Header AD

OLE WENU WEZI WA MAJI’-NAIBU WAZIRI AWESO

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ametoa onyo kali kwa wezi wa maji na wahujumu wa miundombinu ya maji na kuwataka waache tabia hiyo mara moja kwa kuwa Serikali imechoka kuingia gharama kubwa za utekelezaji wa miradi ya maji na kuhujumiwa.
Hayo yamesemwa wakati alipotembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) wakati akizungumza na Bodi, menejimenti na watumishi wa mamlaka hiyo inayotoa huduma ya maji kwa wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Aweso amesema wizara itaanzisha kampeni kabambe nchi nzima ya kubaini mtandao mzima na wale wote wanaoihujumu Serikali kwa wizi wa maji na miundombinu yake na kuziagiza mamlaka zote nchini kuweka mikakati mizuri ya kudhibiti tabia hiyo.
Amesema miradi ya maji imegharimu fedha nyingi sana ili kuwanufaisha wananchi wote kwa kufuata taratibu za kupata huduma hiyo kihalali na si kinyume na taratibu, akisisitiza kuwa ni haki ya mwananchi kupata maji lakini pia ana wajibu wa kuitunza miundombinu ya maji ili itoe huduma ya uhakika na endelevu.
‘‘Ninatangaza vita na wezi wa maji na wahujumu wa miundombinu ya maji, ole wenu wenye tabia hiyo maana tumechoka kwa kuwa inaturudisha sana nyuma kimaendeleo na nitalivalia njuga suala hili mpaka likome’’, amesisitiza Aweso.
Aidha, Naibu Waziri Aweso ametembelea mradi wa Hoza Salala uliopo Kijiji cha Kibati, wilayani Mvomero, mradi uliokuwa umegubikwa na tuhuma za ufisadi ambapo ameivunja Bodi ya Maji ya mradi huo na kuagiza iundwe mpya baada ya kugundua matumizi mabaya ya fedha kwa wajumbe wa kamati ya bodi.
 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akizungumza na Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA).
 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA, Mhandisi Nicholaus Angumbwike kwenye mtambo mpya wa kusafisha na kutibu maji wa Mambogo, Morogoro.
 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akiongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA, Mhandisi Nicholaus Angumbwike alipotembelea Bwawa la Mindu, Morogoro.
 Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso na Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Sadiq Morad wakiwa kwenye eneo la mradi wa Hoza Salala, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kibati, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.
OLE WENU WEZI WA MAJI’-NAIBU WAZIRI AWESO OLE WENU WEZI WA MAJI’-NAIBU WAZIRI AWESO Reviewed by crispaseve on 05:31 Rating: 5

No comments

Post AD