Kutana Na Mshauri Bingwa Wa Biashara Mr CHARLES MSULUZYA NAZI
NAMNA YA KUANZISHA BIASHARA.
Ukitaka kufanya biashara yoyote ile unatakiwa kufanya utafiti.
Kutokufanya utafiti ni chanzo cha biashara nyingi kuharibika. Lazima
ujiulize kwamba unataka kufanya biashara gani? Usiseme unataka kufanya
biashara yoyote ile kwani kusema kwamba unataka kufanya biashara yoyote
ile ni kupoteza mwelekeo kwa kuwa utakuwa hujui unataka kufanya nini.
Kama hujui cha kufanya hakuna kitu utakachokifanya. Hili ni tatizo la
watu wengi. Hata baadhi ya watu niliokutana nao wakitaka ushauri
wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo hili. Njia ya kukusaidia kuamua ufanye
biashara gani ni kwa kujiuliza umewahi kufanya kazi au biashara gani?
Umesomea nini? Vipaji vyako ni vipi? Ni biashara ipi au kazi ipi
unapenda zaidi kuliko nyingine na kwa sababu gani? Ukisha jiuliza
maswali haya chukua kalamu na karatasi uandike maswali yako na kuyajibu.
Ukikagua maswali na majibu yako utagundua shughuli unayoipenda,
unayoiweza na una kipaji nayo na hiyo ndiyo inayokufaa. Ukishachagua
biashara unayoipenda ni rahisi sana kufanikiwa kwani shughuli utazifanya
kwa hiyari bila kujilazimisha. Kama unashindwa kuamua ni biashara gani
ufanye, soma sura ya sita katika kitabu hiki. Nimeelezea kuhusu mawazo
yanayoweza kukusaidia kuanzisha biashara mbalimbali ambazo unaweza
kuzifanya. Kama utakuwa bado hujafikia uamuzi baada ya hapo basi tafuta
na wasiliana na washauri ili mbadilishane mawazo na ufundishwe jinsi ya
kuamua ufanye biashara gani.
Mambo mengine unayotakiwa kuyafanyia utafiti ni:-
(i) Kujua siri ya bishara unayotaka kufanya ili upate mbinu
za kupata mafanikio. Unaweza kupata siri au kujifunza mbinu kutoka kwa
watu wanaofanya biashara kama unayotaka kufanya. Suala hili ni gumu sana
kwani wafanyabiashara wengi huwa wanaficha siri za biashara zao ili
kulinda wasizidiwe maarifa na washindani wao. Unaweza kuipata siri hiyo
kama utakwenda kupata ushauri toka kwa mfanyabiashara ambaye yuko mbali
na mahali unapofanyia biashara, au tafuta ushauri kwa wataalamu wa mambo
ya biashara.
(ii) Fanya utafiti wa soko la bidhaa unazouza au unazotarajia
kuuza. Jiulize, je bidhaa unazotaka kuziuza zina soko? Utawauzia watu
gani na utauzaje? Kama wewe ni mzalishaji, una mazao / bidhaa unapaswa
kuuza kwa jumla, mchanganyiko ama rejareja? Je utatangaza vipi bidhaa
zako? Maelezo ya namna ya kutangaza bidhaa zako utayapata katika Sehemu
ya Tatu ya Kitabu hiki. Utafiti wa soko unaweza kuufanya kwa kuwauliza
wafanya biashara waliotangulia maswali hayo ya utafiti kwani wao
wamekuwapo kwenye soko na wanazijua siri za soko.
(iii) Tengeneza bajeti yako kwa kuorodhesha vitu vinavyohitajika
na gharama zake ili kuweza kuanzisha biashara yako. Vitu hivyo ni:-
(a) Gharama za Kujenga au kupanga ofisi
(b) Gharama za Leseni ya biashara
(c) Makadirio ya kodi toka TRA
(d) Garama ya vifaa vya ofisi yaani, Samani, makaratasi, mitambo, mashine, nk
(e) Manunuzi ya malighafi au bidhaa za kuanzia biashara
(f) Idadi ya wafanyakazi na gharama za mishahara yao.
(g) Gharama nyinginezo kama vile, umeme, maji, nk.
(iv) Unatakiwa kujua ni mtaji kiasi gani unahitajika kuanzisha
biashara yako. Mtaji huo utaujua baada ya kujumlisha gharama
zilizoorodheshwa katika kupengele namba (iii)Gharama hizi ni za mwaka
ule wa kwanza wa kuanzia
(v) Tafuta Mtaji.
Mtaji unaweza kupatikana kutoka kwenye vyanzo vifuatavyo:-
(a) Akiba au mshahara
(b) Msaada au mkopo kutoka kwa ndugu na jamaa.
(c) Kuingia ubia na mtu mwenye mtaji
(d) Mkopo toka baadhi ya asasi kama vyama vya akiba na mikopo
(SACCOS), NGO za kifedha sipokuwa Benki kwani hizi huwa hazitoi mikopo
kwa mtu anayeanzisha biashara.
TARATIBU ZA KISHERIA ZA KUFUATA ILI KUANZISHA BIASHARA
Baada ya kufanya utafiti na kupanga mipango ya kuanzisha biashara
unatakiwa kwanza kuangalia taratibu za kisheria ambazo unatakiwa
kuzifuata na kuzitekeleza. Kama biashara yako ni ndogo anza kama mtu
binafsi. Faida ya kuanza biashara kama mtu binafsi ni urahisi wa
kuanzisha biashara; urahisi na wepesi wa kutoa maamuzi kwani huhitaji
ridhaa ya mtu mwingine kabla ya kutoa uamuzi; mtaji unaohitajika utakuwa
mdogo kutokana na gharama za uendeshaji kuwa ndogo, biashara hii
inaweza kuendeshwa kwa msaada wa familia kwa kumtumia mke au mume,
watoto au ndugu na jamaa na raslimali za familia kama nyumba na samani.
Unapoanzisha biashara na kuiendesha mwenyewe unakuwa huru tofauti na
mifumo mingine. Matatizo ya kufanya biashara kama mtu binafsi ni:-
Kushindwa kupanua biashara yako kwa ufinyu wa mtaji; kufilisiwa mali
zako za binafsi iwapo biashara yako itafilisika kwani katika mfumo huu
mali ya biashara na mali binafsi si rahisi kuzitenganisha; Kuongeza
mtaji inakuwa ni vigumu, hivyo unaweza kushindwa kupanua biashara yako.
Ili kuepukana na matatizo niliyoyataja hapo juu unaweza kuungana na
watu wengine kufanya biashara kwa ubia. Faida za kufanya biashara kwa
ubia ni: Kupata fursa ya kuongeza mtaji kwa kushirikiana na
wafanyabiashara wengine ambao wataleta mitaji yao; Kuongeza ujuzi katika
shughuli kwa kuleta wataalamu pale taaluma Fulani inapohitajika.
Matatizo ya kuendesha biashara kwa njia ya ubia ni: Kufilisiwa mali zako
binafsi endapo biashara yako itafilisika; kudhulumiana mali endapo moja
wa wabia atakuwa si mwaminifu ambapo anaweza kuingia mikataba mibovu na
kusababisha hasara ambayo itabebwa na wabia wote. Ni muhimu
kuwachunguza watu tunaotaka kujiunga nao ili tujue kama ni waaminifu.
Pia ni vyema kuwapo na mkataba wa maandishi mnapoanzisha biashara ya
ubia mkimshirikisha mwanasheria kama shahidi ili kujikinga na
kudhulumiana; Kufariki kwa mbia mmoja kunaweza kusababisha kuvunjika kwa
ubia; kotokuelewana kwa wabia kunaweza kusababisha kuvunjika kwa ubia.
Kama biashara ikikua unaweza kuanzisha kampuni. Mfumo wa uendeshaji wa
kampuni unazo faida zifuatazo: unatenganisha majukumu ya wamiliki mali
na kampuni yaani kampuni inaposajiliwa inakuwa inakuwa na hadhi na
kutambulika kisheria kama ni mfumo tofauti na wamiliki. Mfumo huu
unatenganisha majukumu kati ya menejimenti na wamiliki wa kampuni;
madeni ya kampuni yatalipwa hadi kufikia kikomo cha mtaji uliowekezwa na
wamiliki. Hivyo, mali binafsi za wamiliki wa kampuni haziwezi kukamatwa
kufidia madeni ya kampuni endapo kampuni itafilisika. Mfumo wa kampuni
unatoa nafasi ya kupanua mtaji kwa kukusanya mitaji kwa kuongeza
wanahisa au kupitia soko la mitaji ya hisa. Mfumo huu ndiyo unafaa kwa
biashara kubwa kwani unatoa nafasi ya kupanuka kwa biashara na kuendelea
kuwapo kwa biashara hata kama baadhi ya wamiliki wake wakifa au kujitoa
katika kampuni.
Mambo ya muhimu ya kutekeleza kisheria kabla ya kuanzisha biashara ni:-
(a) Kuwa na ofisi
(b) Kukata leseni
(c) Kusajiliwa na TRA kama mlipokodi na kupewa namba ya mlipakodi
(d) Kufanyiwa makadirio ya kodi ya mapato ya awali
(e) Kutimiza masharti mengine ya keshiria kuwa mfano kama wewe
unataka kufanya biashara ya ukandarasi wa ujenzi wa majengo lazima
usajiliwe kwenye Bodi ya Wakandarasi.
Kama unafanya biashara ya kati au kubwa unapaswa kufuata sheria. Ni
makosa kufanya biashara bila kufuata sheria za nchi. Hata hivyo, kuna
biashara zingine ndogo ndogo sana kiasi kwamba uanzishaji wake si rahisi
kufuata sheria hizo hapo juu, mfano uuzaji wa maandazi, karanga na vitu
vingine vidogovidogo. Hizi zinaitwa biashara zisizo rasmi au biashara
ndogondogo. Ni vyema ukachunguza kama biashara unayoifanya ni ndogo au
kubwa ili ujue kama unapaswa kufuata taratibu za kisheria au la, kwani
kutokujua utaratibu na sheria siyo kinga ya kukufanya usishitakiwe.
CHARLES MSULUZYA NAZI
Mwandishi wa makala hii ni mshauri wa biashara na mtunzi wa kitabu cha
Mbinu za biashara na maarifa ya kupata pesa na utajiri. Kwa mawasiliano
piga simu namba 0755394701 barua pepe cnazi2002@yahoo.com au tembelea tovuti yake http://www.squidoo.com/mshauricharles
Kutana Na Mshauri Bingwa Wa Biashara Mr CHARLES MSULUZYA NAZI
Reviewed by crispaseve
on
15:22
Rating:

Post a Comment