Header AD

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA UBUNIFU

Ofisa Mwandamizi wa Maendeleo ya Jamii, Idara ya Kuondoa Umasikini katika Wizara ya Fedha, William Ghumpi akimpatia Kitabu cha Taarifa ya Utekelezaji wa Malengo ya Milenia 2014, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, HAB Mkwizu, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam jana. Wapili kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma. (Picha na Kassim Mbarouk).

Na Salma Ngiwilizi – Maelezo
SERIKALI imewataka watumishi wa umma nchini kuonyesha ubunifu na weledi  katika utendaji kazi wa majukumu yao mbalimbali ili kuweza kukidhi matarajio ya wananchi.

 Aidha  imewasisitiza watumishi  wa umma wanawake  kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na ufanisi  ili kuonyesha uwezo  wao na uhodari   katika kutekeleza majukumu  yao.

Kauli hiyo ilitolewa jana  na Kaimu Katibu Mkuu  wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma HAB Mkwizu wakati  akifungua maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,  Mhe. Celina Kombani yanatoendelea kwenye  viwanja vya Mnazi  Mmoja.

Kauli mbiu ya maonesho hayo ni “Utumishi wa Umma katika Bara la Afrika ni chachu ya kuwawezesha Wanawake  kuongeza Ubunifu na Kuboresha utoaji wa Huduma kwa Umma”.

Serikali imetoa miongozo mbalimbali ya kisera inayokusudia kumpa mwanamke wa nchi  hii fursa sawa ya kuchangia maendeleo ya nchi yetu.

Baadhi ya miongozo hiyo ni pamoja na Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996, Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000, na mwongozo wa anuai za jamii mwaka 2010.

 Alisema  hadi sasa utekelezaji wa miongozo hii umeleta matokeo chanya ambapo nchi yetu inajivunia kufikia mafanikio kadhaa , ambayo ni pamoja kuongezeka kwa idadi hya wanawake katika ngazi  za maamuzi Serikalini kutoka asilimia 26 mwaka 2005 na kufikia  asilimia 34 mwaka 2014.

“Wale waliopata nafasi walizopewa au kupata kutokana na juhudi zao. Ujuzi au uzoefu wao wanazitendea haki kwa kusimamia vizuri wale walio chini yao na kutoa huduma bora iliyotukuka kwa wananchi,” alisisitiza.

 Aliongeza kuwa  mafanikio  mengine ni kujenga uwezo wa watumishi wanawake kupata sifa za ziada ,kuongeza ubunifu na kuboresha upatikanaji wa huduma na Serikali imekuwa ikitoa ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili kwa wanawake katika Vyuo Vikuu vya hapa nchini. 

Hivyo katika kipindi cha miaka 10 jumla ya watumishi wanawake 251 walipatiwa ufadhili na kuhitimu masomo yao katika shahada mbalimbali  za uzamili.

 Alitoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kutoka asasi za kiraia,sekta binfasi na vyombo vya habari kuendelea kutoa mchnago katika kuhimarisha Utumishi wa Umma  katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA UBUNIFU WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA UBUNIFU Reviewed by crispaseve on 02:54 Rating: 5

No comments

Post AD