SERIKALI YAJIPANGA KUWA NA SERA YA FILAMU
Mtendaji
Mkuu Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fisoo akiwasilisha Rasimu ya awali ya Sera ya
Filamu wakati wa moja ya kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya awali ya Sera
ya Filamu kilichofanyika hivi karibuni, kulia ni Mkurugenzi msaidizi kutoka
Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi.
Verediana Mushi, na Kushoto ni mdau wa filamu Bw. John Kitime.
Wadau
mbalimbali wa tasnia ya filamu wakijadiliana wakati wa kikao cha wadau cha
kujadili rasimu ya awali ya Sera ya Filamu kilichofanyika hivi karibuni.(Picha
na Genofeva Matemu).
======== ======= =======
SERIKALI YAJIPANGA KUWA NA SERA YA FILAMU
Na: Genofeva
Matemu – Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WHVUM
Serikali
ya Tanzania imejipanga kuendeleza kwa dhati TASNIA ya Filamu ili kuwa chanzo
kikubwa cha ajira kwa wasanii na pia kuongeza uchumi wa nchi.
Ni
dhahiri kuwa sekta ya filamu ni njia madhubuti ya kutambulisha jamii kiutamaduni,
kisiasa na kijamii na pia katika kukuza
na kuongeza fursa za nchi katika uwekezaji na utalii.
Filamu
na Makala za Filamu zikitumika vizuri zitaweza kuhamisha na kuondoa
tofauti mbalimbali zilizopo ndani ya
jamii na hivyo kuongeza umoja na mshikamano baina ya watu wa makabila na watu
wenye asili mbalimbali, hivyo kuutambulisha utamaduni wa Mtanzania.
Kazi na shughuli za Filamu nchini zimekuwa zikisimamiwa
na Sera ya Utamaduni ambayo ilitayarishwa na kupitishwa mwaka 1997 pamoja na Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza na 4 ya
mwaka 1976.
Katika kipindi cha kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2013
kumekuwepo na maendeleo makubwa katika
Tasnia ya Filamu nchini hivyo kuisababishia Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 kutokidhi
baadhi ya mahitaji ya tasnia ya filamu na
kupelekea mahitaji ya kurekebisha Sera ya Utamaduni kama Sera mama na kutungwa
kwa Sera ya Filamu.
Mnamo
Desemba 12 mwaka 2013, wadau mbalimbali kutoka Wizara ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo, Bodi ya
Filamu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi walishiriki
katika kikao cha wadau cha kujadili rasimu ya awali ya Sera ya Filamu.
Wadau wengine ni
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Kazi na Ajira, BASATA, Idara ya
Sanaa na Sanaa za Maonyesho, Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, Mamlaka ya Mapato
Tanzania, Mtandao wa Muziki, Swahili Films,
ROSAF, TAPAF, Umoja wa Mashirikiano wa Filamu, Filamu Cental, Chama cha Hakimiliki Tanzania, Shirikisho la Sanaa za
Maonyesho pamoja na G&S Associates
and Advocates.
Hata hivyo
wadau ambao hawakushiriki walipewa nafasi na Serikali kuwasilisha maoni yao
ambapo mwitiko umekuwa mzuri na maoni yanaendelea kupokelewa ili hatimaye kuwa
na Sera bora na shirikishi.
Katika kikao
hicho Rasimu ya awali ya Sera ya Filamu iliwasilishwa kwa kuelezea historia
fupi ya filamu nchini, vikao vya wadau vilivyofanyika vya mapendekezo ya kuwa
na Sera ya Filamu kati ya mwaka 2004 na 2013, nyaraka kama Mpango Mkakati wa
Bodi ya Filamu unaoonyesha haja ya kuwa na Sera ya filamu pamoja na kuelezea
malengo mahususi na matamko ya Sera mpya inayopendekezwa kutungwa.
Aidha, wadau
walijadili uzoefu wa nchi nyingine kama Kenya, Nigeria, China, Afrika Kusini,
Marekani, Canada, India na Uingereza na matokeo ya tafiti mbalimbali
zilizofanyika pamoja na Changamoto zinazoikabili Tasnia ya Filamu nchini.
Miongoni
mwa mapendekezo yaliyotolewa na wadau ni pamoja na kuwa Sera itamke
uanzishwaji wa Chuo cha Taifa cha Filamu,
Sera itamke kuwepo kwa Mfuko ambao utasaidia katika kuimarisha Sekta ya
Filamu
na Sanaa za maonyesho kwa ujumla, Sera itoe tamko kuhusu kusimamia
maadili katika tasnia ya Filamu na kudhibiti ukatili wa kijinsia
katika tasnia ya Filamu.
Pia walipendekeza kuwa hoja na matamko yawe na takwimu zaidi, Sera
itamke namna ya kumlinda msanii wa Tanzania, mzalishaji wa ndani na wawekezaji,
pamoja na kupiga vita udhalilishaji wa watoto wa kike.
Kwa upande mwingine, wadau hao walitoa pongezi kwa Wizara kwa kuandaa Rasimu
ya awali ya Sera ya Filamu iliyotokana na maoni mbalimbali ya wadau, Sera ambayo
itaiwezesha Tasnia ya Filamu kupata mwelekeo bayana na kukidhi matakwa ya kila
mdau katika tasnia ya filamu.
Wizara inapenda
kuujulisha umma kuwa imekua na inaendelea kushirikiana na wadau wa Filamu kwa
kila hatua ili hatimaye ifanikishe azma ya kuwa na nyaraka zote muhimu katika
kuendeleza, kusimamia, kuratibu na kukuza tasnia ya filamu nchini.
SERIKALI YAJIPANGA KUWA NA SERA YA FILAMU
Reviewed by crispaseve
on
16:30
Rating:
Post a Comment