UFUNGUZI WA MAFUNZO JUU YA MWONGOZO WA USIMAMIZI WA UWEKEZAJI WA UMMA YANAYOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA CHUO CHA MIPANGO, DODOMA TAREHE 27 HADI 31, MACHI 2017
Na Thomas Nyindo.
Maofisa wa Idara za Sera na Mipango kutoka Wizara, Idara
na Wakala za Serikali wametakiwa kuongeza ufanisi na ubunifu katika kuandaa na
kusimamia miradi ya maendeleo ili kuharakisha malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu
Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bw. Maduka Kessy wakati akifungua mafunzo
ya Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma yanayoendelea katika ukumbi wa
Chuo cha Mipango Dodoma.
Kessy alieleza kuwa mafunzo hayo
yanalenga kuwajengea uwezo maofisa wanaosimamia masuala ya Sera na Mipango
katika kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo, hususan, ile inayogharamiwa
kwa fedha za Serikali ili kufanya Tanzania kuingia kwenye nchi za kipato cha
kati kama ilivyoaninishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo.
“Mipango ya maendeleo tunayojiwekea,
kama taifa, inapaswa kutafsiriwa katika miradi na programu za utekelezaji,
hivyo mafunzo haya yatatusaidia kuongeza ufanisi, ubunifu na uwajibikaji katika
kuandaa miradi na kusimamia miradi yenye tija kwa wananchi,” alisema Kessy.
Aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo
kuwa wao ni miongoni mwa wadau muhimu katika kuifanya Tanzania ipige hatua za
maendeleo kwa kuwa ndio wanaohusika katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa
miradi ya maendeleo.
Aidha, Kessy alieleza kuwa mafunzo hayo
yatawasaidia washiriki kuongeza ufanisi na ubunifu katika kuchagua miradi,
kutafuta fedha za ugharamiaji na kuboresha uratibu wa kufungamanisha
uwekezaji wa umma kwa kubainisha hatua za kufuata katika kujumuisha miradi ya
maendeleo katika bajeti za maendeleo.
“Mwongozo huu utawasaidia kufanya
maamuzi katika kuchagua miradi sahihi ya uwekezaji katika sekta ya umma na
kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji wake. Sote tunafahamu kuwa azma yetu ya
maendeleo kitaifa ni kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025,” alisema.
Kaimu Katibu Mtendaji huyo alieleza
kuwa zipo changamoto zinazokabili usimamizi wa miradi ya maendeleo, kuanzia
hatua ya kubuni, kutekeleza hadi kukamilisha miradi hiyo. Kwa hiyo Mwongozo wa
Usimamizi wa Uwekezaji waRasilimali za Umma ni mojawapo ya maandiko muhimu
ambayo yamebuniwa kukabiliana na changamoto hizo.
Dkt.
Lorah Madete, Kaimu Naibu Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi Jumla, Tume ya
Mipango (aliyesimama), akitoa neno kwa washiriki wa mafunzo kabla ya
kumkaribisha mgeni rasmi ili afungue mafunzo hayo ya siku tano. Waliokaa ni Bw. Maduka Paul Kessy, Kaimu
Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango (katikati) na Bw. John Mduma, Mhadhiri
Mwanamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mgeni
Rasmi Bw. Maduka Paul Kessy, Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango
(aliyesimama) akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo kuhusu Mwongozo wa Usimamizi
wa Uwekezaji wa Umma kwa washiriki kutoka Idara za Sera na Mipango za Wizara, Idara zinazojitegemea
na Wakala za Serikali. Wengine ni Bi. Lorah Madete, Kaimu Naibu
Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi Jumla, Tume ya Mipango (kulia) na Bw. John
Mduma, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (kushoto).
Washiriki
wa Mafunzo wakimsikiliza kwa makini Mgeni Rasmi (hayupo pichani) wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo.
Dkt.
John Mduma, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (aliyesimama),
akitoa neno kwa washiriki wa mafunzo mara baada ya mafunzo hayo kufunguliwa
rasmi.
Washiriki
wa mafunzo kuhusu Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma kutoka Idara za Sera na Mipango za Wizara, Idara zinazojitegemea
na Wakala za Serikali pamoja na
wawezeshaji wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni
Rasmi mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
UFUNGUZI WA MAFUNZO JUU YA MWONGOZO WA USIMAMIZI WA UWEKEZAJI WA UMMA YANAYOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA CHUO CHA MIPANGO, DODOMA TAREHE 27 HADI 31, MACHI 2017
Reviewed by crispaseve
on
02:59
Rating:
Post a Comment