Header AD

 Maparachichi yanayouzwa na SACOMA toka Kenya
Kutoka Kulia Bw. Nigel Shepherd, Mh. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Bi. Perez Ochieng, Balozi  Peter Kallaghe. Waliosimama nyuma, Bw. Sam Ochieng (SACOMA), Bw. Hugh Morris na Bw David Smith
Perez Ochieng wa SACOMA (aliyeshika matunda ya Cherry) akiwa na Mh Waziri Mkuu.
Meneja Mwendeshaji Masoko wa New Spitalfields Market, Nigel Shepherd akitoa maelezo kwa Mh. Waziri Mkuu. Kando ni Juma Bozdogan
Mh. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na msafara wake wakiondoka eneo la ghala la soko kuelekea mkutanoni. Kulia kwake ni Balozi Peter Kallaghe na Mkurugenzi wa SACOMA, Sam Ochieng. 
--
CHANGAMOTO : UWEZEKANO WA WAKULIMA, VIJANA NA WAFANYABIASHARA KUUZA BIDHAA UINGEREZA
Imeandikwa  kwa ushirikiano wa Urban Pulse na Freddy Macha
--

Ijumaa iliyopita itajulikana kama siku mlango mdogo ila muhimu sana ulipofungua kitasa chake kwa baadhi ya wananchi wanaojituma kikazi na kibiashara Tanzania.  Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda alitembelea soko la mboga na matunda lililoko Leytonstone,  mashariki ya London. Matembezi  yalidhihirisha mahusiano ya ujirani mwema kati yetu  Watanzania na  Kenya yenye  kampuni iliyoshajijenga ndani ya soko hili maarufu na kubwa sana.
 Soko hilo linaloitwa Spitalfields si sehemu inayofahamika na wengi  wanaoishi Uingereza licha ya kwamba jina hilo  si  rahisi kutamka au kuandikwa.  Lakini Spitalfields (tamka “Spitol-fildz”), itakua eneo muhimu sana kwa  vijana, wakulima na wafanyabiashara Tanzania, miaka  ijayo.
Hapa ndipo mboga na matunda toka sehemu mbalimbali duniani huletwa  halafu zikasambazwa  maduka makubwa ya vyakula Uingereza. Hivyo basi mlango kufunguliwa ni “uwanja muafaka”  kwa wote wanaojituma na kutaka maendeleo  kiuchumi.
Spitalfields ina zaidi ya miaka mia tatu. Ingawa ilipoanzishwa makao yake  yalikuwa mtaa wa Brick Lane karibu na Liverpool Street, leo  tawi jipya, New Spitalfields Market limehamishwa karibu uwanja  yalipofanyika mashindano ya Olimpiki mwaka jana. Tawi hili  lilifunguliwa rasmi  1991 na linaongoza Ulaya nzima kwa usambazaji wa matunda na mboga toka nchi zenye joto duniani.
Kati ya nchi hizo  ni ndugu zetu wa Kenya kupitia kampuni yaSACOMA(“Sahara Communities Abroad”)  iliyoanzishwa mwaka 2000 kuendeleza wananchi wasiojiweza kiuchumi na kielimu walioko jimbo la kusini ya jangwa la Sahara wanaozungumza Kiswahili. Licha ya kusafirisha bidhaa na kuziuza  New Spitalfields, SACOMA , anasema msemaji wake Bi Perez Ochieng hutoa ajira kwa takriban watu 30,000 Ulaya na Kenya.
Perez Ochieng, mumewe Sam Ochieng (mkurugenzi SACOMA) na meneja mwendeshaji New Spitalfields, Bw. Nigel Shepherd  walimtembeza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  akiongozana na Balozi wetu Ungereza , Mhe Peter Kallaghe, mkurugenzi wa Kituo cha Biashara Tanzania, London, Yusufu Kashangwa  na maofisa wengine. Ubalozi wa Tanzania Uingereza ndiyo ulioratibu na kuandaa tukio zima.
 Waziri Mkuu  na  wenzake walikuja London kuhudhuria mkutano wa kimataifa unaoangalia namna ya kuondoa njaa na umuhimu wa lishe bora kwa kina mama na watoto ulimwenguni. Mkutano  umeandaliwa na asasi za serikali na zisizo za kiserikali kukutanisha mataifa makubwa (yaani G8),  wachangiaji, wadhamini na watoaji misaada kwa lengo la kutokomeza njaa na kusaidia kuwapatia kina mama na watoto lishe bora.
Baada ya matembezi ndani ya ghala, SACOMA iliandaa kikao  kifupi kuonyesha namna na pia mazao gani huuzwa. Baadhi ya mazao  yaliyowekwa mezani kilipofanyika kikao ni pamoja na  mahindi ya kuchemsha, ndizi kisukari, juisi za matunda, viazi vitamu, maembe sindano na mboga maarufu ya Sukumawiki ambayo hutumiwa zaidi Kenya. Sukuma Wiki (iliyo ndani ya familia ya mboga za kabeji) huuzwa tayari imefungwa kwenye mifuko na SACOMA.
Wakati wa kikao hicho wazungumzaji wahusika walieleza namna ambavyo soko litawafaidi wakulima , vijana na wafanyabiashara wa Tanzania hasa wale wanaojituma. 
Meneja  Mwangalizi wa soko, Nigel Shepherd na Wana SACOMA walifafanua baadhi ya masharti yanayotakiwa kufikiwa kuleta bidhaa hizi sokoni. Mojawapo ni kuzingatia taratibu za uuzaji wa mazao uliowekwa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU). Taratibu hizo ni mathalan upandaji mazao unavyofanywa kusudi umudu safari ya muda mrefu, hifadhi yake katika makasha ya baridi, usafi wa jumla, ufungaji na utangazaji (branding).
Perez Ochieng alitoa mfano  namna SACOMA ilivyojitahidi kuwahusisha vijana wa Kenya katika kilimo ambacho kimewaletea ajira  na kuboresha maisha yao. Akifafanua Perez alisema kawaida vijana  waishio mijini huwa hawavutiwi na kazi za kilimo lakini kuna “mengi ya kuzingatiwa ikiwemo kazi za kupakia bidhaa, kuzifunga katika mifuko, uendeshaji magari, uandishi wa makasha, nk.”
Akiendeleza hoja zaidi Waziri Mkuu ambaye kazaliwa mazingira ya kilimo alisema shughuli hii imedunishwa na mtazamo kuwa ni kazi ngumu na chafu ya jembe tu.  “Inabidi tuweke mazingira yatakayowafanya vijana waone kazi zao zinaweza kupata soko. Kazi kubwa inahitajika kufanywa kuwafanya vijana wapende kilimo.”
Akitoa mfano wa kampuni ndogo ya vijana wa Gongo Seke walioamua kufanya biashara ya kilimo cha bustani  aliyotembelea karibuni mkoa wa Mwanza,  Waziri Mkuu alisema hiyo inathibitisha wapo wanaoweza kufuata fani hii.
Mheshimiwa Pinda aliwahakikishia wenyeji kwamba si tatizo hata kidogo kwa Tanzania kuuza bidhaa zake.  Akithibitisha uzoefu wake kama mkulima, Waziri Mkuu aliwachekesha wasikilizaji  aliposhika moja ya ndizi kisukari zilizokua mezani akasema Watanzania wanaweza kuleta ndizi zilizovimba zaidi na maembe dodo makubwa kuliko yale sindano yaliyoonyeshwa.   
Kufuatana na takwimu zilizotolewa na idara ya habari ya CNN mwaka jana, ingawa uchumi wa Afrika unatazamiwa kukua kwa asilimia 4.5  idadi  ya vijana inatazamiwa kuongezeka mara mbili barani mwaka 2045. Leo asilimia 30 ya vijana walio na umri kati ya miaka 18 hadi 29 hawana ajira katika jamii nyingi za Afrika.
Reviewed by crispaseve on 03:19 Rating: 5

No comments

Post AD