Yote Uliyowahi Kutaka Kujua Kuhusu Mkito.com: Mahojiano Na Mwanzilishi Mwenza,Sune Mushendwa

Wengine
wakaamua kuachana na muziki [wengine muziki umewaacha wao] kutokana na
ukosefu wa soko la uhakika na kuona kadhaa ya kupanga foleni ukisubiri
“hela yako”.
Mabadiliko ya masoko ya kazi za wasanii duniani kutoka kwenye mifumo ya
ki-analojia kwenda kwenye dijitali na pia kutoka katika mifumo ya vitu
kama CD mpaka kwenda kwenye matumizi ya simu na vikabrasha vingine vya
mikononi, kulimaanisha kwamba soko la wasanii wa kitanzania [na Afrika
kwa upana wake] lilikuwa linazidi kufifia.
Hakuna
tena shabiki anayetaka kubeba furushi la CD. Inakuwaje?
Hapo ndipo baadhi ya vijana wakaona fursa kuthibitisha kwamba penye
tatizo ndipo pa kukimbilia.Fursa ni kama dhahabu au almasi.Huwezi
kuiokota kando ya bahari ikiwa imetupwa ufukweni na mawimbi ya bahari.
Wazo la fursa likazaa Mkito.Com mahali ambapo wasanii sasa wanapumua na
huku changamoto pekee ni kuwashawishi mashabiki kupakua kazi zao kutoka
Mkito.Com.
Kila
mara shabiki anapofanya hivyo, msanii ananufaika na kupata nguvu zaidi
ya kuingia tena studio kunogesha mambo. It’s a win win situation.
Sune Mushendwa [pichani juu] ni mwanzilishi-mwenza wa Mkito.Com.
Kujua mengi zaidi nilimtafuta na kupiga naye story kidogo. Ameelezea
mengi. Nakukaribisha usome mahojiano yangu naye ili ujue yote ambayo
umekuwa ukitaka kuyajua kuhusu Mkito.Com .Twende pamoja;
BC:
Sune karibu sana ndani ya BongoCelebrity. Hii ni mara yako ya kwanza
hapa na bila shaka wasomaji wangependa kupata japo kwa kifupi tu
historia yako. Ulizaliwa wapi,ukakulia wapi na kusomea wapi na mambo
kama hayo?
SM:
Asante sana kwa kunikaribisha. Mimi nimekulia Arusha na ndipo
niliposoma pia. Baada ya sekondari nilienda kusoma chuo kikuu nchini
Finland ambako mama yangu ndipo anapotokea.
BC:
Wajasiriamali wengi ambao nimewahi kufanya nao mahojiano huniambia
kwamba waliamua kufanya wanachokifanya baada ya kukosa au kubughudhiwa
na kitu fulani.Huwa kuna kisa au mkasa nyuma ya pazia.
Kwa upande wa Mkito kuna kisa au mkasa wowote? Ilikuwaje mpaka ukasema Aha…Mkito ikaanza? Na hili jina lilikuja namna gani?
SM: Baada ya kutoka masomoni nilianzisha studio ya
muziki Arusha.Lakini tatizo kubwa lililoonekana moja kwa moja ni kwamba
wasanii pamoja na studio zinapata tabu sana katika kusambaza na kuuza
kazi zao. Niliona tunahitajika njia ya kuweza kusambaza muziki kirahisi
na pia kuingiza kipato kwa msanii. Baada ya research na maandalizi ya
zaidi ya miaka 4 ndipo Mkito.com ilipozaliwa tarehe 30 April 2014.
BC: Mpaka sasa Mkito imefanikiwa kuwa na wasanii wangapi? Nini masharti ya msanii kujiunga au kuweka kazi zake katika Mkito?
SM: Kuna wasanii takriban 600 waliojiunga mpaka sasa na
wanaongezeka kila siku. Masharti ya kujiunga ni marahisi, uwe umerekodi
wimbo anghalau mmoja wenye ubora. Baada ya hapo msanii anaweza
kujitengenezea akaunti yake kupitia tovuti www.mkito.com
na kupakia[upload] nyimbo zake mwenyewe. Msanii baada ya hapo anaweza
kufuatilia mauzo yake mwenyewe kupitia akaunti yake aliyoitengeneza.
BC:
Bado nikiwa katika swali au maswali ya wasanii. Msanii akishaingia
katika mkataba au makubaliano na ninyi, bado anakuwa na haki na uhuru wa
kuendelea kusambaza kazi zake katika platforms zingine kama vile
iTunes,Spotify,Google Play nk?
SM: Tunaamini kuwa kazi ya msanii ni mali yake pekee
kwahivyo hatumzuii msanii aliyejiunga nasi kusambaza kazi zake kwa njia
yoyote nyingine aipendayo. Kama huduma yetu ni bora basi tunaimani
msanii mweyewe atachagua kutumia huduma zetu siyo mpaka tumfunge kupitia
mikataba.
BC:
Nilisoma mahali kwamba mlipoanzisha Mkito lengo lilikuwa kuwa na
watumiaji waliojiandikisha [registered users] milioni 1 katika mwaka wa
kwanza. Mpaka sasa mmefikia wapi katika lengo hilo?
SM: Nilishasoma hilo mimi pia lakini siyo ukweli kuwa
lengo ni kufikisha watumiaji milioni 1. Lengo ni kufikisha watumiaji
waliyojiandikisha laki 5 ndani ya mwaka moja. Tumekaribia nusu ya hiyo
idadi mpaka sasa na dalili zote ni kuwa tutafika na kuvuka hiyo idadi.
BC: Kuna baadhi ya wasanii ambao nimeongea nao kuhusu huduma kama hii
ya Mkito na nyinginezo wanasema kwamba huduma hizi kimsingi zinawapunja
au kuwadhulumu kwa sababu hamuendi nao bega kwa bega katika matayarisho
ya muziki [kwa maana ya gharama na karaha zote za maandalizi] bali nyie
mnasubiri wapike kisha muwasaidie tu kupakua huku nanyi mkijitengenezea
faida. Unawaambiaje wasanii kama hao na kuna tofauti gani kubwa kati ya
wasambazaji wale wa zamani na nyie hapo?
SM: Mkito.com ni kampuni ya usambazaji wa muziki na siyo studio ya kurekodi au kampuni ya management.
Kwa
maana hiyo sisi faida tunaingiza katika uuzaji wa muziki kupitia tovuti
yetu tu. Kama tungehusika na kurekodi na management ya wasanii basi
tungedai makato kwenye mauzo yote kama ring tones, CD, shows n.k. lakini
kama nilivyosema faida yetu ni katika uuzaji wa muziki tu.
Kuhusiana na tofauti ya Mkito.com na makampuni mengine; tangia mwanzo
tumehakikisha kuwa mauzo yote yanawekwa wazi ili msanii ajue muda wote
kuwa mauzo yake yakoje. Hili bado sijaona likifanyika na wengine ingawa
ni la muhimu sana. Inabidi kujiuliza madhumuni ya haya makampuni
kutokuweka mauzo wazi.

BC:
Kwa mtu ambaye hajui Mkito ni nini na angependa kufahamu zaidi na hata
kujiunga na huduma ya Mkito[nazungumzia mtu mtumiaji wa kawaida] ungempa
maelezo gani kwamba Mkito ni nini na nini ategemee pindi atakapoingia
Mkito.com?
SM:
Mkito.com ni huduma ya kwanza nchini ya kusambaza muziki kidigitali
ambapo mtu anaweza kupakua nyimbo kwa sh 250 tu kupita simu yake au
computer. Pia nyimbo zote zinapatikana bure lakini zinaambatanishwa na
matangazo mafupi ya kibiashara. Haya matangazo katika nyimbo za bure
ndiyo yanawalipa wasanii. Ni muhimu kujua kwa Watanzania wote kuwa ni
jukumu letu kulinda muziki wetu na unavyopakua nyimbo kupitia Mkito.com
unakuwa unauhakikia kuwa msanii analipwa kwa kazi yake na wewe pia
unasaidia kuuendeleza muziki wa Kitanzania.
BC: Bila shaka kwenye biashara kama ya Mkito ambayo kwa ukaribu sana
inahusiana na tekinolojia za mitandaoni,matatizo hujitokeza.Kuna mtu
kushindwa kupakua[download] wimbo au nyimbo na kuna kero zingine
nyingi.Mkito mnashughulikiaje matatizo kama hayo? Na kimsingi ni
changamoto gani ambazo mnakabiliana nazo kila siku au mara kwa mara?
SM: Kuna maelfu ya aina tofauti za simu na computer
ambazo kila siku zinatumika kupakua nyimbo Mkito.com. Sasa ni vigumu
kuhakikisha kuwa tovuti itafanya kazi na kila aina ya simu lakini kwa
kiasi kikubwa sana tumefanikiwa kutatua matatizo yanapojitokeza.
Pia
tunayo huduma kwa wateja ili mtu akipata shida anaweza kutuandika barua
pepe au kupiga simu na tunamsaidia kutatua tatizo lake haraka.
BC: Kwa upande wa muziki, wasanii,wasimamizi [managers] wao nk
nikikupa nafasi hii kuongea nao moja kwa moja ungewaambia nini au
ungewapa ushauri gani kuhusiana na suala zima la muziki nk?
SM: Muziki ni biashara, wote tunafahamu hilo. Kwahiyo
ninawakaribisha wasanii wote kuja kujiunga Mkito.com tuwasaidie
kutangaza, kusambaza na kuuza muziki wao. Nafahamu kuwa wengi wanakuwa
na wasiwasi kuwa wataibiwa – hili siyo kweli kwa upande wa Mkito.com,
labda waliotutangulia. Kama nilivyokwisha sema kila kitu kinawekwa wazi
na kama wewe ni msanii mwenye kazi nzuri basi kuwa na imani kuwa unaweza
kujipatia kipato kizuri kutokana na mauzo ya muziki wako kupitia
Mkito.com
BC: Shukrani sana kwa muda wako Sune. Nakutakia kila la kheri katika kazi zako
Asante sana. Lakini na mimi nikuulize wewe swali moja. Je,
umeshapakua nyimbo ngapi mpaka sasa kupitia Mkito.com ili kuwapa support
wasanii wa Tanzania? J
BC:
Mpaka leo,nimeshapakua nyingi.Sikumbuki idadi kamili. Lakini mchango
wangu zaidi ni kuwajulisha watumiaji wengine [wasomaji wangu kwa mfano]
juu ya kazi mpya za wasanii na wapi pa kuzipata. Asante kwa swali zuri
Sune.
Yote Uliyowahi Kutaka Kujua Kuhusu Mkito.com: Mahojiano Na Mwanzilishi Mwenza,Sune Mushendwa
Reviewed by crispaseve
on
05:28
Rating:
Post a Comment