Header AD

WAZIRI MKUU: WANAOHITIMU JKT WAPEWE NYENZO


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itapaswa itafute njia za kuwawezesha vijana wanaohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili waweze kutekeleza kwa vitendo mafunzo wanayoyapata na waweze kujiajiri.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Agosti 4, 2015), wakati akizungumza na wananchi na washiriki wa maonyesho waliohudhuria uzinduzi wa maadhimisho ya 22 ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) ambayo mwaka huu yanafanyika kitaifa kwenye viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi.

Akizingumza mara baada ya kutembelea mabanda zaidi ya 10, Waziri Mkuu Pinda alisema kuna haja ya kuwatafutia fursa za kujiajiri vijana wanaohitimu mafunzo hayo ili wasibweteke.

“JKT ndiyo inayofundisha vijana wetu katika fani mbalimbali… tuwatafutie fursa za kujiajiri mara wanapohitimu mafunzo ili wasitoke huko na kubweteka eti hawana kazi,” alisema.

Alisema kuna haja ya kuweka mfumo maalum kupitia Wizara ya Ulinzi na JKT ambao utawatambua vijana wachache wanaotoka katika mikoa mbalimbali hapa nchini ambao hupatiwa mafunzo ya ujasiriamali kama vile kutengeneza batiki, sabuni, samani, mabanda ya kuku, kufuga mbuzi, ng’ombe, samaki na kuku na kilimo cha bustani za mboga za majani.

“Mtu akishapatiwa ujuzi huu akaachwa arudi kijijini hawezi kufanya chochote… lazima atakaa kijiweni na kudai hana ajira. Tutafute mfumo wa kuwasaidia ili wapate mtaji wa kuanzia, wajiajiri kupitia kile walichofundishwa na baadaye iwe ni mfumo wa kuzungusha ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika,” alisema huku akishangiliwa.

Waziri Mkuu pia alitumia fursa hiyo kukipongeza kituo cha utafiiti cha Naliendele kwa kuibua aina mpya 16 za mbegu za korosho ambazo zimesaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo hadi kufikia tani 200,000 kwa mwaka ikilinganishwa na tani 16,000 miaka michache iliyopita.

“Ninawasihi ndugu zangu wa Lindi na Mtwara tusikilize wataalamu wanatuambia nini kwa sababu utafiti ndiyo mkombozi mkubwa wa kilimo cha Tanzania. Tufuate maelekezo wanayotuelekeza na hii si kwa korosho tu, iwe ni karanga, ufuta au alizeti kwani ni mazao yanayokubali vizuri katika ukanda huu wa Kusini,” alisema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo imekuwa ikitekeleza mipango ya Kitaifa ikiwemo shughuli za kuendeleza kilimo kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) ambayo imefikia ukomo. “Hivi sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Awamu ya Pili ya Programu hiyo yaani ASDP II. Programu hiyo  imekuwa ikitekeleza Kilimo Kwanza na miradi mbalimbali ya kilimo na imekuwa muhimili muhimu katika kuendeleza kilimo chetu nchini,” alisema.

Waziri Mkuu Pinda amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Manispaa na Halmashauri za Wilaya wabadili mitazamo yao kama kweli wana nia ya kuwasaidia wananchi.

“Viongozi hatuna budi tuwe karibu na wananchi na hasa maafisa ugani. Hawa wanapaswa kujituma ili waweze kweli kubadili wananchi kwani asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima, wafugaji na wavuvi,” alisisitiza.

Maadhimisho hayo ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) yanatarajiwa kufungwa Jumamosi, Agosti 8, mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 5, 2015.
WAZIRI MKUU: WANAOHITIMU JKT WAPEWE NYENZO WAZIRI MKUU: WANAOHITIMU JKT WAPEWE NYENZO Reviewed by crispaseve on 03:21 Rating: 5

No comments

Post AD