MSAMA AKABIDHI MILIONI MBILI KWA AJILI YA KUSAIDIA MAPAMBANO DHIDI YA MAUAJI YA ALBINO
Msama akikabidhi hundi ya sh. milioni moja kwa Mjumbe
wa Kamati Kuu Taifa ya Chama cha Albino Tanzania, Mohamed Chanzi.
Katikati anayeshuhudia ni Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha la
Pasaka, Hudson Kamoga.
Mwenyekiti wa Tamasha la Pasaka, Alex Msamaakifafanua jambo.Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa ya Chama cha Albino Tanzania, Mohamed Chanzi akitoa neno la shukrani.
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Msama Promotions, waandaaji wa Tamasha la
Pasaka, kupitia kitengo chake cha maafa, imetoa msaada wa sh. milioni 2 kuunga
mkono kampeni ya kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini (albino).
Akitoa hundi ya fedha hizo jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti wa Tamasha la Pasaka, Alex Msama, alisema anaungana na Rais Jakaya
Kikwete katika hatua ya kupinga ukatili na mauaji ya albino.
Alisema fedha hizo zitatumika kuongeza nguvu ya kuhamasisha
juhudi za kupinga vitendo vya kikatili dhidi ya albino, kwani na wao ni
binadamu kama walivyo watu wengine.
“Nawaomba wadau na Watanzania kwa ujumla, wazidi kuunga
mkono harakati hizi ili kukomesha mauaji yanayoendelea nchini pamoja na kutoa
elimu kwa watu wenye dhana potofu ya kuamini kwamba viungo vya albino
vinatajirisha,” alisema.
Pia Msama aliiomba serikali itenge eneo maalumu lenye
ulinzi mkali ili kuwaweka watoto albino, ambao hawana uwezo wa kujilinda dhidi
ya vitendo wanavyofanyiwa.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Albino Tanzania
(TAS), Mohammed Chanzi, aliishukuru kampuni hiyo kwa kugundua umuhimu wa
kulinda watu wenye ualbino nchini. “Hatuna pa kukimbilia zaidi ya kumuomba Mungu na wadau
mbalimbali kutusaidia, kwani hata sisi tunatamani kuishi kama binaadamu
wengine, pia tunaomba taasisi na Watanzania wasikie kilio chetu na kutuunga
mkono katika hili,” alisema.
MSAMA AKABIDHI MILIONI MBILI KWA AJILI YA KUSAIDIA MAPAMBANO DHIDI YA MAUAJI YA ALBINO
Reviewed by crispaseve
on
04:46
Rating:
Post a Comment