UJUMBE WA BABA MTAKATIFU FRANCISCO KWA KIPINDI CHA KWARESMA 2014
Mama
Kanisa anakianza kipindi cha Kwaresima, yaani siku arobaini za toba na
wongofu wa ndani; kusali na kufunga; kusoma na kulitafakari Neno la
Mungu pamoja na kumwilisha imani katika matendo, kwa Jumatano ya Majivu.
Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi
tena.
Hizi ni
nyakati za toba na zimewekwa na Mama Kanisa kwa ajili ya mazoezi ya
maisha ya kiroho; zinajikita katika liturujia ya toba, kuhiji kama
ishara ya toba, kujinyima kwa hiyari kama sehemu ya kufunga na kutoa
sadaka kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; ni
mwaliko wa kushiriki kidugu kazi za mapendo na kimissionari
zinazotekelezwa na Mama Kanisa.
Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka
2014 unaongozwa na kauli mbiu “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu
Kristo, Jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri,
ili kwamba, ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”. Huu ni mwaliko
kwa waamini kuonesha moyo wa ukarimu kwa jirani zao kama ilivyokuwa
nyakati za Mtakatifu Paulo aliyewahimiza Wakorintho kuwasaidia ndugu zao
waliokuwa wanateseka mjini Yerusalemu.
Baba Mtakatifu katika tafakari hii anaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi
Mungu ambaye ni tajiri na mwingi wa rehema kwa njia ya Yesu Kristo,
Mwanaye wa pekee amejinyenyekesha na kuwa maskini, ili aweze kuwa karibu
na binadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Hiki ni kielelezo cha
upendo wa Mungu ambao ni neema na baraka inayotolewa kwa binadamu
anayependwa na Mwenyezi Mungu, kiasi cha hata Kristo kujisadaka maisha
yake.
Huu ndio upendo unaoshirikisha, unajenga na kuimarisha umoja na udugu
kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho,
Mwenyezi Mungu amefikiri na kutenda kama binadamu katika mambo yote
isipokuwa hakutenda dhambi.
Kwa njia ya umaskini wa Yesu, Mwenyezi Mungu amependa mwanadamu aweze
kutajirika, hii ndiyo mantiki ya Fumbo la Umwilisho na Fumbo la
Msalaba. Alibatizwa mtoni Yordani si kwa vile alikuwa anahitaji toba,
wongofu wa ndani na msamaha, bali alipenda kuonesha mshikamano wa dhati
na binadamu mdhambi kwa kujitwika dhambi zake mabegani mwake, ili aweze
kuwafariji, kuwaokoa na kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na
mauti.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka
huu anasema, Yesu alijifanya kuwa jirani na Msamaria mwema, kwa kuguswa
na mahangaiko ya binadamu, ili hatimaye, aweze kumwonjesha huruma na
mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Utajiri wa Yesu
unajionesha kwa namna ya pekee kwa kumtegemea Baba yake wa mbinguni,
katika kutekeleza mapenzi yake na hatimaye kuvikwa taji la utukufu. Yesu
anatambua kwamba, ni Mwana pekee wa Mungu, Masiha anayewaalika wafuasi
wake kujitajirisha kutoka kwake na kushiriki udugu na kujitahidi
kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa kuishi kama watoto wa Mungu na
ndugu zake Kristo.
Kila wakati Mwenyezi Mungu anaendelea kumkomboa mwanadamu kutoka
katika umaskini wake kwa njia ya umaskini wa Yesu, kwa kuonja na kuguswa
na umaskini wa jirani zao tayari kujifunga kibwebwe kusaidia kupambana
na umaskini: wa hali, kipato na maadili. Umaskini ni kielelezo cha
kukosa imani, mshikamano na matumaini. Umaskini wa kipato unawakumba
wote wanaoishi katika mazingira ambayo ni kinyume kabisa cha utu na
heshima ya binadamu.
Hawa ni watu wanaopokonywa haki na mahitaji msingi kama vile:
chakula, maji, malazi, huduma bora za afya, fursa za kazi na ajira,
maendeleo na ukuaji wa kitamaduni. Kanisa linaendelea kujisadaka kwa
ajili ya kupambana na umaskini wa kipato katika mikakati yake ya
kichungaji inayopania kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa
linaiona na kuitambua sura ya Kristo miongoni mwa maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa linapania kuhakikisha kwamba,
utu na heshima ya binadamu vinaendelea kupewa kipaumbele cha pekee kwa
kukomesha ubaguzi ambao wakati mwingine ni chanzo kikuu cha umaskini.
Kanisa linahimiza matumizi bora ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya
ustawi na maendeleo ya wengi. Jamii iongozwe katika misingi ya haki,
usawa, kiasi na ushirikiano.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna umaskini wa kimaadili,
unaomfanya mwanadamu kuwa ni mtumwa wa dhambi, ulevi wa kupindukia,
mcheza kamari na mtazamaji wa picha za ngono. Hili ni kundi la watu
lililopoteza dira na mwelekeo wa maisha kwa kukata tamaa! Ni watu
wanaoogelea katika utupu kwa kukosa fursa za ajira pamoja na kuendelea
kudhalilishwa utu na hehima yao kama binadamu: wanakosa chakula na
malazi; hawana haki ya kupata huduma bora katika sekta ya elimu, afya na
maendeleo. Matokeo yake ni watu kuelemewa mno na umaskini wa kimaadili
kiasi hata cha kutema zawadi ya maisha!
Umaskini huu ni chanzo kikuu cha myumbo wa uchumi kimataifa na
matokeo yake ni umaskini na utupu wa maisha ya kiroho. Hali hii
inajionesha pale mwanadamu anapomn’goa Mwenyezi Mungu katika maisha na
vipaumbele vyake, kiasi hata cha kutema upendo na huruma yake. Hapa
mwanadamu anadhani kwamba, anaweza kujitegemea mwenyewe na wala haitaji
msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini ikumbukwe kwamba, ni Mungu peke
yake anayeweza kukomboa na kumwokoa mwanadamu.
Baba Mtakatifu anasema, Injili ni dawa inayoponya umaskini wa maisha
ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa kila Mkristo kuhakikisha kwamba,
anashiriki kutangaza Injili ya Kristo katika medani mbali mbali za
maisha, ili watu waonjeshe upendo na huruma ya Mungu; ili hatimaye,
waweze kushirikishwa maisha ya uzima wa milele. Waamini wawe ni
watangazaji amini wa Injili ya Furaha inayojikita katika huruma na
matumaini; mwanga na faraja kwa wote wanaotembea katika giza na uvuli wa
mauti. Ni mwaliko wa kumfuasa Kristo aliyethubutu kuwaendea maskini;
akaonesha sifa ya kuwa mchunga mwema kwa kumwendea Kondoo aliyekuwa
amepotea, ili kumwonjesha upendo wake. Kwa kushikamana na Yesu, waamini
wanaweza kuwa na ujasiri wa kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji
Mpya na maendeleo endelevu.
Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi hiki cha Kwaresima anawataka
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha ushuhuda wa pekee kwa
maskini wa hali, maadili na maisha ya kiroho wanaokutana nao kila siku
ya maisha yao, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya
Yesu Kristo. Kwaresima ni muda muafaka wa kujisadaka kwa ajili ya
kuwasaidia wengine, kwa kutambua kwamba, kwa njia hii pia tunafanya
toba.
Waamini wanaweza kuwatajirisha jirani zao na hivyo kushiriki katika
mchakato wa kuganga na kuponya umaskini unaomwandama binadamu. Ni
matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini wataweza kukitumia
kipindi hiki cha Kwaresima ili kupata neema na baraka zinazobubujika
kutoka kwa Kristo mwenyewe!
Ujumbe huu umehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
UJUMBE WA BABA MTAKATIFU FRANCISCO KWA KIPINDI CHA KWARESMA 2014
Reviewed by crispaseve
on
15:20
Rating:
Post a Comment