MRISHO NGASA KUICHEZEA YANGA BURE, AOMBA MASHABIKI WA SOKA WAMCHANGIE KULIPA DENI ANALODAIWA NA SIMBA.
Mrisho Ngassa alichukua pesa
ya Simba kimya kimya, akavinjari mitaani na kupiga dili zake, siku
zikasonga, maisha yakaenda ikafika siku akasaini mkataba mwingine na
Yanga.
Hata hivyo, Shirikisho linalosimamia soka nchini (TFF) limemwamuru
azirudishe fedha hizo alizochukua Simba pamoja na faini juu. Ngassa
hakuwa na kinyongo, Ijumaa jioni iliyopita akiwa na begi lake akatinga
ofisi za TFF kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam na kulipa kwa
kutumia hundi ya Sh45 milioni.
Ngassa, ambaye amecheza mechi yake ya kwanza ya Yanga Jumamosi
iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting sasa ameibuka na kuwaomba mashabiki wa
Yanga wenye nia njema wamchangie kuziba pengo alilonalo mfukoni kwa vile
adhabu aliyopewa imemgharimu sana. Unajua Sh45 milioni si mchezo!
Mchezaji huyo ambaye amemaliza adhabu yake ya kutokucheza mechi sita
ametamka maneno haya kwa huruma: “Nawaomba watu ambao wana nia ya dhati
kunichangia niweze kurudisha fedha zangu kwenye namba yangu ya simu au
akaunti yangu ya CRDB ambayo ni 01J2095037800.’’
Ngassa alidai kwamba fedha hizo alizilipa mwenyewe kutoka mfukoni
kwake na sasa amebaki katika wakati mgumu ndiyo maana anaomba wasamaria
wema kutoka Yanga kujipigapiga na kumchangia kitu kidogo kwenye akaunti
yake hiyo na kwenye simu yake.
Katika hatua nyingine, mchezaji wa zamani wa Simba, Yusuph Macho
‘Musso’ alisema hakuna mchezaji mwenye rekodi ya kucheza misimu mingi
kwenye ligi pasipo kuchuja kama Ngassa hatua ambayo amesema ni mchezaji
bora wa Afrika Mashariki kwa sasa.
“Ni mchezaji ambaye ananishangaza kwa kasi yake
uwanjani, amecheza ligi kwa misimu mingi lakini hajawahi kuchuja wala
kasi yake kupungua kuanzia kwenye timu yake mpaka Taifa Stars, ni winga
pekee kwa sasa Afrika Mashariki,” alisema Musso alipozungumza na
Mwanaspoti mjini Dodoma.
MRISHO NGASA KUICHEZEA YANGA BURE, AOMBA MASHABIKI WA SOKA WAMCHANGIE KULIPA DENI ANALODAIWA NA SIMBA.
Reviewed by crispaseve
on
12:21
Rating:
Post a Comment