Header AD

LULU KUFIKISHWA TENA MAHAKAMANI JUNI 18.


Mwigizaji wa filamu, Elizabeth Michael 'Lulu' anayekabiliwa na kesi ya kumuua mwigizaji mwenzake, Steven Kanumba, akisindikizwa na askari Magereza kuingia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwa ajili ya kusomewa mashitaka  yake. Kesi hiyo imehairishwa hadi juni 18. (PICHA NA DOTTO MWAIBALE)

KESI ya mauaji inayomkabili msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ imeahirishwa hadi Juni 18 mwaka huu,  kwa sababu upelelezi wa shauri hilo bado haujakamailika.

Wakili wa Serikali Peter Sekwao alidai kuwa kesi hiyo imekuja kwa kutajwa, pia alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Baada ya kudai hivyo Hakimu Mkazi , Agustina Mmbando wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 18 mwaka huu, ambapo itakuja kwa kutajwa.

Awali  Mei 7 mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi la mawakili wa upande wa  utetezi katika kesi inayomkabili Lulu kuwa mahakama
 imuone ana miaka chini ya miaka18.

Hivyo mawakili hao wakiongozwa na wakili  Kennedy Fungamtama  waliomba mahakama itambue hivyo, hivyo kesi hiyo ihamishiwe katika mahakama ya watoto.

Wakati Fungamtama akiwakilisha ombi hilo,aliiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo ana miaka 17 hivyo shauri lake linatakiwa kuhamishiwa katika mahakama ya watoto.

Sanjari na hilo alidai kuwa upande wa mashtaka haujawasilisha mahakamani hapo pingamizi lolote kuhusu umri wa miaka hiyo hata pale mshtakiwa mwenyewe alipoieleza mahakama kuwa ana miaka 17 badala ya 18.

Fungamtama aliwasilisha cheti cha kuzaliwa  alichodai kuwa cha mshtakiwa ili mahakama hiyo iweze kujiridhisha kuhusu umei wa mshtakiwa huyo kinachoonesha mwaka na mahali alipozaliwa.

Hata hivyo wakili wa serikali katika kesi hiyo Elizabert Kaganda alipinga ombi hilo na kudai kuwa ameshtushwa na ombi hilo kwakuwa kesi imekuja kutajwa na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza ombi lolote kwakuwa kesi hiyo haitasikilizwa mahakamani hapo.

Kaganda alidai kuwa kesi hiyo bado ipo katika hatua ya upelelezi ambao bado haujakamilika ana kwamba miongozi mwa vitu wanavyovichunguza ni pamoja na umri wa mshtakiwa huyo.

Pia Kaganda alidai kuwa katika cheti cha kuzaliwa kilichooneshwa mahakamani hapo na Fungamtama alidai kuwa hawawezi kukiamini kwa kuwa ni kina jina la Dayana Elizabert wakati mshtakiwa anaitwa Elizabert Michael.

Akitoa uwamuzi wa maombi hayo hakimu Mmbando aliutaka upande wa utetezi kusubiri kesi hiyo itakapowasilishwa katika mahakama kuu ndipo wawasilishhe maombi hayo kwakuwa mahakama hiyo hivi sasa haina mamlaka.

Katika kesi hiyo Lulu anashtakiwa kwa kosa la mauwaji ya msanii nguli wa Filamu nchini, Steven Kanumba.
Reviewed by crispaseve on 03:22 Rating: 5

No comments

Post AD