Header AD

Yanga bingwa 80%


Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli.
John Joseph, Dar es Salaam
BAADA ya kipigo cha mabao 8-0 ambacho timu yake ilikipata katika mechi ya Ligi Kuu Bara, juzi, Kocha wa Coastal Union ambaye anasifika kwa kuwa na maneno ya ‘shombo’ alikuwa mpole na kutamka: “Nilijua tutafungwa lakini si kwa idadi hii ya mabao, Yanga wapo vizuri ndiyo maana hata wameifunga timu ya nje bao tano…”

Kauli ya Julio ambaye inajulikana wazi kuwa hajawahi kuipenda Yanga hata kwa utani, inathibitisha jinsi timu hiyo ilivyo kwenye kiwango kizuri na kama itatumia vema mechi zilizosalia, basi itatwaa ubingwa wa msimu huu wa 2014/2015.
Yanga inaongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi sita ikiwa imesaliwa na mechi sita tu, uchambuzi ufuatao unaonyesha jinsi Wanajangwani hao walivyo na nafasi kubwa ya kuwa mabingwa na kama itashindikana basi wao wenyewe ndiyo watatakiwa kujilaumu.
IPO KWENYE KIWANGO
Katika mechi sita zilizopita, Yanga imeshinda tano, mbali na kushinda imeonyesha uwezo wa juu hata inapocheza dhidi ya timu za nje.Iliichapa BDF ya Botswana mabao 2-0 kisha ikaikandamiza FC Platinum ya Zimbabwe 5-1, hiyo ni dalili tosha kuonyesha kuwa Kocha Hans van Der Pluijm ametengeneza kikosi chenye maelewano mazuri.

Yanga imeshinda mechi tano kati ya sita za ligi na hiyo ni dalili nzuri kuwa wapinzani wao wana kazi ngumu ya kuwazuia: Mbeya 1-3 Yanga, Simba 1-0 Yanga, Yanga 2-1 Kagera, Mgambo 0-2 Yanga, JKT 1-3 Yanga, Yanga 8-0 Coastal.Jumla ya mabao ya Msuva, Tambwe na Mrwanda ni 28 ambayo ni idadi kubwa kuliko yale yaliyofungwa na timu nyingine zote kwenye ligi hiyo isipokuwa Yanga.
SAFU KALI YA USHAMBULIAJI
Simon Msuva licha ya kuwa ni winga lakini amekuwa hodari wa kufunga na ndiye anayeongoza kwa mabao akiwa amefunga mabao 13. Amiss Tambwe (9), Danny Mrwanda (6) na Mrisho Ngassa (3).
Ushirikiano wa washambuliaji hao unaonekana kuwa hatari kwenye mabao, pia Kpah Sherman ambaye alikuwa na ukame, naye juzi alianza kuonyesha makali, licha ya kufunga moja lakini alitengeneza mengine mawili.

Kasi hiyo ya kufunga inaonekana kuziacha mbali timu nyingine nyingi za ligi kuu ambazo safu zao za ushambuliaji bado zinayumba, wakiwemo wapinzani wao wa karibu Azam FC na Simba.
TAKWIMU ZINAIBEBA YANGA
Yanga ndiyo timu ambayo imeshinda mechi nyingi (13), imefungwa mabao machache kuliko timu zote (11) na imefunga mabao mengi kuliko timu zote (36).Azam ambao ndiyo wanaonekana kuwa washindani wakuu wa Yanga wameshinda mechi 10, wamefunga mabao 26, wamefungwa mabao 13, hiyo ni dalili kuwa watakuwa na kazi ngumu kuifikia Yanga na kama wakiifikia basi tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa inaweza kuwabeba Yanga.

AZAM WAMEANZA KUVURUGANA
Siku chache zilizopita Azam ilimfukuza kazi kocha wake, Joseph Omog kutokana na kutolewa katika mashindano ya kimataifa, nafasi yake inashikwa na msaidizi wake Mganda, George Best Msimbe, ambaye naye bado hajaifanya timu hiyo kucheza soka la kuvutia.

Mbali na hapo, baada ya mechi ya juzi dhidi ya Mbeya City, inaripotiwa kuwa baadhi ya viongozi wa Azam walikwaruzana kiasi cha kutaka kutwangana makonde, hiyo ni dalili kuwa mambo yanaweza kuendelea kuwa magumu zaidi kwao.Mechi sita zilizopita zinaonyesha Azam imeshinda tatu na sare tatu: Ruvu 0-0 Azam, Azam 0-0 Prisons, JKT 0-1 Azam, Azam 1-0 Ndanda, Coastal 0-1 Azam, Azam 1-1 Mbeya.
SIMBA WAPO MBALI
Timu pekee ambayo inaweza kuzuia au kuchelewesha ubingwa kwa Yanga ni Azam, vigogo wengine Simba wapo mbali na ubingwa huo kwa kuwa wamezidiwa pointi nane na bado wapo mbele kwa mchezo mmoja zaidi ya Yanga. Ikumbukwe kuwa vigogo hao wawili hawakutani tena msimu huu kwa kuwa wameshamalizana.
Yanga bingwa 80% Yanga bingwa 80% Reviewed by crispaseve on 08:32 Rating: 5

No comments

Post AD