MASHABIKI IVORY COAST WAIDHARAU TAIFA STARS.
Edo Kumwembe, Abidjan MASHABIKI katika mitaa mbalimbali ya jiji la Abidjan wameonekana kuidharau timu ya soka ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kwa kuonyesha hewani vidole vitatu ikiwa ni ishara kwamba timu yao ya taifa itashinda mabao 3-0. Katika mitaa mbalimbali ya Abidjan na katika hoteli ya Ibis Plateau iliyopo katikati ya jiji la Abidjan, mashabiki wa Ivory Coast ambayo ilichapwa kwa matuta na timu ya Zambia katika mechi ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Gabon walionyesha kutoiheshimu Stars huku wakitaja majina ya wachezaji wao nyota kama Didier Drogba na kuashiria vidole vitatu hewani. “Tutashinda mabao matatu na yote atafunga Drogba. Hamtuwezi hata kidogo sisi Tembo. Tanzania ni timu ndogo na timu ndogo huwa inafungwa na timu kubwa ugenini labda kama mngekuwa nyumbani kwenu.” Alisema shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Alina Keita kwa lugha ya Kifaransa kupitia mkalimani ambaye ni Mtanzania Juma Abdul aliyeishi Ivory Coast kwa miaka 11 sasa. Mhudumu wa kike katika hoteli ya Ibis Plateau, Gladys Konne alisema ana uhakika Ivory Coast itaifunga Stars katika uwanja wa Felix Houpheut-Boigny, lakini akakiri kwamba matokeo kati ya Ivory Coast na Zambia katika pambano la fainali bado yanamsumbua akilini na anaamini kuwa timu ndogo inaweza kuifunga timu kubwa. Katika kivutio kingine, msafara wa Taifa Stars ulishangazwa na namna ambavyo wanajeshi wa Ivory Coast walivyowasindikiza kufika hotelini baada ya kuwapokea katika uwanja wa ndege wa Felix Houpheut-Boigny mara baada ya kutua juzi Jioni. Wanajeshi zaidi ya 30 walipanda katika lori la wazi wakiwa na silaha za kivita wakiusindikiza masafara wa Stars katika mitaa ya Abidjan wakiwa nyuma ya basi la Stars. Kwa mujibu wa habari za ndani, hali hiyo imetokana na historia ya vurugu na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyolikumba taifa hilo katika miaka ya karibuni hasa baada ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Laurent Gbagbo kukataa kuachia madaraka kwa rais mpya wa nchi hiyo aliyeshinda uchaguzi, Alassane Quattara mwanzoni mwa mwaka jana. Chanzo Mwananchi. |
Reviewed by crispaseve
on
11:28
Rating:


Post a Comment