MOURINHO YUPO TAYARI KUIFUNDISHA UNITED HATA LEO KAMA MOYES AKIFUKUZWA
LONDON, England
MARA baada
ya Kocha Sir Alex Ferguson wa Manchester United kutangaza kuwa
atastaafu kufundisha soka, majina mengi ya makocha watakaochukua nafasi
yake yalitajwa. Jose Mourinho ambaye kipindi hicho alikuwa akiinoa Real
Madrid, alikuwa mmoja wa waliotajwa kwa wingi.
Bahati
haikuwa yake, Kocha David Moyes aliyekuwa Everton akapata nafasi hiyo,
wengi hawakutegemea, lakini inavyoonekana Mourinho aliumia, kwani
inaaminika ana mapenzi na Man United na bado anatamani kuifundisha timu
hiyo licha ya kuwa sasa ni bosi wa Chelsea.

Kutokana
na mwenendo mbaya wa United kipindi hiki, baadhi ya wachambuzi wa soka
wanaamini kuna uwezekano mkubwa wa kocha huyo kukubali kuifundisha
United hata leo hii endapo itatokea United imemtimua Moyes, kisha yeye
akahitajika kutua klabuni hapo.
Zifuatazo
ni sababu chache zinazoonyesha kocha huyo raia wa Ureno ana mapenzi na
timu hiyo maarufu kwa jina la Mashetani Wekundu licha ya kuwa anaiongoza
vema Chelsea:
Kuonyesha heshima anapokutana nayo
Achana na ile mara ya kwanza alipokuwa Porto, tangu Mourinho alipoondoka
England mara ya kwanza, amekuwa akiizungumza vizuri United na kuonyesha
heshima kubwa kwa Ferguson tofauti na makocha wengine.

Wakati alipokuwa Madrid, siku timu yake ilipocheza dhidi ya United,
Mourinho alionekana kuwa mwenye nidhamu kubwa tofauti na awapo uwanjani
wakati timu yake ikicheza dhidi ya timu nyingine.
Hata mara baada ya mechi hiyo ambayo Madrid ilishinda, alisema: "Timu bora imepoteza mchezo.”
Kumtetea Alex Ferguson
Wakati Ferguson alipomweka benchi straika wake tegemeo, Wayne Rooney,
katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, Mourinho alisema: "Sir
Alex ameshinda kwa kufanya maamuzi mengi magumu, kila anachofanya yupo
sawa na haihitaji maswali, ni kocha aliyetengeneza historia."
Kuitetea United ilipoyumba
Mwanzoni mwa msimu huu, United ilikuwa ikiyumba kama ilivyo sasa,
haikupata matokeo mazuri, lakini Mourinho alipoulizwa alisema: “United
ni United, inaweza kufanya lolote na muda wowote.”

United bado ni timu kubwa
Mourinho yupo Chelsea, ni timu kubwa lakini kwa sifa na rekodi za ubora
bado haijafikia kuwa daraja moja sawa na AC Milan, Barcelona, Liverpool,
Real Madrid, Juventus na Inter Milan, hivyo nafasi hiyo ni kubwa.
Heshima kila anapocheza dhidi ya United
Mara kadhaa imewashangaza wengi kuwa Mourinho anapocheza dhidi ya timu
kubwa nyingine ni jambo la kawaida kukwaruzana na wapinzani, iwe
wachezaji au makocha, lakini anapofika Old Trafford huwa anaonyesha
heshima na kuwa mstaarabu.
Hana maneno ya ‘shombo’ akikutana na Mashetani hao, lakini mara nyingi
amekwaruzana na mabosi wa timu nyingine kama vile Manchester City na
Arsenal.
Kujulishwa na Ferguson kinachoendelea
Hivi karibuni Mourinho alisema mara baada ya United kufanya maamuzi ya
kumchukua Moyes, alipata taarifa hizo mapema kutoka kwa Ferguson
mwenyewe, wengi wanajiuliza kwa nini kocha huyo mkongwe alienda
kumjulisha! Wanaamini kuna ukaribu zaidi ya urafiki juu ya taarifa hizo.
Katika kura za maoni zilizopigwa kwenye mitandao barani Ulaya
zinaonyesha kuwa mashabiki wengi wa United wamekubali hoja kuwa United
ingemchagua Mourinho kuliko Moyes.
Kura hizo zipo hizi
Wanaomtaka Mourinho 80.9%
Wasiomtaka Mourinho 19.1%
Jumla ya kura: 8,114
Wewe
shabiki wa Tanzania unadhani Mourinho alikuwa ni mtu sahihi kuinoa
United? Tuma maoni katika namba 0719 137090. Maoni yako yatachapishwa
Ijumaa ijayo katika gazeti hili
MOURINHO YUPO TAYARI KUIFUNDISHA UNITED HATA LEO KAMA MOYES AKIFUKUZWA
Reviewed by crispaseve
on
03:08
Rating:
Post a Comment