BASATA YAPIGA MARUFUKU DISKO TOTO NA UKIUKAJI WA SHERIA ZA UENDESHAJI KUMBI ZA SANAA NA BURUDANI KIPINDI HIKI CHA SIKUKUU YA EID-EL-FITR
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini linawakumbusha
wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata sheria, kanuni na
taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa
na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa
matumizi ya kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa
makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu.
Aidha, BASATA linawakumbusha
wamiliki wote wa kumbi za burudani kwamba ni marufuku kukusanya watoto
katika kumbi zao kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’ ili kuepuka maafa
yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati
za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kutamani
kutengeneza faida katika biashara zao kiasi cha kuandaa disko kwa watoto
hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa makubwa ambayo yangedhibitika kwa
kufuata sheria, kanuni na taratibu.
BASATA kama mtoaji wa vibali vya
kumbi za sherehe na burudani linasisitiza kwamba halitafumbia macho
ukumbi wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba na kuruhusu maonesho
machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu hasa yale yanayoonesha maungo
ya ndani. Hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote
atakayekiuka maagizo haya.
BASATA linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa sherehe njema ya Eid El Fitr na yenye furaha tele.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
BASATA YAPIGA MARUFUKU DISKO TOTO NA UKIUKAJI WA SHERIA ZA UENDESHAJI KUMBI ZA SANAA NA BURUDANI KIPINDI HIKI CHA SIKUKUU YA EID-EL-FITR
Reviewed by crispaseve
on
07:29
Rating:
Post a Comment