Taasisi ya watumishi housing kutumia bilioni 400 kujenga nyumba za watumishi wa serikali
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Watumishi Housing Company, Dkt. Fred
Msemwa akitoa mada kuhusu mkopo wa ujenzi wa nyumba bora za kisasa kwa
watumishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakati wa
warsha ya siku moja iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya
Habari Jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 14, 2014.
Baadhi
ya Watumishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
wakifuatia uwasilishaji wa mada kuhusu mkopo wa nyumba bora za watumishi
wa umma wakati wa warsha iliyotolewa na Taasisi ya Watumishi wa Housing
Company leo Alhamisi Jijini Dar es Salaam.PICHA NA BENJAMIN SAWE- MAELEZO.
TAASISI ya
Watumishi Housing Company imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 400 kwa ajili ya
ujenzi za watumishi wa Serikali katika mikoa 13 nchini.
Ujenzi wa nyumba
hizo unatarajia kuanza mwezi oktoba mwaka huu, ambapo katika awamu ya kwanza,
taasisi hiyo imepanga kujenga jumla ya nyumba 2500 katika kipindi cha mwaka wa
fedha 2014/15 na Mikoa itayonufaika na ujenzi wa nyumba hizo ni Mtwara,
Rukwa,Mbeya, Morogoro, Dodoma, Pwani, na Dar es Salaam.
Mikoa mingine ni
pamoja na Tanga, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Kigoma na Kilimanjaro, na jumla ya
nyumba 50,000 zinatarajiwa kujengwa na taasisi hiyo hadi kufikia mwaka 2019. Akizungumza
katika warsha ya siku moja kwa Watumishi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dkt. Fred Msemwa alisema mara
baada ya kukamilika nyumba zinatarajia kuuzwa kiasi cha Tsh. Milioni 19 hadi
Milioni 119.
Dkt. Msemwa
alisema mpaka sasa Ofisi imeanza utaratibu wa kuuza vipande vitavyowekezwa katika
ardhi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Pensheni wa
mashirika ya Umma (PPF), mfuko wa pensheni wa watumishi wa umma (PSPF), na mfuko
wa taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF),
Mifuko mingine
ni pamoja na mfuko wa pensheni wa watumishi wa Serikali za Mitaa ( LAPF), mfuko
wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF), pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa, ambapo
waombaji watapaswa kupitisha maombi yao kupitia kwa waajiri wao.
Aliongeza kuwa
tayari ofisi yake imekwishapata maelekezo kutoka katika Benki Kuu ya Tanzania
(BOT), ambapo moja ya masharti ni pamoja na makato ya riba yasiyozidi aslimia
10, na mtumishi atatakiwa kutumia kipindi cha miaka 5 hadi 25 ili kurejesha
mkopo katika taasisi hiyo.
Akifafanua zaidi
Dkt. Msemwa alisema Nyumba hizo zitakuwa ni za kisasa zaidi kwani maeneo yote
yaliyojengwa nyumba hizo yamepimwa na kutakuwa na miundombinu bora zaidi
ikiwemo barabara, maji na umeme, hivyo aliwataka watumishi wa umma kujitokeza kwa wingi ili
waweze kujipatia nyumba hizo.
Kwa mujibu wa Dkt. Msemwa mpaka sasa
wamepokea jumla ya maombi 500 kutoka kwa watumishi wa Serikali na ofisi yake
imeanza mchakato wa kupitia maombi hayo na kuangalia kama wamekamilisha vigezo
vya kimsingi ikiwemo masharti ya kuwa mwajiriwa katika sekta ya umma pamoja na
kuwa mwanachama wa mfumo wowote wa pansheni.
“Leo hii watumushi wengi wa Serikali
wameshindwa kununua nyumba kutoka katika taasisi mbalimbali, utakuta nyumba ya
Tsh. Milioni 30,000,000 mtumishi anatakiwa kukatwa asilimia 10 ya mshahara wake
ambayo ni Tsh. 3,000,000, hivyo wengi wao wamejikuta wakishindwa” alisema.
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
Dar es Salaam
14.08.2014
Taasisi ya watumishi housing kutumia bilioni 400 kujenga nyumba za watumishi wa serikali
Reviewed by crispaseve
on
00:11
Rating:
Post a Comment