Header AD

MILIONI 80KUNUNUA GARI YA WANAFUNZI IFUNDA




MILIONI 80KUNUNUA GARI YA WANAFUNZI IFUNDA

Na Denis Mlowe,Iringa

ZAIDI ya shilingi milioni 80 zinatarajia kutumika katika ununuzi wa gari ya wanafunzi wa shule ya wasichana Ifunda iliyoko katika wilaya ya Iringa vijijini mkoani Iringa.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Zaina Salingwa alisema hayo katika harambee iliyofanyika sambamba na mahafari ya nane ya kidato cha sita shuleni hapo kuwa kuna changamoto kubwa ya usafiri wa wanafunzi katika shule hiyo na wanatarajia kukusanya fedha hiyo kuweza kuondokana na hali hiyo.

Alisema shule inakabiliwa na wakati mgumu inapojitokeza dharula katika kutekeleza majukumu ya shule na wanafunzi wanapohitaji gari wakipatwa na matatizo hususani katika kipindi cha ugonjwa.

“Tunaomba wadau mbalimbali, wazazi na makampuni mbalimbali kutuchangia katika ununuzi wa gari la wanafunzi ambalo bei yake ni kubwa hivyo tunategemea sana misaada kutoka kwao” alisema Salingwa

Aidha alisema kuwa shule hiyo ina upungufu wa vitabu kwa wanafunzi  na tatizo la walimu katika masomo ya Hisabati, Fizikia, Kemia na baiolojia na kuongeza kuwa shule ina walimu wawili wa somo la hisabati, walimu wawili kemia na mwalimu mmoja wa somo la fizikia huku idadi ya wanafunzi wanaosoma sayansi ni kubwa na kuitaka serikali kuwaongezea walimu.

Salingwa alisema miundo mbinu ya shule imechakaa kutokana na kujengwa zaidi ya miaka 30 iliyopita na kukabiliana na uchakavu wa vyoo, jiko, mifumo ya umeme na maji taka.

“ Shule hii inakabaliwa na uchakavu wa maeneo yake hii inahatarisha usalama wa mali za shule, mali za wanafunzi na maisha yao, tunaomba serikali na wadau  mbalimbali pia katika hili watusaidie ukarabati unaohitaji fedha nyingi.” Alisema Salingwa

Kwa upande wao wanafunzi wa wanaotarajia kuhitimu kidato cha sita katika risala iliyosomwa na Hildegarda Colman walisema gari la shule imekuwa changamoto kubwa katika shule hiyo na mara nyingi mwanafunzi anapougua na kulazimika kusafirishwa kwenda hospitalini nyakati za usiku inawawiha vigumu kupata usafiri.

Colman alisema shule inakabiliwa na upungufu wa vitabu kwa masomo yanayotolewa hapo ya sayansi japokuwa kila mwaka vinanunuliwa lakini vimekuwa havitoshelezi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi.

Aidha alisema shule ya wasichana Ifunda inakabiliwa na ukosefu wa maktaba hivyo wanalazimika kutumia chumba cha darasa kwa matumizi ya maktaba ambayo hata hivyo haikidhi mahitaji ya wanafunzi.

“Tunakabiliwa na ukosefu wa kompyuta hata moja kwa matumizi ya wanafunzi kama unavyojua mabadiliko ya dunia, mitaala inabadilika, kukosekana kwa kompyuta kunatunyima fursa ya kuendana mabadiliko hayo, tunaomba tusaidiwe hata komputa chache tujifunze na tuzitumie kutafuta maarifa ya kitaaluma” alisema Colman

Katika harambee Kampuni ya Asasi ilichangia jumla ya shilingi milioni 3 na jumla ya fedha zilizopatikana ni shilingi milioni 9.7 zilipatikana kati ya hizo fedha taslimu shilingi milioni 5.5 na ahadi shilingi milioni 4.2.
MILIONI 80KUNUNUA GARI YA WANAFUNZI IFUNDA  MILIONI 80KUNUNUA GARI YA WANAFUNZI IFUNDA Reviewed by crispaseve on 09:48 Rating: 5

No comments

Post AD