Header AD

MWAKYEMBE AWAFUNDA WAJUMBE WA KAMATI YA KUZUIA MUAJI YA KIMBARI KWA NCHI ZA MAZIWA MAKUU


Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Dkt Harrison Mwakyembe amewataka wajumbe wa Kamati ya Kimataifa inayojishughulisha na kuzuia mauaji ya kimbari katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu kuangalia upya mikakati ya kuondoa vitendo vya mauaji ya kimbari na ukiukwaji wa haki za binadamu katika ukanda huo.

Dkt. Mwakyembe amesema Ukanda wa Maziwa Makuu umekuwa ukishuhudia vitendo vya mauaji ya kimbari vikishamiri licha ya kwamba kila nchi imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali na kusaini makubaliano ya kikanda na kimataifa ya kuzuia vitendo hivyo.

Amesema wakati sasa umefika wa kujiangalia ni kwanini vitendo hivyo vimekuwa vikishamiri pamoja na jitihada zote ambazo kila nchi imekuwa ikizichukua ili kukomesha vitendo hivyo.

“ Ni wazi kuwa siku hizi mwelekeo wa matukio ya kihalifu umebadilika, zimeibuka njia nyingi mpya zinazosababisha mauaji ya kimbari na hata ukiukwaji wa haki za binadamu, kutokana na hali hiyo kuna haja ya kuboresha mikakati yenu ili kuzuia kuendelea kutokea kwa mauaji ya kimbari na ukiukwaji wa haki za binadamu,” alisema.

Aidha Mhe. Waziri pia amewaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni jukumu lao kuangalia namna ya kukabiliana changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza na hivyo kufanya vitendo hivyo kuendelea kuwepo miongoni mwa nchi za maziwa makuu.Amewataka wataalamu hao kwenda mbali zaidi na kubainisha hatua zitakazofaa kuchukuliwa za kisera, kisheria na kiutawala ili kukabiliana na changamoto ya kuendelea kuwepo kwa vitendo hivyo ili kuvikomesha ndani ya nchi za ukanda wa maziwa makuu 

Mhe. Dkt Mwakyembe alikuwa akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo na kubadilisha na uzoefu wajumbe wa Kamati hiyo kwa nchi za Maziwa Makuu yanayofanyika jijini Dar es salaam. Mafunzo hayo yanajumuisha wajumbe kutoka nchi za Zambia, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Congo DRC, Sudani Kusini na mwenyeji Tanzania.
MWAKYEMBE AWAFUNDA WAJUMBE WA KAMATI YA KUZUIA MUAJI YA KIMBARI KWA NCHI ZA MAZIWA MAKUU MWAKYEMBE AWAFUNDA WAJUMBE WA KAMATI YA KUZUIA MUAJI YA KIMBARI KWA NCHI ZA MAZIWA MAKUU Reviewed by crispaseve on 06:01 Rating: 5

No comments

Post AD