MAKOCHA WA SIMBA,ABDALLAH KIBADENI NA JAMHURI KIWEHLO WAFUNGASHIWA VIRAGO,MWENYEKITI RAGE NAYE ASIMAMISHWA
Wakati Kamati ya utendaji ya Simba ikimsimamisha mwenyekiti wake Ismail
Aden Rage, imewafungashia virago makocha wake Abdallah Kibadeni 'King' na msaidizi wake Jamhuri Kiwehlo 'Julio' kuinoa timu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi.
Akizungumza na Makao Makuu ya klabu hiyo mchana wa leo, Kaimu Mwenyekiti wa Simba Joseph Itang'are 'Kinesi' alisema kikao cha kamati ya utendaji kilichokaa jana usiku kimefikia uamuzi wa kumsimamisha
mwenyekiti wao kwa kile walichoeleza kutokuwa na imani nae baada ya
kushindwa kuitisha mkutano mkuu wa mabadiliko ya katiba.
Hii
itakuwa mara ya pili kwa Rage, kusimamishwa ndani ya klabu hiyo,awali
alisimamishwa mapema mwezi Machi, baada ya wanachama kufanya mapinduzi
ya kumuondoa Rage akiwa kwenye matibabu nchini India hata hivyo
aliporudi alisema hatambui mapinduzi hayo na kuitisha mkutano
alioufanya kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi Oyestabay huku akiadi
kuitisha mkutano mkuu wa dharura wa mabadiliko mapema mwezi Agosti hata
hivyo aliharisha kwa kile alichoeleza ni kupisha mwezi mtukufu wa
Ramadhani.
Lakini jana Kinesi alisema "Mkutano mkuu wa mwaka ulikuwa ufanyike mwezi huu wa Novemba na ajenda kubwa ni mabadiko ya katiba, lakini cha kushangaza Rage amewambia wanachama hakuna mkutano mpaka mwakani na ameondoka yupo nje ya nchi.
"Sasa
hii ni ukiukwaji wa katiba, hatuna imani naye na hata kama angekuwepo
tungemueleza wazi kitendo chake hatukiafiki na hatuna imani naye,
tumemsimamisha mpaka Desemba Mosi na hii ni kwa mujibu wa katiba ya
Simba kifungu cha 30.
Kinesi alisema Desemba Mosi ndio utafanyika mkutano mkuu wa wanachama na hatma ya Rage
itajulikana kwenye mkutano huo iwapo wanachama wataridhia kumuondoa au
wataamua adhabu yake ya kumsimamisha iendelee au arejeshwe kundini
kumaliza muda wake ambao unafikia ukingoni Aprili Mwakani.
Mbali
na Rage, pia rungu hilo la Kamati ya utendaji limeangukia benchi ya
ufundi la klabu hiyo baada ya kuwafungashia virago Abdallah Kibadeni
'King' na Jamhuri Kiwehlo 'Julio' kutokana
na mwenendo mbovu wa timu yao iliyomaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi ikiwa inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 24.
Kinesi
alisema nafasi ya Kibadeni itachukuliwa na aliyekuwa kocha wa timu ya
Gor Mahia Zdravko Logarusic raia wa Crotia akisaidiwa na Seleman
Matola.
Alisema kocha huyo atatua nchini Desemba Mosi na timu itaanza rasmi mazoezi Desemba 2 kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi.
Kibadeni
alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alisema "Nashukuru nimeacha timu
kwenye nafasi nzuri, kilichofanyika ni demokrasia naheshimu hilo, bado
nitaendelea kuwa mwanachama wa Simba, na bado nina mkataba na klabu
hiyo, nitafatilia nipate haki yangu.
CHANZO:MICHUZI BLOG
MAKOCHA WA SIMBA,ABDALLAH KIBADENI NA JAMHURI KIWEHLO WAFUNGASHIWA VIRAGO,MWENYEKITI RAGE NAYE ASIMAMISHWA
Reviewed by crispaseve
on
12:42
Rating:
Reviewed by crispaseve
on
12:42
Rating:

Post a Comment