Header AD

SOMO LETU LA 3 LEO JUMATATU: VIFAA VITUMIKAVYO KUTAFUTA CHANELI KATIKA MADISHI NA AINA ZA MADISHI YA KUTUMIA KUPATA CHANNEL NYINGI


Jumatatu iliyopita ilikua ni siku ambayo tulitoa somo la pili Jinsi ya Kulisoma BOFYA HAPA na leo tunaendelea na somo la tatu kama ambavyo linajieleza hapo chini
 
Vifaa muhimu vinavyohitajika wakati wa kutafuta chaneli kutoka katika satelaiti yoyote:

  1. Spectrum Analyzer inayoweza kuonyesha mawimbi (electromagnetic radiations) hadi 15GHz, 20GHz au 30GHz (spectrum analyzer huonesha picha ya mawimbi, masafa yake, nguvu iliyoko katika mawimbi na hata kama mawimbi yanaingiliana yanaonekana). Kwa ufupi Spectrum Analyzer huonesha kila kitu (picha kamili ya mawimbi katika masafa mbalimbali).
Mitambo hapo juu inaitwa Spectrum Analyzer. Vifaa hivi hutusaidia kuona, kusikia, kupima na kuchunguza tabia za mawimbi katika "Electromagnetic Spectrum". Zipo Spectrum Analyzer za uwezo tofauti wa kuona mawimbi tokea 20Hz hadi 3GHz, 10GHz, 26GHz, 67GHz na kuendelea.

  1. Field Strength meter (huonesha nguvu ya mawimbi husika).

  1. Satellite Finder (ina mita na hutoa mlio fulani ambao wakati unatafuta signal mlio huo huongezeka kadri mawimbi ya masafa unayoyatafuta yanavyoongezeka). Hufungwa kati ya (LNB/ LNC (Low Noise Block) / Low Noise Converter respectively).

  1. Compass kwa ajili ya kuonesha uelekeo wa dishi (kuzungusha dishi kuelekea magharibi, kaskazini mashariki, kaskazini magharibi, mashariki, kusini mashariki, kaskazini mashariki, kusini, kaskazini, kutegemea sehemu ulipo duniani kutoka satelaiti unayoitafuta. Kwa lugha ya kitaalamu "Azimuth Angle". Dishi lazima lielekezwe satelaiti ilipo. Mfano kama satelaiti ni Intelsat 906 (nyuzi 64) dishi linaelekea Kaskazini Mashariki (tukiwa Dar es Salaam) kwa sababu satelaiti hiyo ipo juu ya bahari ya Hindi jirani na maeneo ya India. Kwa maeneo mengine dishi linaweza kuelekea uelekeo tofauti kwa sababu inategemea anayefunga dishi alipo katika uso wa dunia kutoka katika satelaiti hiyo.

  1. Inclinometer kwa ajili ya kupima ulalo au mwinuko wa dishi  "elevation angle" (mzunguko wa dishi juu na chini). 

  1. Pimamaji. Pimamaji ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba dishi linakaa katika msawazo (0 - level) na kama unafunga katika bomba hakikisha bomba linasimama wima (upright)  nyuzi 90).

  1. TV ndogo kwa ajili ya kuonesha mawimbi (kama unatumia Satellite Finder, King'amuzi au Risiva ya kawaida).

  1. Vifaa vinginevyo (toolbox).

Angalizo:
Kama huna Spectrum Analyzer unaweza kutumia Field Strength Meter (Signal Strength Meter) kama huna vyote hapo unaweza kutumia Satellite Finder pamoja na King'amuzi au satelaiti risiva ya aina yoyote.

Kutafuta chaneli za Multichoice/Dstv.

Wakati wa kutafuta chaneli (signal) za Multichoice/ Dstv mafundi wengi hutumia ving'amuzi vya Multichoice/Dstv.

Ukifika site bila King'amuzi cha Dstv ufanyeje?

Wazo mbadala:
Unaweza kutumia satelaiti risiva yoyote; wakati wa kutafuta chaneli chagua satelaiti yoyote ambayo imesetiwa (satelite setup) katika Masafa ya LNB: Low Frequency 9750MHz na High Frequency 10700MHz. Haya ni masafa anayotengenezwa na sakiti inayoitwa "local oscillator" iliyopo katika king'amuzi au risiva.

Kabla ya yote tuone hatua muhimu ambayo hufanyika katika LNB:


LNB ni nini?

Kirefu cha LNB ni "Low Noise Block". Ni kifaa kinachofungwa katikati ya dishi (at the focus of the dish) kwa madishi yanayoitwa Prime Focus Dishes (Madishi ya C Band; madishi ya futi sita na kuendelea) na pembeni mwa dishi kwa madishi ya Ku Band (Offset dishes; madishi ya sentimita 60 na kuendelea). Kazi yake kubwa ni kupokea mawimbi kutoka katika satelaiti, kuyaongeza nguvu, kuyapunguza masafa (downconvert), na kisha kuyapeleka katika king'amuzi au risiva ambayo huyatengeza na kutoa RF (Radio Frequency), Video Baseband (Video Signal) na Sauti (Audio). Mawimbi yaliyopatikana katika king'amuzi au risiva yakiunganishwa katika televisheni tunapata picha na sauti.


Katika Ku Band masafa televisheni na redio yanayofika katika dishi ni kuanzia 10.6GHz au 10.7GHz hadi 12.75GHz.


Aina za LNB.

Zipo LNB za aina kuu mbili kwa kuzitofautisha kutokana na Masafa.
  1. LNB za Ku Band na
  2. LNB za C Band.

a) LNB za Ku Band (LNB zilizoandikwa 10.7GHz hadi 12.75GHz)
; baadhi ya LNB za Ku Band   zimeandikwa 10.6GHz hadi 12.75GHz. Ni LNB zinazofanya kazi ya kupokea mawimbi ya Televisheni / Redio kutoka katika satelaiti kuanzia 10.6GHz /10.7GHz  hadi 12.75GHz.
   
 Kuna aina mbalimbali za LNB za Ku Band baadhi yake ni LNB zinazotoa "output moja",      "output mbili", "output nne", "output nane", Quatro na nyinginezo. LNB za Quatro haziwezi kuunganishwa moja kwa moja katika king'amuzi au risiva; inabidi ziunganishwe katika vifaa hivyo kupitia vifaa     vinavyoitwa "multiswitch"

Dishi la Ku Band

 
Picha hapo juu inaonesha dishi la kupokea mawasiliano ya televisheni katika Ku Band. Yapo madishi ya ukubwa tofauti kuanzia kipenyo cha sentimita 30, 45, 60, 90, 120 na kuendelea. Katika ukanda wetu (Tanzania na nchi za jirani) tunatumia zaidi madishi ya sentimita 90cm. Ni vizuri zaidi kutumia Madishi ya kipenyo cha sentimita 120cm kwa sababu mawimbi katika masafa ya Ku Band huathiriwa sana na mvua (hunyonywa na matone ya mvua) na kusababisha picha kukatikakatika wakati na wakati mwingine picha kupotea kabisa wakati mvua zinaponyesha.
LNB za Ku Band
LNB ya Ku Band ya njia moja (Single output Ku Band LNB)

LNB ya Ku Band ya njia nane (Eight output octo LNB). Kila njia "Output" inajitegemea.


b) LNB za C Band:

    Ni LNB zinazofanya kazi ya kupokea mawimbi ya Televisheni / Redio kutoka katika
    satelaiti kuanzia 3.6GHz hadi 4.2GHz. Zipo za aina nyingi mfano
       1. Single Solution C Band LNB. Hii ni LNB yenye output moja lakini inauwezo wa kugawa
           mawimbi (satellite signal kwa zaidi ya risiva moja).
       2. LNB za output moja, output mbili, output nne na kuendelea.


LNB za C Band:


 LNB ya C Band inayotoa njia moja (1 output LNB)

LNB ya C Band inayotoa njia mbili (2 output LNB)

Kwa kawaida mawimbi yanayotoka katika satelaiti yana masafa makubwa sana kiasi kwamba ni shida kupita katika waya ( kadri masafa yanavyoongezeka ndivyo inavyozidi kuwa rahisi kwa mawimbi kupotea katika waya) hivyo lazima masafa hayo yapunguzwe ndio yaweze kupita katika waya.

LNB ya Ku Band (10.6GHz / 10.7 hadi 12.75GHz) hufanya kazi sawa na LNB za C Band tofauti yake ni kwamba LNB za Ku Band zinafanya kazi katika masafa makubwa ukilinganisha na LNB za C Band (3.6GHz hadi 4.2GHz).


Jambo muhimu sana la kuzingatiwa.
Mawimbi yanayotumwa katika satelaiti na kupokelewa na madishi majumbani na maofisini mwetu huwa yana namna yanavyokaa. Kuna yanayokuja katika mfumo wa koili (coil) na yanayokuja katika mstari myoofu ambayo yanakuja wima (Vertically Polarized) na mengine yanakuja yakiwa yamelala (Horizontally Polarized)

Mawimbi yanayokuja mfumo wa koili:
Yanakuja katika coil za aina mbili tofauti ambazo ni:
a) Right Circular na
b) Left Circular. 

Hii inamaana vituo vya televisheni /radio hutuma katika satelaiti mawimbi ambayo husafiri katika mfumo wa:
a) Left Circular Polarized
b) Right Circular Polarized
c) Horizontal
d) Vertical

Mfano:
Tuchukue mfano wa chaneli za C Band ambazo tunazipata kutoka katika satelaiti inayoitwa IS 906 iliyopo nyuzi za longitudo 64.2 Mashariki mwa mstari wa Greenwich ambayo tunaitumia sana hapa kupokea mawasiliano ya televisheni na redio ya vituo vilivyoko hapa kwetu ambavyo ni:
Chaneli 10, TBC, Startv, ITV, Capital, EATV, TVM (Mozambique), na nyinginezo.

ITV, CAPITAL na EATV mawimbi yao yanabebwa na Frequency Moja (3641MHz) na yanakuja katika mfumo wa koili (coil) katika kundi la "Right Circular - R" na TBC (3891MHz), Startv (3884MHz) mawimbi yao ni "Left Circular (L)"

LNB hupokea mawimbi yote (Left Circular Polarized, Right Circular Polarized, Vertical Polarized na Horizontal Polarized) ila hufanyia kazi mawimbi ya aina mbili tu ambayo ni Vertical Polarized na Horizontal Polarized.

Kuna kifaa (kinafanana na kipande cha sabuni) mbacho wakati wa kufunga dishi lazima ukichomeke ndani ya LNB (ndani ya feedhorn) kwa kukatiza katikakati ya antena mbili zilizoko katika LNB ya C Band au unakichomeka kilale sambamba na antena mbili zilizoko katika LNB (antena moja ni kwa vertically polarized waves na nyingine ni kwa horizontally polarized waves). Kifaa hiki kinaitwa "Teflon Slab"

"Teflon Slab" hubadilisha mawimbi yanapokatiza katika feedhorn;  Right Circular polarized waves hubadilishwa kuwa "Vertical" na Left Circular polarized waves hubadilishwa kuwa "Horizontal".

Kwa mawimbi ambayo ni "linear" (Vertical na Horizontal) hakuna haja ya kuweka Teflon Slab katika LNB.
 
Mfano chaneli za Asia tunazozipata toka satelaiti IS 10 iliyopo nyuzi za longitudo 68.6 Mashariki mwa mstari wa Greenwich haziitaji kuweka Teflon Slab katika LNB yake. 
 
Mawimbi ya ITV, CAPITAL, EATV ambayo ni Right Circular hubadilishwa na Teflon Slab  kuwa Vertical na Mawimbi ya TBC, Startv, ambayo ni Left Circular hubadilishwa na kuwa Horizontal.
 
Somo litaendelea Jumatatu ijayo Hapahapa Lukaza Blog Na Muda ni Uleule saa mbili na Nusu Asubuhi Tunakaribisha maswali ambapo tutamtumia Mtaalamu wetu Aweze kujibu. Unaweza Kututumia Maoni,Ushauri na Maswali juu ya MAda hii.
 
Endelea Kuwa na Lukaza Blog 24/7  @ LUKAZA BLOG
Reviewed by crispaseve on 08:35 Rating: 5

No comments

Post AD