MWANAMKE ALIYEOA WANAUME WAWILI
MWANAMKE
mkazi wa kijiji cha Ikandamoyo, wilayani Katavi, Veronica Saleh ‘Mama
Kaela’ (50), amefanya uamuzi adimu wa kuolewa na wanaume wawili ambao
anaishi nao kijijini hapo.
Kijiji
hicho kipo umbali wa takribani kilometa 30 kutoka mjini hapa katika
Jimbo la Katavi linalowakilishwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Pamoja na
ndoa hiyo iliyowezeshwa na mume mkubwa kukubali kuishi na mume mdogo,
imeelezwa kuwa mwanamke huyo ndiye ‘aliyewaoa’ wanaume hao kwa zaidi ya
miaka saba sasa, huku akiwa na amri kuu katika nyumba, kama ilivyo
katika ndoa za kawaida.
Wanaume hao ni Paulo Sabuni ‘Baba Kaela’ (60) ambaye ndiye mume mkubwa na Arcado Mlele (45) ambaye ni mume mdogo.
Taarifa
za kuwapo kwa ndoa hiyo ya aina yake, ziliifikia Globu ya Jamii na
kufanyiwa uchunguzi kwa zaidi ya wiki tatu, na hatimaye katikati ya wiki
hii, wahusika walikubali wao wenyewe kuzungumzia suala hilo. Kwa mujibu
wa maelezo ya mwanamke huyo ambaye alionekana kuwa msemaji wa familia
hiyo, yeye na mumewe mkubwa, walifika kijijini hapo miaka 24 iliyopita,
wakitoka kijiji cha Usumbwa mpakani mwa Chunya, Mbeya na Tabora.
Wakiwa
kijijini hapo mume wake aliendelea kufanya kazi ya ukulima wakati yeye
mama (Veronica), pamoja na kilimo hujihusisha na upishi na uuzaji wa
pombe ya kienyeji iitwayo kayoga.
Mwanamke
huyo ambaye amesema ana watoto wanne, Alfred (20), binti mwenye miaka 16
(ambaye ameolewa) na wengine wawili wa kiume, mmoja akisoma darasa la
sita na mdogo ana miaka saba, amesema hana shida na waume wake.
Ingawa
wanandoa hao walizungumza kwa hadhari, majirani walikiri kuwa mwanamke
huyo anaishi na wanaume hao wawili kwa amani na kwamba mwanamke huyo
ndiye mwenye sauti na si waume zake.
“Si siri
tena sasa, tumeshawazoea, kwani wanaishi kwa amani ila yule mume mdogo
anaishi kwenye nyumba aliyoachiwa na marehemu baba yake, lakini
anashinda kwa mume mkubwa, ambapo inajulikana kijijini hapa kuwa ni
nyumba kubwa. “Basi pale ni mambo yote, kula na kunywa, mama huyu
amewapangia zamu wanaume hao kama afanyavyo mume mwenye wake wengi.
Ama kweli
ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni,” alisema mkazi mmoja kwa
masharti ya jina lake kutoandikwa gazetini. Ilielezwa, kwamba wanaume
hao wana akili timamu na hawatumii kilevi cha pombe kama ilivyo kwa mke
wao.
Hata
hivyo, mume mkubwa anapewa sifa za upole tofauti na mume mdogo
anayetajwa kuwa mkorofi kiasi cha mara kadhaa kumchapa makofi mkewe
anapomuudhi.
Majirani
wanadai kwamba Mama Kaela na mumewe Paulo, walipofika kijijini hapo,
walipokewa na kuishi maisha ya kawaida, lakini baadaye mama huyo alianza
kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Arcado, ambaye naye alilazimika
kuachana na mkewe wa ndoa anayefahamika kijijini hapo kwa jina la Mama
Pere.
Ilielezwa
na mashuhuda hao kwamba mume mkubwa alipobaini uhusiano huo, alikuja
juu, lakini mwanamke huyo inadaiwa alimweleza mumewe huyo, atake asitake
lazima wataishi wawili, vinginevyo ataachana naye, ndipo mume mkubwa
alipokubali kuishi na mume mwenza.
Katika
maisha ya kawaida katika familia hiyo, inaelezwa kwamba katika baadhi ya
siku ikitokea kuwa mama huyo amechoka kupika, mume mdogo huchukua
jukumu la kupika na kumwandalia chakula na maji ya kuoga mume mkubwa.
“Lakini
mara nyingi kwa mfano, ikiwa ni zamu ya mama huyo kulala kwa mumewe
mkubwa, basi humfulia nguo zake kisha anakwenda kwa mumewe mdogo nako
anamfulia nguo.
“Ndivyo
wanavyoishi, nasi sasa tumewazoea ila yule mama ni mkali na ana sauti
pale kwake kwa wanaume wale ila tunaona kama ana wivu sana kwa huyu
mdogo ambaye naye pia ana wivu kwa mkewe huyo, labda anahofia kuwa mama
huyo anaweza kuongeza mwanamume mwingine,” anasema mmoja wa majirani
hao.
Hakuna
mazuri yasiyokuwa na machungu, japo familia hiyo inaelezwa kuwa na
amani, mtoto wao mdogo nusura avuruge uhusiano wa wanandoa hao, baada ya
kuibuka mzozo wakati wa maandalizi ya ubatizo wake.
Kwa
sababu anazojua mama, ingawa inafahamika kuwa wote ni watoto wa mume
mkubwa, mke huyo katika hati za ubatizo aliandikisha ubini wa mtoto huyo
kuwa ni Mlele (akimaanisha kuwa mtoto wa mume mdogo), lakini mume
mkubwa aliweka pingamizi kanisani akidai yeye ndiye baba halali wa mtoto
huyo.
Kwa
mujibu wa mwanamke huyo, yeye na Arcado ni waumini wa madhehebu ya
Katoliki wakati Paulo ni Mpentekoste. Madai ya mzozo wa uhalali wa
`ubaba’ wa mtoto huyo, yalithibitishwa na baadhi ya wakazi wa kijiji
hicho, akiwamo mwalimu wa dini wa Kigango cha Kanisa Katoliki Uruira,
Mashaka Abel. Walisema miaka sita iliyopita, mtoto huyo akiwa na umri wa
mwaka mmoja, alifanyiwa taratibu za ubatizo, lakini ilishindikana,
kutokana na wanaume hao, kila mmoja kudai ndiye baba mzazi wa mtoto.
“Lilikuwa
jambo la kustaajabisha sana, kwani familia hiyo ilifanya maandalizi
yote ya sherehe ya ubatizo wa mtoto huyo, lakini siku hiyo kanisani
wakati huo ilikuwa ni kigango cha Katumba ambacho sasa ni Uruira, sakata
lilianzia pale Padri alipomwuliza mama wa mtoto huyo ubini wa mtoto
naye akasema ni Mlele.
“Hapo
ndipo mume mkubwa alipopinga na kudai kuwa mtoto yule si wa Arcado bali
wake na yeye ndiye baba halali. Padri hakuamini, aliuliza tena na tena
na majibu yakawa ni yale yale, ndipo ubatizo ukashindikana,” alisema
Katekista Abel.
Kazi ya
kutafuta undani wa ndoa hiyo haikuwa rahisi kutokana na mazingira ya
woga na usiri uliokusudiwa kubaki, ambapo awali mama alisema kwamba mume
wake ni Paulo pekee japo siku ambayo mwandishi wa habari hizi alifika
kijijini hapo na baadaye nyumbani kwa wanandoa hao na kumkuta mume mdogo
(Arcado akimsaidia mkewe kukoroga pombe. Awali katika utambulisho,
walidai kuwa ni mtu na mdogo wake na kusita kuzungumzia maisha yao ya
kifamilia.
Mke wao
ambaye alionekana wazi kuwa ni msemaji mkuu alifoka na kuja juu, akidai
kuwa hayuko tayari kuzungumzia uhusiano wake na wanaume hao wawili,
ingawa alikiri kuwa wanaishi pamoja.
"Kwa hiyo
umefunga safari yote hii kutoka huko ulikotoka ili uje kwangu mie
Veronica … nasema sitaki kabisa mtu kuja hapa na kutaka kunivurugia
mpangilio wa maisha yangu, kwanza nani alikueleza hayo, wambea wakubwa
hao yanawahusu nini watu hao?” alihoji.
“Mie mume
wangu ni huyu Paulo basi … sasa leo umeniachia vurugu ndani ya nyumba
nitapigwa na huyo mume wangu Paulo, kwani mmenishikisha ugoni?” alifoka
Mama Kaela. Hata hivyo, mume mkubwa alidai kuwa hatamwadhibu mkewe huyo
na kwamba wataendelea kuishi pamoja na mdogo wake Arcado kwa amani. Hata
hivyo, akina mama wengi kijijini hapo wanalaani kitendo cha mama huyo
kuishi na wanaume wawili ambapo waliomba uongozi wa Kanisa uingilie
kati, ili mama huyo aweze kufunga ndoa na mume mmoja.
MWANAMKE ALIYEOA WANAUME WAWILI
Reviewed by crispaseve
on
15:13
Rating:
Post a Comment