MFUMO WA STAKABADHI GHALANI MKOMBOZI KWA WAKULIMA.
Jovina Bujulu- MAELEZO
Kuwepo
na mfumo wa stakabadhi ghalani kumekuwa ni mkombozi pekee kwa wakulima
wadogo na wa kati kwa kuwawezesha kupata bei nzuri ya mazao yao,
ukilinganisha na bei zilizokuwa zinatolewa na wafanyabiashara
wanaponunua mazao yakiwa shambani kwa kutumia vipimo ambavyo sio sahihi.
Taarifa
iliyotolewa na bodi ya usimamizi wa Stakabadhi za Ghala imesema kuwa
kabla ya mfumo huo kuanza wakulima walikuwa wakipunjwa bei ya mazao na
wafanyabiashara na kutolea mfano zao la korosho ambapo katika msimu wa
2015/2016, kilo moja ya korosho ilinunuliwa kwa shilingi 2900 na msimu
wa 2016/2017 bei ilipanda na kufikia shilingi 4,000 kwa kilo ambazo ni
sawa na ongezeko la asilimia 15.9
Mfumo
huo umewanufaisha wakulima kwa kutumia ghala ambazo ziliachwa kwa muda
mrefu bila matumizi ambazo zimekuwa na tija kwa wakulima.
Kupitia
ghala hizo zenye ujazo wa kuanzia tani 200 hadi 5000 na kuendelea
wameweza kuhifadhi mazao yao vizuri na kwa ubora unaotakiwa kwa matumizi
ya sasa nay a baadaye.
Aidha,
mfumo huo umeongeza ajira kwa wakina mama na vijana hasa katika maeneo
ya kuchambua, kupokea na kupanga mazao ghalani. Vijana wengi wameajiriwa
kwa kazi ya kushusha, kupanga na kupakia mazao na wameweza kujiajiri
katika kilimo baada ya kuona mfumo huo unavyofanya kazi vizuri na kuwa
na uhakika wa soko la mazao yao.
Wakulima
pia wamepata mafanikio kwa kuwa na uhakika wa vipimo vya mazao yao
yanayohifadhiwa ghalani kupimwa kwa kilogramu na si vinginevyo ambapo
kabla ya mfumo huo wakulima walikuwa wakiibiwa mazao yao kutokana na
matumizi ya vipimo ambavyo si sahihi.
Kwa
kuhifadhi mazao yao katika ghala zenye leseni, wakulima wamekuwa
wanatumia mazao hayo kama dhamana ya kupata mikopo kutoka katika taasisi
mbalimbali za fedha. Hii imewezekana kutokana na wakulima hao kujiunga
katika umoja kupitia vikundi au vyama vya ushirika .
Wafanyabiashara
pia wameneemeka na mfumo huu, ambapo kwa sasa wameweza kupunguza
gharama za kufuata mazao maeneo mbalimbali mazao yanapatikana kwa wingi
badala yake mazao hayo wanayapata katika eneo moja kkwenye ghala
zilizosajiliwa na hivyo kuondoa hatari ya kuibiwa pesa zao na madalali
wasio waaminifu.
Mfumo
huo pia umekuwa na faida kwa bodi za mazao katika kuandaa bajeti za
mahitaji ya pembejeo na kuongeza ili kuboresha na kuongeza uzalishaji.
Aidha,
mfumo huo umechochea na kuharakisha uanzishwaji wa soko la bidhaa
nchini, kutokana na kuwepo kwa bidhaa zenye ubora na zinazopatikana kwa
wakati. Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, inatoa wito kwa
wakulima kuunga mkono uhamasishaji wa matumizi ya soko hilo ili kuongeza
tija na kasi ya kukuza biashara ya mazao ya kilimo hapa nchini.
Mfuko
wa Stakabadhi Ghalani ulianza mwaka 2000 ukifadhiliwa na Mfuko wa
Kimataifa wa Bidhaa. Lengo la mfuko huo ni kuwezesha wakulima kufaidika
na ongezeko la bei katika msimu wa mazao, kuongeza mapato ya wakulima na
kuboresha kipato chao ikiwa ni pamoja na kuwapa wakulima nguvu ya soko
kwa kuhamasisha utumiaji wa vikundi vya wakulima na ushirika.
MFUMO WA STAKABADHI GHALANI MKOMBOZI KWA WAKULIMA.
Reviewed by crispaseve
on
02:41
Rating:
Post a Comment