HAMAD RASHID ATAKA CUF IJITOE SERIKALI YA MSETO
MBUNGE wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), amelaani matumizi ya nguvu za
Jeshi la Polisi wakati wa chaguzi mbalimbali huku akikishauri chama chake
kujiondoa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa baina yao na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kutokana na kutowasaidia wananchi.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, Hamad alisema kuwa
ameshangazwa na nguvu kubwa ya Jeshi la Polisi iliyotumika katika uchaguzi mdogo
wa Bububu uliomalizika hivi karibuni na hivyo kusababisha kujeruhi wananchi bila
sababu.
Alisema CUF iliingia katika serikali ya mseto kwa lengo la kuweka uhuru na
haki lakini wameshindwa kufikia azima hiyo na kwamba ikiwa muafaka huo ni kwa
maslahi ya watu wachache basi wajitoe.
“Mimi nashangaa sana hayo mazungumzo sijui yalikuwa ya nini na ‘ndoa’ ilikuwa
ya nini kama ilikuwa ni kwa masilahi ya watu wachache huku wananchi hawanufaiki
nayo, wanapigwa risasi, basi CUF wajiondoe kama si kwa masilahi ya wananchi
wote,” alisema Hamad.
Hata hivyo, Hamad alisema Serikali ya Zanzibar inaundwa na vyama viwili,
hivyo ni dhahiri kwamba CCM na CUF ndio wametumia nguvu katika kuvikandamiza na
kuhujumu vyama vidogo vya siasa ambavyo havikuwa na serikali.
Katika uchaguzi huo wa Jumapili ambao CCM iliibuka kidedea ikifuatiwa na CUF
na Chama kipya cha ADC, vurugu kubwa zilizuka huku matokeo hayo yakipingwa
vikali.

Post a Comment