MWENYEKITI WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA MPYA AWAONGOZA WAJUMBE KATIKA VIKAO VYA KATIBA KUFANYA DHAMBI DODOMA.
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kupitia Taasisi za Elimu ya Juu (wanafunzi), Teddy Ladislaus, akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana. Kulia ni mwanafunzi wa Chuo cha Mipango Dodoma, Mfinanga Elisante. Picha na Emmanuel Herman
Dodoma. Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba anayedhaniwa kuwa na umri mdogo zaidi, Teddy Ladislaus (22), amesema kitendo cha Bunge hilo kuendelea na vikao vyake ni kutumia vibaya fedha za walipakodi na ni ‘dhambi’ ambayo wajumbe wanawatendea Watanzania likiongozwa na mwenyekiti wake Samwel Sitta.
Kwa sababu hiyo, mjumbe huyo kutoka Kundi la Wajumbe 201, ametaka liahirishwe ili kuokoa fedha hizo kwa kuwa kuna dalili kwamba Katiba bora haitapatikana kama Rais Jakaya Kikwete alivyoahidi alipoanzisha mchakato huo Desemba 31, 2011.
Binti huyo anayesubiri kutunikiwa Shahada ya Kwanza ya Teknolojia ya Habari na Biashara katika Chuo Kikuu cha Mzumbe baadaye mwaka huu aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba: “Tutakuwa tumetenda dhambi kubwa ikiwa tutawahadaa mamilioni ya Watanzania kwamba tutawaletea Katiba bora wanayoihitaji kama alivyosema Mheshimiwa Rais Kikwete wakati si kweli.
“Ni dhambi ya dhuluma ambayo tunapaswa, siyo tu kutubu, bali kutubu na kuacha. Nawaomba viongozi wakuu watambue kuwa Katiba bora itapatikana kwa maridhiano na siyo kwa ushindani na ubabe wa kisiasa”. Alisema lazima aisemee dhambi hiyo ambayo inaonekana kupumbaza fikra za walio wengi na kuweka masilahi ya watu wachache mbele, huku fedha za wananchi zikiendelea kutumika kwa kazi ambayo haina tija kwa sasa.
“Siwezi kuukana uzalendo wangu na kuogopa gharama za kusimamia ukweli. Dhamira yangu imeongoza fikra zangu kuamua kulisemea hili kwa niaba ya wale ninaowawakilisha,” alisema.
Alisema fedha nyingi zinazotumika sasa zingeelekezwa kutatua changamoto nyingine za kijamii, ikiwamo kuwapatia mikopo kundi kubwa la wanachuo walio na vigezo, kulipa malimbikizo ya madai ya watumishi hasa walimu na kugharimia miradi mingine ya maendeleo.
“Tumefumba masikio na hatutaki kusikia wasia na kilio cha wananchi na tumefumba macho hatutaki kuona uhalisia wa maisha ya Watanzania wenzetu, hii siyo sawa hata kidogo,” alisema.
Kauli yake iliungwa mkono na Rais Mtaafu wa Chuo cha Mipango, Mfinanga Elisante na Rais Mstaafu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Hemed Ngw’ali ambao aliambatana nao.
“Hakuna haja ya matumizi ya fedha nyingi kiasi hicho kwa jambo lisilo na tija kwa nchi wakati ni wiki saba sasa wanafunzi wako katika mazoezi ya vitendo na hawajui hatima yao na wanawaona watu wakiwa huku Dodoma wakitumia fedha,” alisema Ngw’ali.
Elisante alisema maridhiano kati ya pande mbili zinazokinzana ni muhimu sana katika kufanikisha mchakato wa Katiba.
Ladislaus alisema mgogoro uliopo baina ya makundi yenye masilahi ya kisiasa ni dhahiri umekwaza mchakato huo, hivyo busara zitumike kuuahirisha kwa sasa hadi hapo kutakapokuwa na maridhiano na mwafaka wa kitaifa kuhusu suala hilo.
“Mazunguzo siku zote ni ‘give and take’ yaani kulegeza msimamo katika baadhi ya hoja badala ya kila upande kushupaa kwa kile unachokiamini. Tukiwa na nia ya dhati ya kuzungumza, tukashauriana, tukaridhiana na kukubaliana jinsi ya kutekeleza yale tuliyoafikiana, basi Taifa litapata Katiba bora hivyo kuondoka katika mkwamo wa sasa.
“Kwa sauti moja, tunapenda tena kumsihi Mheshimiwa Rais kuahirisha mchakato huu ili kwanza kupisha maridhiano na pili kuokoa fedha zinazotumika kwa ajili ya kusukuma mbele mchakato huu”.
Alisema kuna kila dalili kwamba hivi sasa Bunge Maalumu linafanya kazi ilimradi lifike mwisho na ionekane kwamba kazi ya kupata Katiba Mpya imefanyika akisema anaamini hawako katika njia sahihi na wanawadhulumu Watanzania ambao wamewapa dhamana ya kuwawakilisha.
“Kwa kuwa Katiba ni moyo wa nchi, tusifanye kazi kwa kulipua ilimradi tuwapendeze wachache walioweka masilahi binafsi mbele. Tukifanya hivyo tutakuwa tunaliweka Taifa rehani na baadaye litaachwa liharibikie mikononi mwetu, sisi vijana.”
Alisema uchambuzi wa Rasimu unaoendelea ndani ya kamati za Bunge hilo unakabiliwa na changamoto ya muda kwani zinatakiwa kujadili sura na ibara nyingi katika muda mfupi kuliko walivyofanya katika awamu ya kwanza ya Bunge hilo. Alisema ikizingatiwa siku 16 walizopewa kwa ajili ya kujadili na kuchambua sura 15 zenye ibara 240, ambazo ni wastani wa Ibara 15 kwa siku, ni dhahiri kazi haitafanyika kwa weledi na kutoa Katiba bora... “Uchambuzi huu wa sasa hauwezi kutuletea Katiba bora iliyokusudiwa.”
Ikulu: JK hana mamlaka kuvunja Bunge
Wakati Ladislaus akitoa wito kwa Rais kulivunja Bunge hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu amesema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba haina kipengele kinachompa Rais uwezo wa kufanya hivyo na kusisitiza kuwa mchakato wa Katiba umeanzishwa kisheria na utamalizika kwa mujibu wa sheria hiyo.
Alisema ni ajabu kuona watu waliosema Rais alifanya makosa kutoa maoni yake wakati akifungua Bunge hilo, kuibuka na kumtaka Rais huyohuyo asitishe Bunge hilo.
“Bunge halitasitishwa na shughuli zake zitaendelea kama kawaida. Hakuna sheria inayomtaka Rais asitishe Bunge, haipo mahali popote,” alisema Rweyemamu.
Alipoulizwa iwapo Rais anaweza kutumia mamlaka aliyo nayo kusitisha Bunge hilo, Rweyemamu alisisitiza kuwa sheria ndiyo inayotakiwa kufuatwa. “Kila siku watu wanawazungumzia Ukawa, mbona wajumbe wanaoendelea na vikao vya Bunge hilo hamuwatazami? Ukawa ni kundi dogo zaidi ikilinganishwa na kundi lililopo bungeni,” alisema.
Wasira, Mnyika watofautiana
Mbali na Rweyemamu, wajumbe wawili wa Bunge la Katiba, Stephen Wasira na John Mnyika jana walitofautiana kwa hoja kuhusu mamlaka ya Rais kuvunja Bunge hilo.
Wakati Wasira akisema Rais hana mamlaka kisheria, Mnyika alisema kuna njia mbili ambazo Rais akiwa mkuu wa nchi anaweza kuzitumia kusaka maridhiano huku Bunge hilo likiwa haliendelei na vikao vyake.
Wasira ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, alisema katika kipindi cha ‘Tuongee Asubuhi cha Star TV kuwa, sheria haimpi uwezo Rais kulivunja Bunge na wanaodhani kwa kuwahamasisha wananchi waandamane kulivunja wanajidanganya.
Mnyika alisema kuna dhana mbili ambazo zinapotoshwa lakini zikitumika vizuri zinaweza kuuvusha mchakato huu kutoka katika matumaini hasi kwenda chanya.
“Rais kama mkuu wa nchi anaweza kabisa kutumia madaraka yake kwa masilahi ya wengi ama kulivunja au kuliahirisha Bunge kupisha maridhiano,” alisema Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema).
Alisema mbali na njia hiyo, inaweza kutumika njia aliyoitumia Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kuliahirisha Bunge kuanzia Agosti 5 hadi Septemba 2 mwaka huu kupitisha kanuni, pia anaweza kufanya hivyo kwa kipindi kirefu ili kupisha majadiliano.
“Rais Kikwete na Sitta kwa mamlaka waliyonayo wangeweza kuliahirisha kama walivyoliahirisha sasa, hadi Novemba au zaidi ya hapo ili kuwezesha majadiliano kuendelea.
“Lakini pia, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba siyo kwamba haimpi Rais mamlaka hayo, yeye ndiye aliyeisaini na yeye kama Mwenyekiti wa CCM aliliongoza Baraza la Mawaziri kuipitisha na kuileta bungeni sasa kwa nini asiwe na uwezo wa kulivunja au kuliahirisha?” alihoji.
Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba alipendekeza Rais Kikwete kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein wapunguze idadi ya siku ambazo Bunge litafanya vikao vyake kutoka 84 hadi chini ya hapo (hakufafanua) ili kubana matumizi.
Kanisa: Mchakato wa Katiba uendelee.
Kanisa la Baptisti Tanzania nalo limepingana na makundi ya wananchi yanayotaka mchakato wa Katiba usitishwe likisema uendelee kwa kuwa tayari mamilioni ya fedha za Watanzania yametumika.
Msimamo huo ulitolewa jana na Katibu Mkuu wa Makanisa ya Kibaptisti Tanzania, Mchungaji Ernest Sumisumi katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za Kanisa hilo Kinondoni B, Dar es Salaam.
Alisema kanisa halitaki mchakato wa Katiba usitishwe kwa sababu ya mgawanyiko wa wajumbe na kuusitisha ni kuwatia hasara wananchi.
Alisema kanisa linatoa wito kwa viongozi wa pande zote mbili kuendelea kufanya mazungumzo ili kuwe na maridhiano ya pamoja ambayo yatawafanya wajumbe wa Ukawa kurudi bungeni.MWANANCHI
MWENYEKITI WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA MPYA AWAONGOZA WAJUMBE KATIKA VIKAO VYA KATIBA KUFANYA DHAMBI DODOMA.
Reviewed by crispaseve
on
05:36
Rating:
Post a Comment