Header AD

Bilioni 43.89 zatumika kusambaza umeme Dodoma


Na Greyson Mwase, Dodoma

Meneja wa Shirika la Umeme Nchini  (Tanesco) mkoa wa Dodoma, Zakayo Temu amesema kuwa Serikali imetenga  jumla ya shilingi  bilioni 43.89 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya  umeme katika mkoa wa Dodoma kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.

Temu aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu  ya Bunge ya Nishati na Madini  iliyopo  mkoani  Dodoma kwa ajili ya kukagua miradi  ya umeme  ili kujionea utekelezwaji wake pamoja na kuzungumza na wawakilishi wa wananchi. Mbali na mkoa wa Dodoma, kamati hiyo  inatarajia kufanya ziara ya kukagua miradi ya umeme katika mikoa  ya Singida, Arusha na Kilimanjaro pamoja na   kuzungumza na wadau wa madini katika mkoa wa Manyara.

Akitoa  taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme katika mkoa wa Dodoma chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya  Pili, Temu alisema kuwa mradi  kabambe wa kusambaza umeme  vijijini  awamu ya pili  unahusisha wilaya  zote za mkoa wa Dodoma, wilaya za Chamwino, Kongwa zikiwa mojawapo.

Akielezea kazi ya usambazaji wa umeme katika wilaya  ya Chamwino  Temu alisema kazi ya kupeleka umeme  itahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovolti 33 urefu wa kilomita 171.5 na  njia ya msongo  wa kilovoti 0.4 urefu wa kilomita 95.

Alisema  ujenzi utahusisha pia ufungaji wa transfoma 22 za ukubwa mbalimbali  pamoja na kuunganisha wateja wapatao 1,195 kwa gharama inayokadiriwa kuwa shilingi za kitanzania bilioni 8.67.

Aliongeza kuwa katika wilaya ya  Chamwino  hadi sasa ujenzi wa miundombinu  ya umeme  umefikia asilimia 52 na wateja 105 kati ya 1,195 wamekwisha unganishwa na huduma ya  umeme na kusisitiza kuwa mradi huu  unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Bilioni 43.89 zatumika kusambaza umeme Dodoma Bilioni 43.89 zatumika kusambaza umeme Dodoma Reviewed by crispaseve on 07:34 Rating: 5

No comments

Post AD