DKT TIZEBA AFUNGA MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI
Waziri
wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa maadhimisho ya
siku ya kitaifa ya siku ya chakula Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja
wa CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Waziri
wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba alipotembelea banda la Kampuni ya
POLYTECH MACHINERY inayojishughulisha na uuzaji wa mashine mbalimbali
ikiwemo za kukamua mafuta ya alizeti wakati wa maadhimisho ya siku ya
kitaifa ya siku ya chakula Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM
Kalangalala Mkoani Geita. Mwingine ni Mhe Dkt Mary Mwanjelwa Naibu
waziri wa Kilimo (Kulia).
Waziri
wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza wakati wa maadhimisho ya
siku ya kitaifa ya siku ya chakula Duniani, yaliyofanyika katika Uwanja
wa CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Naibu
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Mary Mwanjelwa akizungumza jambo na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe wakati wa maadhimisho
ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula Duniani, yaliyofanyika katika
Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita.
Na Mathias Canal, Geita
Waziri
wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba leo Octoba 16, 2017 amefunga rasmi
maadhimisho ya siku ya kitaifa ya siku ya chakula Duniani, yaliyofanyika
katika Uwanja wa CCM Kalangalala Mkoani Geita kuanzia Octoba 10 mpaka
Octoba 16, mwaka 2017.
Akizungumza
katika Kilele cha Maadhimisho hayo waziri Tizeba alisema kuwa Kuanzia
msimu huu wa kilimo Wakulima wa korosho watapata bure pembejeo aina ya
salfa zilizokuwa zikiuzwa kwa bei ya ruzuku.
Alisema
Hatua hiyo ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya
kuhakikisha vikwazo vyote vilivyokuwa, vikiwakabili Wakulima wa zao la
korosho vinaondolewa ili kuwawezesha kuongeza uzalisha na tija zaidi
kutokana na zao hilo.
Mhe
Tizeba alisema Madhumuni ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ni
kutoa nafasi ya kutafakari, namna Jamii katika ngazi ya Kaya, Kijiji,
Kata, Tarafa, Wilaya, Mkoa, Taifa na Kimataifa zinavyoweza kuhakikisha
ongezeko la uzalishaji na upatikanaji wa chakula cha kutosha na chenye
lishe bora kwa watu wote na kwa wakati wote.
Alisema
kuwa Kila mwaka Shirika la Chakula Duniani (FAO) baada ya kufanya
tathmini ya hali ya Chakula hutoa Kaulimbiu ambayo huwa ni dira ya
maandalizi na maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani.
Kaulimbiu
ya mwaka huu 2017 inasema “Badili mwelekeo wa uhamaji; Wekeza katika
usalama wa chakula na maendeleo Vijijini”. Kaulimbiu hii inaweka umuhimu
katika kuweka Mipango na Programu zinazolenga kuongeza tija na
uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo Vijijini; kupuza utegemezi na
kuongeza usawa katika Jamii, sambamba na uhifadhi mazingira ambayo ndiyo
muhimu katika maendeleo ya kilimo na hifadhi ya Jamii ili yachochee
jitihada za kuondoa umaskini.
Alisema
kuwa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka huu ni ya
kujivunia kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika uongozi wa
Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli, kwa kipindi chote nchi
yetu imejitosheleza kwa chakula kwa zaidi ya asilimia 100 na hivyo kuwa
na ziada ya chakula.
Uzalishaji
wa mazao ya chakula kwa mwaka 2016/2017 umefikia Tani 15,900,864 za
chakula kwa mlinganisho wa nafaka. Kati ya kiasi hicho, tani 9,388,772
ni za mazao ya nafaka na tani 6,512,092 ni za mazao yasiyo nafaka.
Hata
hivyo Mahitaji ya chakula kwa mwaka 2017/2018 yatakuwa Tani 13,300,034
ambapo Tani 8,457,558 ni kwa mazao ya nafaka na Tani 4,842,476 ni mazao
yasiyo nafaka.
Dkt
Tizeba aliongeza kuwa Kutokana na uzalishaji huu, nchi itakuwa na
kiwango cha utoshelevu wa asilimia 120 ambapo kiwango hiki kinaonyesha
kuwa nchi itakuwa na ziada ya chakula ya Tani 2,600,831 ambapo mazao ya
nafaka kutakuwa na ziada ya Tani 931,214 na mazao yasiyo nafaka ni Tani
1,669,617 kwa viwango vya utoshelevu vya asilimia 111 na 134 mtawalia.
Alisema Ziada hii inatosha kwa matumizi ya chakula hapa nchini na kuwa
na ziada ya kuuza.
Katika
hatua nyingine Mhe waziri wa kilimo ametumia fursa hiyo kuwaasa
wananchi wote kuwa na hifadhi ya chakula katika kaya zao na kutumia
chakula kilichopo kwa uangalifu hadi msimu mwingine wa mavuno.
‘‘Wahenga
walisema usione vyaelea vimeundwa; hivyo mafanikio tuliyoyapata ni
matokeo ya jitihada za Serikali, Wadau, Wabia wa Maendeleo na Wananchi
wote kwa ujumla wao kwa kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo
hususani kilimo, ufugaji, uvuvi na huduma mbalimbali zinazotolewa,
Aidha zipo changamoto mbalimbali zikiwemo, mabadiliko ya tabianchi,
ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kupungua kwa uzalishaji na tija ya
mazao, uhaba wa malisho ya mifugo na rasilimali maji lakini Tumejipanga
kuendelea, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa
ni pamoja na kuzalisha mbegu bora zinazovumilia ukame, magonjwa na kutoa
mavuno mengi” Alisema Mhe Dkt Tizeba
Sambamba
na hilo, alisema kuwa serikali imejipanga kuendelea kuwaelimisha na
kuwasaidia Wafugaji wa Tanzania, kufuga kitaalamu zaidi ili kuepuka ile
hali ya kuhamahama kwa ajili ya kutafuta malisho na maji.
Kilele
cha maadhimisho ya siku ya Chakula Dunia ilihudhuriwa na Makatibu
Wakuu, Makatibu Tawala, Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la
Umoja wa Mataifa (FAO), Mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Chakula
Duniani (WFP), Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri
za Wilaya, Miji na Majiji, Viongozi wa Vyama vya Siasa, na Viongozi wa
Dini.
DKT TIZEBA AFUNGA MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI
Reviewed by crispaseve
on
08:02
Rating:
Post a Comment