rating:


Post a Comment