BASATA YALAANI TABIA CHAFU NA ISIYO NA MAADILI ILIYOONESHWA NA MSANII SHILOLE KWENYE ONESHO LAKE NCHINI UBELGIJI
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na
burudani nchini limeona picha chafu na zisizo na maadili za Msanii
Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole alipokuwa akifanya onesho lake
nchini Ubelgiji hivi karibuni.
Katika
picha hizo ambazo zimelaaniwa na watanzania wengi nchini kupitia njia
mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, Shilole anaonekana akiwa
Jukwaani huku viungo vyake vya sehemu za siri vikiwa hadharani na zaidi
akionesha tabia ambazo kwa kiasi kikubwa zimefedhehesha na kuidhalilisha
sekta ya Sanaa na Taifa kwa ujumla.
Aidha,
BASATA limepokea malalamiko kwa njia ya simu na mawasiliano ya internet
kutoka kwa watanzania waishio ughaibuni wakilaani tukio la Msanii huyo.
Katika mawasiliano yao wameeleza kwamba wamefedheheshwa na kudhalilika
na tabia hiyo chafu iliyooneshwa na msanii huyu.
Ikumbukwe
kwamba, Shilole ni msanii aliyesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa,
hivyo anapokwenda nje ya nchi kabla hajapata visa anapewa barua ya
utambulisho kama msanii wa Tanzania, hivyo anapokuwa nje ya nchi
anatambuliwa kama msanii Mtanzania, anapofanya kinyume na misingi ya
kazi ya Sanaa, anajifedhehesha yeye mwenyewe, kazi ya Sanaa na nchi yetu
pia.
Aidha,
ikumbukwe kwamba BASATA limeshapata kumwita na kumuonya msanii huyu
kutokana na tabia yake ya kutokujiheshimu pale awapo jukwaani na yeye
aliahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo chafu. Kwa hiyo kuendelea
kwake kufanya matukio hayo na kwa sasa katika ardhi ya nchi nyingine ni
uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea
kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye kujitambua na
kuiheshimu Sanaa kama kazi nyingine.
BASATA linapenda kueleza kwamba;
1. Litamuita
kwa mara nyingine tena kumtaka ajieleze kwa nini alifanya onesho hilo
la kujidhalilisha na kudhalilisha hadhi ya mwanamke, msanii na Sanaa kwa
ujumla
2. Kama
maelezo yake hayataridhisha hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi
yake maana tayari ameshadhihirisha kwamba akifanyacho si Sanaa na
hakina uhusiano na kazi ya Sanaa ambayo ina heshima yake na inahitaji
ubunifu, weledi na kujitambua.
BASATA
linawakumbusha wasanii wote nchini kuwa Sanaa ni kazi kama kazi zingine
lakini siku za hivi karibuni wasanii wengi wamekuwa wakikiuka suala
zima la maadili kwa kutengeneza kazi chafu zisizofaa mbele ya jamii ya
watanzania wanaoipenda na kuiheshimu kazi ya Sanaa yenye staha. Tuungane
kwa pamoja kukemea kazi chafu zinazozalishwa na wasanii wasiojitambua
kwani suala la maadili ni suala mtambuka na linaanzia katika ngazi ya
familia.
Aidha,
BASATA linawataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na
taratibu mara wanapopata mialiko ya kikazi kwenda nje ya nchi.
Linawakumbusha kwamba haiwezekani msanii kutumia picha chafu na mavazi
dhalili na kuonyesha utupu katika kuvuta mashabiki.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
BASATA YALAANI TABIA CHAFU NA ISIYO NA MAADILI ILIYOONESHWA NA MSANII SHILOLE KWENYE ONESHO LAKE NCHINI UBELGIJI
Reviewed by crispaseve
on
03:21
Rating:
Post a Comment