TATHMINI YA ARDHI YA BANDARI MPYA YA MBEGANI YAKAMILIKA
Meneja
Miradi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Bw. Alexander Ndibalema (Kulia
aliyesimama) akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya Timu yaUkaguzi
wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango,
wawakilishi wa wanavijiji vya Mradi wa Bandari Mpya ya Mbegani na Timu
ya Uthamini wa Ardhi wa eneo la mradi. Waliokaa viti vya mbele ni
viongozi wa Timu ya ukaguzi, Bibi Florence Mwanri (Wapili Kulia) na
Prof. Longinus Rutasitara (Watatu Kulia). Kushoto ni Mratibu wa ziara
hiyo, Bibi Salome Kingdom.
Mmoja
wa viongozi wa Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kulia) akizungumza katika
mkutano huo.
Mthamini Mkuu wa Ardhi ya Mradi huo, Mhandisi Emmanuel Mrema (Kulia) akizungumza katika mkutano huo.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Pande, Bw. Ubezi Kondo (Kulia aliyesimama) akizungumza
wakati Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango ilipopita kijijini hapo kujua hali ya zoezi la tathmini ya
ardhi kwa ajili ya mradi wa Bandari Mpya ya Mbegani. Kulia kwake ni
Mmoja wa viongozi wa Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri na Mthamini Mkuu wa Ardhi
ya Mradi huo, Mhandisi Emmanuel Mrema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Pande, Bw. Ubezi Kondo (Kushoto) akionesha eneo itakapokuwepo Bandari Mpya ya Mbegani. Wanaotazama ni Meneja Miradi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Bw. Alexander Ndibalema (Kulia), Mthamini
Mkuu wa Ardhi ya Mradi huo, Mhandisi Emmanuel Mrema (Wapili Kulia) na
Mmoja wa viongozi wa Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Watatu Kulia).
Meneja Miradi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Bw. Alexander Ndibalema (Kulia) akitoa maelezo juu ya maendeleo ya Mradi wa Bandari
Mpya ya Mbegani katika eneo itakapokuwepo bandari hiyo.
Wanaomsilikiliza ni Timu Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya
Rais, Tume ya Mipango. Picha na Saidi Mkabakuli
======== ========= ========
TATHMINI YA ARDHI YA BANDARI MPYA YA MBEGANI YAKAMILIKA
Na Saidi Mkabakuli
Tathmini iliyokuwa ikifanyika katika kutimiza ndoto ya kuwa na Bandari mpya ya Mbegani kufikia mwaka 2017 na kutekeleza Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16) imekamilika
kwa takribani asilimia 90 ya eneo zima la mradi huo.
Hayo
yamedhihirishwa na Mthamini Mkuu wa Ardhi ya Mradi huo, Mhandisi
Emmanuel Mrema wakati akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja naTimu
ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
ilipofanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo.
Mhandisi
Mrema alisema kuwa mpaka sasa jumla ya kaya 1100 kutoka vitongoji vya
Bisibisi, Mji Mpya, Mlingotini na Pande vimeshafanyiwa tathmini, ambapo
makadirio ya awali yanaonesha jumla ya shilingi bilioni 23 zinatarajiwa
kulipwa kupisha mradi.
“Mpaka
sasa takribani asilimia 90 ya eneo la mradi ambalo ni sawa na hekta
2000 limeshakamilika, ambapo kwa mujibu wa mapendekezo ya tathmini
tunatarajia malipo kufanyika kufikia mwezi Juni mwaka huu,” alisema
Mhandisi Mrema.
Akizungumza
katika mkutano huo, mmoja wa viongozi wa Timu Ukaguzi wa Miradi ya
Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri
alisema kuwa kuna haja ya kuhakikisha fidia kwa wanavijiji hao inalipwa
kwa wakati ili kuondoa usumbufu wa kusubiri malipo ya kwa muda mrefu
hali itakayochochea kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi.
“Nawaomba
muhakikishe malipo yanafanywa kwa wakati ili kuwaondoshea usumbufu
wananchi ili kulinda heshima ya Serikali na kuondosha kero ya kusubiri
ya kusubiri kwa muda mrefu,” alisema Bibi Mwanri ambaye ni Naibu Katibu
Mtendaji anayeshughulikia Huduma za Jamii na Maendeleo ya Idadi ya Watu.
Akijibu
hoja ya ushirikishwaji wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha
Pande, Bw. Ubezi Kondo alisema kuwa kwa kiasi kikubwa wamekuwa
wakishirikishwa katika kila hatua ya uthamini huo. Aliongeza kuwa hali
hii imewaongezea hamasa ya kuupisha mradi huo ili kutimiza ndoto ya
Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete ya kujenga Bandari hiyo pamoja na ahadi
aliyoitoa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1968.
“Kwa
hakika tunaukubali mradi huu kwa mikono miwili ili kutimiza ndoto na
ahadi za Rais Kikwete na ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa mwaka 1968 wakati
akifungua Chuo cha Mbegani ambapo aliahidi kuwa atahakikisha kunajengwa
Bandari ya kisasa Mbegani,” alisema Bw. Kondo.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mtendaji (Uchumi Jumla), Prof.
Longinus Rutasitara ambaye ni kiongozi mwenza wa ukaguzi huo, uwekezaji
katika Bandari mpya ya Mbegani unatoa fursa za kimkakati katika kufikia
malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 -
2015/16).
“Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16) unaweka
bayana kuwa uwekezaji wa Bandari ni mojawapo ya maeneo ya kipaumbele na
kimkakati ambapo kukamilika kwa ujenzi wa bandari mpya ya Mbegani
Bagamoyo kunatarajiwa kupunguza msongamano wa meli katika bandari ya Dar
es Salaam,” alisema Prof. Rutasitara.
Serikali
imeaandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ukiwa na lengo la kuwa na
mfumo madhubuti wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo la
Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025.
TATHMINI YA ARDHI YA BANDARI MPYA YA MBEGANI YAKAMILIKA
Reviewed by crispaseve
on
13:45
Rating:
Post a Comment