BALOZI SEIF AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA SKULI YA JAMII KATIKA KIJIJI CHA KIWENGWA UNGUJA KASKAZINI.
Othman Khamis Ame,Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Maendeleo
ya ujenzi wa Skuli ya Msingi ya Jamii katika kijiji cha Kiwengwa
Kiliomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “ B “ yanaendelea vyema katika
hatua za mwisho zitakazoiwezesha skuli hiyo kuanza kuchukuwa wanafunzi
wa Elimu ya maandalizi kuanzia mwezi Januari Mwaka ujao wa 2016.
Ujenzi
wa skuli hiyo uliohusisha pia vyoo na Tangi la Kuhifadhia maji ambavyo
vinajengwa kwa kutumia Taaluma ya Chupa za Maji zilizotiwa mchanga
unafadhiliwa na Mradi wa Kimataifa wa Give kutoka Nchini Marekani.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ujenzi wa Skuli hiyo Bwana Tahir Ali alimueleza Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyepeta fursa ya kukagua
maendeleo ya ujenzi huo kwamba Kamati hiyo kwa kushirikiana na Wananchi
kupitia ushauri wa Wizara husika ya Elimu wanatarajia kuanza usomeshaji
mapema mwakani kwa hatua ya watoto wa maandalizi.
Bwana
Tahir alisema juhudi za Wanakijiji kwa kuungwa Mkono na Shirika la
Kimataifa la Give la Marekani zimelenga kuwakomboa Watoto wa Kijiji
hicho ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikosa fursa muhimu za kielimu.
Naye
Meneja Mpya wa Mradi wa Kimataifa wa Give kutoka Marekani Bwana Joshi
Winter alisema Uongozi wa Mradi huo umejipanga vyema katika kuhakikisha
ujenzi wa Skuli hiyo unakamilika vizuri na kutoa fursa kwa watoto wa
Kijiji hicho kupata Elimu.
Meneja
wa Mradi huo wa Give ameuomba Uongozi wa Kijiji hicho kwa kushirikiana
na Serikali Kuu kuandaa mazingira ya kupata eneo kubwa zaidi kwa ajili
ya matayarisho ya ujenzi wa Majengo ya Sekondari katika Skuli hiyo ya
Jamii Kiwengwa ambapo Taasisi yake itakuwa tayari kusaidia ufadhili.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema
Taasisi hiyo ya Kimataifa inafaa kupongezwa na wapenda Elimu hapa Nchini
kutokana na hatua yake ya kuunga mkono makundi ya jamii katika
kujikomboa kielimu.
Balozi
Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi za
taasisi na mashirika ya maendeleo ndani na nje ya nchi yaliyojitolea
kusaidia Wananchi hasa wanaoishi katika mazingira magumu ya kimaisha
ambayo huwa kikwazo cha kupata elimu.
Taaluma
ya matumizi ya chupa za Maji zinazotiwa mchanga iliyobuniwa Nchini
Nicaragua Amerika Ya Kusini katika ujenzi wa majengo mbali mbali ya
makazi na huduma za Kijamii inatumika kwa lengo la kutunza mazingira.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikagua maendeleo ya ujenzi wa
Skuli ya Jamii katika Kijiji cha Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.Kushoto
ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Skuli hiyo Bwana
Tahir Ali, Kulia yake Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi
ambapo nyuma yao ni jengo la Vyoo lililojengwa kwa kutumia chupa za maji
zilizotiwa mchanga.
Balozi
Seif Ali Iddi wa kwanza kulia akimpongeza Meneja wa Mradi wa Kimataifa
wa Give kutoka Nchini Marekani Bwana Josh Winter kutokana na Taasisi
yake kusaidia maendeleo ya Elimu Zanzibar.Picha na –OMPR – ZNZ.
BALOZI SEIF AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA SKULI YA JAMII KATIKA KIJIJI CHA KIWENGWA UNGUJA KASKAZINI.
Reviewed by crispaseve
on
07:31
Rating:
Post a Comment