SIMBACHAWENE AIASA KAMATI YA PAMOJA YA UENDESHAJI WA MGODI WA TANZANITEONE
WAZIRI
wa Nishati na Madini, George Simbachawene ameiasa Kamati ya Pamoja ya
Uendeshaji wa Mgodi wa TanzaniteOne, “Joint Operating
Committee”-JOC kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ili
kuwanufaisha wadau wa Tanzanite katika uvunaji wa madini hayo, huku
wakilinda maslahi ya mgodi huo kwa Taifa.
Simbachawene
ametoa rai hiyo hivi karibuni wakati akizindua Kamati ya hiyo ya JOC,
katika hafla iliyofanyika kwenye eneo la mgodi wa TanzaniteOne uliopo
Mirerani, katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
“Suala
la kulinda maslahi mapana ya mgodi huu kwa Wabia na Taifa linawezekana,
iwapo Wanakamati ya JOC mtafanya kazi kama timu kwa kila mmoja kutimiza
wajibu wake ipasavyo. Hivyo basi ipokeeni kazi hii na kuitekeleza kwa
ari, kasi na nguvu kubwa” Alisisitiza Mh. Simbachawene.
Ameigiza
Kamati hiyo ya JOC kukamilisha majadiliano ya kuboresha Mkataba wa ubia
uliokuwepo baina ya STAMICO na TML kwani mabadiliko ya Mkataba huo
yataleta matokeo chanya katika udhibiti na uendelezaji wa mgodi na
biashara nzima ya Tanzanite kwa manufaa ya wabia wote na Taifa pia.
“Baadhi
ya vipengele vinavyohitaji kuboreshwa ni pamoja na suala la kutangaza
chimbuko la Tanzanite duniani kuwa ni Tanzania; kuimarisha mazingira ya
mgodi kuwa kivutio cha utalii na mafunzo; kuchangia huduma za jamii
zinazozunguka mgodi na kupanda miti katika maeneo ya mgodi ili kutunza
mazingira” alifafanua Mh. Simbachawene.
Kamati
hiyo ya JOC ina wajumbe 6 ambao ni Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO; Bi.
Asha Jumanne Ngoma, Prof. Peter Antony Kopoka kwa upande wa STAMICO na
Bwana Faisal Juma Shahbhai, Bwana Hussein Omary Gong’a na Bwana Halfan
Mpenziye Hayeshi kwa upande wa Sky Associates Ltd. Kamati hii inaongozwa
na Bwana Faisal Juma Shahbhai.
Katika
uzinduzi wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Simbachawene pia aliwakumbusha
wajumbe wa Kamati ya JOC kumsimamia kikamilifu mwendeshaji wa mgodi huo
yaani TML ili aweze kutekeleza masharti ya mkataba wa ubia katika
uzalishaji wa Tanzanite, kwa manufaa ya pande zote.
Aidha
amewasisitiza wajumbe wa JOC kufanya maamuzi yenye tija katika
uidhinishaji wa bajeti, kubuni mipango ya maendeleo ya mgodi; kuandaa
sera za uendeshaji; kuunda kamati za ushauri kulingana na mahitaji na
kuingia makubaliano ya pamoja na Kitengo cha Uangalizi na Usimamizi
(Monitoring and Evaluation Unit), kuhusu mfumo wa uendeshaji mgodi, ili
kuongeza uzalishaji wa tanzanite na kukuza soko la ndani.
Ameitaka
Sky Associates kutoa nafasi za ajira kwa Watanzania bila ubaguzi na
kuzingatia misingi ya utawala bora katika uendeshaji wa mgodi huo huku
wakitoa maslahi bora kwa wafanyakazi wake.
Simbachawene
amesema STAMICO kwa upande wake, haina budi kuwapatia Wafanyakazi wake
waliopo Mirerani vitendea kazi stahili ili wasiwe na kisingizio cha
kushindwa kutekeleza majukumu yao, na ameitaka Menejimenti ya Shirika
hilo ipime utendaji kazi wa wafanyakazi wake mara kwa mara ili kukuza
ufanisi.
Kuhusu
suala la kuboresha mahusiano mazuri na Wachimbaji wadogo, Simbachawene
amesema mahusiano kati ya TanzaniteOne na Wachimbaji Wadogo yaendelee
kuimarishwa, na amekiri kuitambua Kamati Maalum iliyoundwa na Kamishna
wa Madini, ili kuisaidia Serikali kuweka mfumo mzuri wa uchimbaji katika
mgodi huo, jambo ambalo litaepusha ajali na kupunguza migogoro baina ya
wadau.
“Nazitambua
changamoto za wizi na utoroshaji wa madini ya Tanzanite ambazo ni
matokeo ya wadau wasio waaminifu; nichukue fursa hii kuwataarifu kuwa
Serikali imefanya marekebisho ya Kifungu cha 6(4) cha Sheria ya Madini
ya Mwaka 2010. Kifungu hicho sasa kinampa Kamishna wa Madini mamlaka
kamili ya kutaifisha na kupiga mnada madini yanayokamatwa yakimilikiwa
kinyume cha Sheria. Hivyo, wote wenye tabia ya kufanya biashara ya
madini kinyume cha Sheria wajiandae kupoteza madini yao” Aliongeza kwa
msisitizo Mh. Simbachawene.
Awali,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bwana Deusdedith Magala
amemshukuru Mh. Simbachawene kwa kuunda Kamati hiyo ya JOC na kuizindua
rasmi, kwani itasaidia kulinda hisa za STAMICO, za Serikali na mali za
mgodi, na pia kuuwezesha mgodi kufanya maamuzi makubwa na yenye tija.
Bwana Magala amesema tangu Juni 2013 STAMICO
ilipoingia ubia wa umiliki wa mgodi wa TanzaniteOne na kampuni
ya TML kwa uwiano wa 50:50 wa leseni ya uchimbaji wa Tanzanite, Bodi za
Wakurugenzi za wabia hao wawili ndio zimekuwa zikifanya kazi kama Kamati
ya JOC, jambo ambalo lilileta mzigo mkubwa wa kazi kwa bodi hizo.
Katika
hafla hiyo ya uzinduzi wa Kamati ya Ushirikiano ya Mgodi wa
TanzaniteOne, Mh. Simbachawene na ujumbe wake pia walikagua shughuli za
uchimbaji wa Tanzanite katika mgodi wa CT, zikiwemo uchorongaji,
uchotaji na utoaji wa udongo na kujionea athari za kimazingira
zilizosababishwa na wachimbaji wadogo kwenye kitalu C.
Hafla
hiyo ya uzinduzi wa JOC ilihudhuriwa na mwakilishi wa Kamishna wa Madini
Tanzania, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Wakurugenzi wa
Kampuni ya Sky Associates Ltd na TML, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi
wa Madini Tanzania (TMAA), Kamishna Msaidizi wa Madini - Kanda ya
Kaskazini, Wajumbe wa Kamati ya Pamoja ya Uendeshaji (JOC) na Waandishi
wa Habari.
Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene (aliyevaa miwani) akipata
maelezo kuhusu uchimbaji, ndani ya shimo la mgodi wa chini (underground mine) wa TanzaniteOne wakati alipotembelea mgodi, kabla ya kuzindua Kamati ya Pamoja ya Uendeshaji mgodi huo (JOC).
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (aliyekaa katikati) katika picha na Wajumbe wa Kamati ya Pamoja ya Uendeshaji “Joint Operating Committee – (JOC) ” ya mgodi wa TanzaniteOne, baada ya kuizundua Kamati hiyo mgodini hapo mwishoni mwa wiki. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa JOC Bwana
Faisal Juma Shahbhai na kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
STAMICO, Duesdedith Magala. Wajumbe wengine waliokaa kutoka kushoto ni
Asha Jumanne Ngoma, Prof. Peter Antony Kopoka (wa tano), Bwana Hussein
Omary Gong’a (aliyesimama kushoto) na Bwana Halfan Mpenziye Hayeshi
(aliyesimama kulia).
Waziri
wa Nishati na Madini, George Simbachawene (mwenye overall ya Kibluu)
akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya JOC, Faisal Juma
Shahbhai (aliyevaa kofia ngumu ya Kibluu) kuhusu uzalishaji wa Tanzanite
katika mgodi wa TanzaniteOne. Anayemsikiliza (mwenye overall ya
Kijani) ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Duesdedith Magala.
SIMBACHAWENE AIASA KAMATI YA PAMOJA YA UENDESHAJI WA MGODI WA TANZANITEONE
Reviewed by crispaseve
on
04:50
Rating:
Post a Comment