Header AD

Makamu wa mwenyekiti wa CCM Tanzania bara ,Philip Mangula aongoza mazishi ya Tasili Mgoda Iringa asisitiza watanzania kudumisha Upendo

 
post-feature-image
 Makamu  wa mwenyekiti wa CCM Tanzania bara ,Philip Mangula akiweka  shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa marehemu Tasili Mgoda wakati wa mazishi yaliyofanyika juzi mjini Mafinga
 Waziri  wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi, Wiliam Lukuvi ambae ni mbunge wa jimbo la Isimani  mkoani Iringa  akiweka  shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa marehemu Tasili Mgoda wakati wa mazishi yaliyofanyika juzi mjini Mafinga
 Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Mufindi Marcelina Mkini akiweka  shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa marehemu Tasili Mgoda wakati wa mazishi yaliyofanyika juzi mjini Mafinga
Mbunge wa  jimbo la Mufindi Kaskazini  mahamudu Mgimwa  (kushoto ) na mbunge wa  Kilolo Venance Mwamoto wakiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa marehemu Tasili Mgoda wakati wa mazishi yaliyofanyika juzi mjini Mafinga
Mwakilishi  wa vyama  vya upinzani  kutoka  chama cha demokrasia na maendeleo (chadema)  wilaya ya  Mufindi akiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Iringa marehemu Tasili Mgoda wakati wa mazishi yaliyofanyika juzi mjini Mafinga (picha zote na matukiodaimaBlog 
---
 Na  MatukiodaimaBlog 

MAKAMU mwenyekiti  wa chama  cha mapinduzi (CCM)  Tanzania  Bara  Philip Mangula ameongoza  mamia  ya wakazi wa  mkoa  wa Iringa na  mikoa ya jirani katika mazishi  ya aliyekuwa mwasisi wa TANU na mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa  wa Iringa Tasili Mgoda aliyefariki Oktoba 14  wakati wa kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha baba wa Taifa mwalimu Julius Nyerere na kuzikwa  jana  katika makaburi ya Mafinga  wilaya ya Mufindi  kudai kuwa ameondoka  kwa  kuacha upendo kwa Taifa .

Mangula katika  salamu  zake alisema  kuwa  siku mbili kabla ya  kifo  chake Mgoda alimpigia simu japo kwa bahati mbaya hakuweza  kuwasiliana kutokana na kuwa katika mkutano na kuwa kati ya  watu na  viongozi ambao  walikuwa na upendo kwa wengine marehemu Mgoda ni mmoja na  hivyo kuwataka wanafamilia ,wananchi wa Mufindi  na  wana CCM   kudumisha upendo na  kuendelea  kufanya kazi  kwa  uadilifu   zaidi kama  njia ya kumuenzi   marehemu  huyo Mgoda na baba  wa Taifa  ambao  katika  uongozi  wao  waliweza  kuongoza kwa kuzingatia misingi ya uadilifu .

Alisema  kuwa Mgoda  kuna mambo  mengi ambayo hayaelezeki aliyoacha kama  kielelezo  cha uzalendo  wake  ndani ya  wilaya ya  Mufindi ambako  alianzisha shule  za shirika la  elimu Mufindi ( MET) lakini katika Taifa ni  moja kati ya watu  waliofanya kazi kwa karibu na mwalimu Nyerere ila katika ukombozi wa Taifa la  Namibia  kwa  kumhifadhi  mpigania  uhuru wa Namibia Rais wa Kwanza wa  nchi hiyo  Sam Nujoma  akiwa anafukuzwa na serikali ya  wakoloni nchini  mwake .

Alisema  kuwa  marehemu Mgoda  alikuwa ni mtu mwenye upendo  kwa  wote na hakupenda makuu katika  utawala  wake  hivyo ni  vizuri kuendelea  kumuenzi kwa  kutenda mema na  kupendana  zaidi .

Mwenyekiti wa UWT Mufindi   Marcelina Mkini  alisema  kuwa  wao kama  wanawake  wanatambua mchango mkubwa ambao  Mgoda  aliutoa kwao ikiwa ni pamoja na kujenga  misingi  bora ya uongozi  ndani ya chama na jumuiya  hiyo na  kuwa katika  wilaya ya  Mufindi ni  mengi ambayo ameyafanya na kubwa  zaidi ni kupigania   uanzishwaji wa mji mdogo wa Mafinga na barabara ya lami kutoka Mafinga kwenda Madibila  wilaya ya Mbarali .

Alisema kuwa  yote  hayo ameyafanya  wakati akiwa mwenyekiti wa Halmashauri ya  wilaya ya  Mufindi na  kubwa  zaidi   ni  uongozi  wake uliotukuka kwa  kuongoza  chama kama mwenyekiti kwa  miaka zaidi ya 40 katika maeneo mbali mbali .

Marehemu   akiwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa aliweza  kupigania  ujenzi wa barabara ya Lami kutoka Iringa - Dodoma na baada ya  kukamilika kwa  ujenzi  huo alifurahi  zaidi na kuwa  sasa  yupo  tayari  kufa wakati  wowote kwani furaha  yake imetimia .

" Enzi ya uhai wake  alitupa moyo  sana  wanawake  wa wilaya ya Mufindi na  kujikuta  tunasonga  mbele kwa  upendo zaidi   hivyo  sisi kwa ajili ya kumuenzi tutaanzisha  mradi wa  wanawake  ambao utapewa  jina la Tasili Mgoda kama  sehemu ya  kumuenzi zaidi"

Mkini  ambae ni mjumbe wa NEC Taifa alisema kuwa   kutokana kifo chake  kuwa ni  histori  kubwa ndani ya Taifa kwa  mhasisi   huyo wa TANU ambaye  alifanya kazi na baba wa Taifa  kifo  chake  kutokea  siku  ambayo ilikuwa ni kumbukumbu ya  kifo cha mwalimu ni  vema  wana CCM kuendelea  kuenzi uzalendo na  kuwakumbuka  waasisi  hao kwa  kuepuka chuki ndani ya  chama na badala yake  kudumisha umoja  zaidi.

Alisema  pamoja na  kuondoka kwa baba  wa Taifa   hivi  sasa watanzania wamepata  tumaini  jipya la uongozi  unaofafana na  ule wa mwalimu  Nyerere kwa  kuwa na Rais Dkt  John Magufuli ambae misingi yake ni  sawa kabisa na ya waasisi hao wa TANU hivyo ni vema  kuzidi  kumwombea  na kuendelea  kuwaenzi  waasisi  waliotangulia kwa  kufanya kazi zaidi.

Hivyo alisema kutokana na  Rais wa awamu ya tano Dkt Magufuli  kuahidi  kutoa  kiasi cha Tsh milioni 50 kwa kila kijiji ana amini  wao kama UWT wilaya ya  Mufindi  watakuwa ni mwanga wa  kuhamasisha  uanzishwaji  wa  vikundi vya  kiuchumi ambavyo  vitanufaika na fedha  hizo  ili  kuwakumbuka  waasisi hao na kutekeleza   kauli mbiu ya hapa kazi   Tu kwa  kufanya kazi bila  kuchoka.

 Kwa  upande  wao  wabunge  walioshiriki katika mazishi  hayo Mahamudu  Mgimwa  wa Mufindi Kaskazini , Cosato  Chumi wa Mafinga , Deo Sanga  kutoka mkoa  wa Njombe   Kaskazini na mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto  walisema kuwa  kuendelea  kumuenzi Mdoga  ni kufanya kazi kwa umoja na kuepuka kutengana kwa misingi ya kisiasa ama dini.

Huku  waziri  wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Wilima Lukuvi ambae ni mbunge wa jimbo la Ismani  akisema kuwa misingi ya uongozi  wake marehemu Mgoda  ndio ambao  leo  wananchi wa mikoa ya kusini  wanafurahia matunda  yake ikiwemo lami ya Iringa - Dodoma na mengine  mengi  ambayo ameyafanya kazi nafasi yake kama mwenyekiti wa CCM mkoa  wa Iringa .

Viongozi  wengine  walijumuika  katika mazishi hayo ni pamoja na naibu katibu mkuu wa CCM Bara
Luhwavi , mkuu  wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu   na  wengine  pia Aliyekuwa mwenyeviti wa wenyeviti wa CCM, Pancras Ndejembi.

Mwenyekiti wa CCM  mkoa wa  Iringa alisema kuwa wazee  wetu hao ambao wametangulia mbele za haki uongozi wao  hauonyeshi kama  walikuwa  wakifuata  mikate katika  serikali ya Tanzania  wala ndani ya CCM hivyo  kuwataka  wana CCM kupunguza njaa katika  kutumikia nafasi  hizo na badala  yake  kuungana kuijenga nchi  na Chama bila  kutanguliza njaa mbele

Akisoma wasifu wa marehemu Tasili Mgoda  , Msambatavangu  alisema  kuwa   Mgoda alizaliwa  July 6 1931 katika  kijiji cha Mdandu wilaya ya  Njombe ambapo kwa  sasa  wilaya ya  wanging'ombe kwa  wakati huo kijiji  cha Mdandu  ndicho kilikuwa makao makuu ya  serikali ya Kikoloni wilaya ya Njombe .

 Elimu

Alipata elimu ya Msingi shule ya msingi  Kidugala kwa muda wa miaka  miwili  kati ya mwaka 1942- 1943 baada ya hapo aliendelea na elimu ya msingi Ilembula ambapo alisoma hadi  darasa la sita mwaka 1947 alipohamia sekondari  ya Malangali  iliyopo wilaya ya  Mufindi  mwaka 1952 alihitimu kidato cha nne pamoja na masomo ya ufundi .

 Mwaka 1973 Mgoda  alikwenda nchini Marekani  kupata  mafunzo ya  kilimo na ufugaji  ,aliwahi  kupata mafunzo ya siasa  na uongozi  chuo  cha Kivukoni  Dar es Salaam  kwa sasa kinajulikana kama chuo cha  kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Utumishi

 Mwaka 1953  alianza  kazi kama msimamizi wa kampuni ya Carpentry Furniture  iliyokuwa jijini Dar es salaam  na mwaka 1956 aliamua kuachana na kazi  hiyo kwa kuwa alikuwa amejiunga na siasa  akiwa ni mmoja wa vijana wachache wa TANU  waliokuwa na jukumu la kuhamasisha  wananchi  kukiunga mkono chama cha TANu  katika  kutafuta UHuru wa Taifa  letu ,mwaka 1957-1958 Mgoda  alikuwa mjumbe wa Halmashauri  kuu ya mkoa  na  wilaya  lakini  pia  akiwa ni mjumbe wa kamati  ya siasa  ya  wilaya na mkoa 

Katika  uhai  wake amepata  kushika nafasi mbali mbali  zikiwemo za ukuu wa wilaya  katika  wilaya mbali mbali nchini  katibu  wa chama ,Mwenyekiti  wa chama mkoa  wa Iringa na udiwani pia uenyekiti wa Halmashauri ya Mufindi nafasi ambayo  alidumu nayo hadi alipostaafu siasa 

Alisema kuwa marehemu Mgoda kwa  kipindi kirefu  alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya shinikizo la damu  na  hivyo akawa anapata matibabu yake Hospitali ya mji wa Mafinga  Hospitali ya  mkoa wa Iringa  na Hospitali ya jeshi Lugalo Dar es Salaam  na kuwa Oktoba 14 hali yake ilibadilika ghafla  na kukimbizwa  Hospitali ya mji wa Mafinga  majira ya saa 8 mchana na uchunguzi wa madaktari ulibaini  kuwa anasumbuliwa na kisukari na shinikizo la damu ndipo  alipoanzishiwa matibabu na majira ya saa 3;45 usiku Oktoba 14 aliaga dunia ,Marehemu Mdoga  ameacha  watoto 14 wajukuu 20

MWISHO
Makamu wa mwenyekiti wa CCM Tanzania bara ,Philip Mangula aongoza mazishi ya Tasili Mgoda Iringa asisitiza watanzania kudumisha Upendo Makamu wa mwenyekiti wa CCM Tanzania bara ,Philip Mangula aongoza mazishi ya Tasili Mgoda Iringa asisitiza watanzania kudumisha Upendo Reviewed by crispaseve on 06:26 Rating: 5

No comments

Post AD