BALOZI SEIF AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA, PIA AKUTANA NA MABALOZI WA TANZANIA KATIKA NCHI ZA MISRI NA ZAMBIA
Balozi wa China Nchini Tanzania Bibi Wang Ke alisema kukamilika kwa utanuzi wa ujenzi wa Eneo la Maegesho ya Ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar utatoa fursa ya kuongezeka kwa huduma za usafiri wa anga baina ya Zanzibar na Mataifa mengine Duniani.
Alisema matayarisho ya ujenzi huo katika hatua za awali za Awamu
ya Pili aliyoyashuhudia baada ya kushuka kwenye Uwanja huo wa Ndege wa
Zanzibar yamempa faraja yeye pamoja na Uongozi mzima wa Benki ya
Kimataifa ya Exim ya Nchini China iliyoridhia kugharamia Mkopo wa ujenzi
huo.
Balozi Wang Ke alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika ofisini kwake
Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika
wadhifa huo wa Kidiplomasia.
Alisema Zanzibar inaweza kurejesha Heshima yake ya kuwa Kituo cha
Kibiashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki chenye uwezo wa kutoa
huduma za Kibiashara kupitia mfumo wa kisasa wa Mawasiliano kupitia
usafiri wa anga badala ya ule uliozoeleka wa Baharini.
Alieleza kwamba zaidi ya Watalii 70,000 kutoka Nchini Jamuhuri ya
Watu wa China wanaweza kuitembelea Zanzibar kila Mwaka kupitia usafiri
wa anga na hata ule wa Baharini iwapo yataandaliwa mazingira mazuri
katika Sekta ya Utalii baada ya kuongezeka kwa huduma za Mawasiliano ya
usafiri.
Bibi Wang Ke aliyeanza majukumu yake Nchini Tanzania Mwezi Mmoja sasa
aliahidi kwamba Nchi yake iliyopiga hatua kubwa Kiuchumi ndani ya
kipindi cha Miaka 30 itaendelea kuiunga mkiono Zanzibar na Tanzania kwa
ujumla katika kuona maendeleo ya Kiuchumi yanakua na kushirikisha
wananchi wote siku hadi siku.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alieleza faraja yake katika kuona Viongozi wote waliiopo hivi
sasa kati ya China na Tanzania bado wanaheshimu ushirikiano wa Mataifa
hayo mawili ulioasisiwa na waanzilishi wake Marehemu Mwalimu Julius K.
Nyerere na Hayati Mao Tse Tung.
Balozi Seif alisema mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na China
kupitia Makampuni na Mashirikia yake mbali mbali umeiwezesha Tanzania
kukuwa Kiuchumi na kustawisha Jamii mambo yanayokwenda sambamba na
kupungua kwa kasi ya ukali wa Maisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza na kumuomba Balozi
huyo wa China Nchini Tanzania kwamba Zanzibar bado inaendelea kuhitaji
Wawekezaji pamoja na Watalii kutoka Nchini China katika azma yake ya
kuimarisha uchumi hasa kwenye Sekta ya Utalii.
Balozi Seif ameishukuru Serikali ya China kwa misaada yake mikubwa
inayotowa na kumuhakikishia kwamba uhusiano wa Kihitoria uliopo wa
Mataifa hayo rafiki utaendelea kudumu kila Mwaka.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alikutana kwa mazungumzo na Mabalozi Wapya Wawili wa Tanzania
Nchini Misri na Zambia walioteuliwa hivi karibu na Rais wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli.
Mabalozi hao ni Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor anayeiwakilisha
Tanzania Nchini Misri na Balozi Abdulrahman Kaniki anayekwenda Nchi
jirani ya Kusini mwa Tanzania ya Zambia.
Katika mazungumzo yao Balozi Seif aliwakumbusha Mabalozi hao
kuzingatia zaidi suala ya Doplomasia ya Kiuchumi ambalo kwa sasa
limechukuwa nafasi ya pekee tofauti na lile ya Kisiasa lililozoeleka
katika mabadiliko ya Kiuchumi yaliyopo Ulimwenguni.
Alisema matunda makubwa ya uwakilishi wa Mabalozi hao yataonekana
katika kasi ya ongezeko la Miradi ya Uwekezaji kutoka katika Mataifa
wanayokwenda kufanya kazi.
Mapema Balozi wa Tanzania Nchini Misri Meja Jenerali Issa Suleiman
Nassor kwa niaba ya Mwenzake Balozi Abdulrahman Kaniki anayekwenda
Nchini Zambia alisema wanaahidi kuitanga Tanzania katika Mataifa hayo
rafiki yenye Uhusiano wa muda mrefu.
Meja Jenerali Nassor aliziomba Taasisi zinazozimamia Sekta ya Utalii
Nchini kuwa wazi kwa masuala yanayohitajika katika kuimarisha Sekta hiyo
kupitia Wawekezaji na Mikataba ya uanzishwaji wa Miradi ya Hoteli.
Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifanya mazungumzo na
Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
ulioongozwa na Naibu Waziri wake Dr. Suzan Kolimba.
Katika mazungumzo hayo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Dr. Suzan alisema wako Zanzibar kufuatilia Rasimu ya
Matayarisho ya Ripoti ya Utawala Bora Barani Afrika kwa upande wa
Zanzibar inayotakiwa kutayarishwa na Wizara zilizo chini ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Dr. Suzan alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Ripoti
ya Utawala Bora Barani Afrika itakuwa ndio Mpango Kazi kwa Maraisi wa
Mataifa ya Bara la Afrika watakayoiwakilisha katika Kikao cha Umoja wa
Afrika {AU} kinachotarajiwa kufanyika Mwezi Febuari mwaka 2018.
Alisema hatua ya awali ya matayarisho ya Ripoti hiyo imeonyesha
mafanikio kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mfano bora wa
Rasimu yake ya Utawala Bora kiasi cha Wataalamu wa masuala ya Kisiasa wa
Bara la Afrika kushauri iwe kigezo cha kuigwa na Mataifa mengine Barani
Afrika.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
28/11/2017.
Balozi
wa China Nchini Tanzania Bibi Wang Ke akisalimiana na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake Vuga
Mjini Zanzibar kujitambulisha Rasmi.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na
Mabalozi wa China Nchini Tanzania na yule aliyepo Zanzibar.
Wa kwanza kutoka Kushoto ni Balozi wa China Nchini Tanzania Bibi
Wang Ken na wa kwanza kutoka Kulia ni Balozi Mdogo wa China aliyepo
Zanzibar Bwana Xie Xiaolon.
Balozi
Seif akiagana na Ujumbe wa Kidiplomasia wa Ubalozi wa China Nchini
Tanzania na Ule wa Zanzibar mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiagana na Balozi wa Tanzania
Nchini Misri Meja Jegerali Issa Suleiman Nassor aliyekaa upande wa Kulia
yake na Balozi Abdulrahman Kaniki aliyekaa upande wa Kushoto
walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Dr. John Pombe Magufuli kushika nyadhifa hizo.
Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Suzan
Kolimba Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi akiwa Zanzibar na Ujumbe wake kufuatilia rasimu ya
Utawala Bora Afrika kwa Wizara za SMZ.
Balozi
Seif akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhan Muombwa Ofisini kwake
Vuga Mjini Zanzibar. Kati kati yao ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Suzan Kolimba.
BALOZI SEIF AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA, PIA AKUTANA NA MABALOZI WA TANZANIA KATIKA NCHI ZA MISRI NA ZAMBIA
Reviewed by crispaseve
on
14:55
Rating:
Post a Comment