Header AD

TWIGA STARS LAZIMA KIELEWEKE LEO MBELE YA ETHIOPIA.

MBIO za kuamua nchi gani itaungana na mwenyeji wa Fainali za Kombe la Matiafa ya Afrika kwa wanawake, Equatorial Guinea na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), zinafikia tamati wikiendi hii, huku timu ya Taifa ya Tanzania (Twiga Stars) ikishuka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuumana na Ethiopia.

Mechi sita zinatarajia kuchezwa, ambako pia zitahusisha mabingwa watetezi Nigeria, Ivory Coast na Afrika Kusini ambazo ni kama tayari zina hatua moja mbele kuelekea kufuzu kufuatia kushinda mzuri katika mechi zao za kwanza.


Ivory Coast iko mbele kwa mabao 7-0 dhidi ya Msumbiji, wakati Nigeria itaikaribisha Zimbabwe ikiwa na ushindi wa mabao 2-0 mkononi waliuopata ugenini mjini Harare.


Banyana Banyana ya Afrika Kusini iko mbele kwa ushindi wa mabao 3-1 walioupata dhidi ya Zambia iliyokuwa nyumbani katika mchezo wa kwanza, huku Tanzania ikihitaji ushindi baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza ugenini Ethiopia.


Kocha wa Twiga Stars, Charles Mkwasa amewaambia waandishi wa habari jana kuwa kikosi chake iko kamili tayari kwa mchezo huo na kuahidi ushindi utakaowapeleka kwenye fainali hizo.


Mkwasa alisema tayari ameshayafanyia kazi mapungufu yaliyopelekea kupoteza mchezo wa kwanza na faraja kubwa ni hatua yake ya kuongeza baadhi ya wachezaji kwenye kikosi hicho.


"Tunafahamu umuhimu wa mchezo huu, ni lazima tushinde ili tuweze kufuzu. Tumejianda vizuri kwa mchezo, wachezaji wangu wana ari na moyo wa ushindi," alisema Mkwasa.


"Kuna makosa ambayo yalijitokeza kwenye mechi yetu ya kwanza lakini tayari nimeshayafanyia kazi na hakuna shaka makosa hayo hayatajitokeza tena leo," aliongeza Mkwasa.


"Ushindi leo ni lazima, ningependa kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuja kutuunga mkono ili tuweze kukamilisha safari ya kwenda kucheza fainali hizi," alisema Mkwasa.


"Wengi mlijitokeza Taifa Stars ilipocheza na Gambia, nawaomba mjitokeza tena kwa wingi katika mchezo wetu dhidi ya Ethiopia," alisema zaidi.


Kwa upande wake, kocha wa Ethiopia, Abrehem Haimanot alisema kikosi chake kimekuja Tanzania kuendeleza ushindi walioupata katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita.


Haimanot alisema anafahamu anakwenda kucheza na na timu nzuri na yenye ushindani mkubwa, na zaidi ya yote itakuwa kwenye Uwanja wa nyumbani ikishangiliwa sana.


"Tanzania ina wachezaji wazuri tunafahamu hilo, lakini ushindi kwetu ni jambo la lazima. Safari yetu ndefu siyo kuisindikiza Stars, bali wao kutusindikiza sisi," alisema.


Katika hatua nyingine Benki ya Posta, imetoa Sh3 milioni kwa Twiga Stars ikiwa ni sehemu ya hamasa kwa wachezaji ili waweze kushinda mechi hiyo.


Aidha, Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mwantum Mahiza amewataka wachezaji Twiga Stars kucheza kwa nidhamu na kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo.



Mechi na matokeo ya awali:

Tanzania vs Ethiopia (1-2)
Msumbiji vs Ivory Coast (0-7)
Afrika Kusini vs Zambia (3-1)
Senegal vs Morocco (0-0)
Nigeria vs Zimbabwe (2-0)
Cameroon vs Ghana (1-1)
Reviewed by crispaseve on 05:16 Rating: 5

No comments

Post AD