TUTAELIMISHA UJINGA NA MARADHI-MDEE
Na Mwandishi Wetu, Tanga
MFUKO
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema unaelekeza nguvu zaidi katika
kuelimisha umma kujikinga na maradhi, hususan yasiyoambukiza ili
kupunguza maradhi hayo kwa wanachama na wananchi kwa ujumla lakini pia
gharama za matibabu ambazo Mfuko unalipa kwa watoa huduma wanaotibu
wanachama wake.
Akizungumza
katika mkutano wa waandaji wa vipindi vya elimu kwa umma kutoka katika
Wizara na Taasisi mbalimbali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Hamis Mdee
aliyataja maradhi hayo kuwa ni pamoja na saratani, kisukari, shinikizo
la damu na uzito uliokithiri ambayo yamekuwa yakiongezeka sana na
kusababisha vifo miongoni mwa jamii.
“Magonjwa
haya yanaongezeka kila kukicha na gharama za matibabu yake ni kubwa
sana hivyo ni lazima sasa tuweke nguvu kubwa ya elimu inayohusu
kujikinga na maradhi haya nah ii itawasaidia sana wananchi kujua namna
ya kuepukana nayo,” alisema Bw. Mdee.
Aidha
Bw. Mdee amesisitiza kuwa NHIF itaendelea kushirikiana na Shirika la
Utangazaji Tanzania (TBC) katika mafunzo ambayo yamekuwa yakiandaliwa na
shirika hilo kwa waandaji wa vipindi ili yawe bora zaidi na manufaa kwa
taasisi wanazofanyika kazi na Serikali kwa ujumla.
Kwa
upande wa Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Tanga Bi. Monica Kalani
ambaye alifunga rasmi mafunzo hayo ya siku 10 alisisitiza umuhimu kwa
watayarishaji wa vipindi vya elimu kwa kutumia lugha fasaha katika
kuwasilisha mada kwa wasikilizaji na watazamaji wa vipindi vyao.
Alisema
watazamaji na wasikilizaji wa vipindi vya elimu kwa umma kupitia TBC 1
na TBC Taifa wanaimani kubwa na vyombo hivyo vya habari, kwa hiyo ni
wajibu wa watayarishaji wa vipindi vinavyorushwa kupitia vyombo hivyo
kutimiza matarajio ya wasikilizaji na watazamaji wao.
“Nyie
ni kundi muhimu sana katika maeneo yenu ya kazi hivyo mafunzo haya
kayatumieni vizuri ili yaoneshe matunda, wananchi wanahitaji sana elimu
mbalimbali kupitia vipindi vya radio na televisheni,” alisema.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Vipindi vya Redio wa Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC), Bi. Suzan Mungi, ameipongeza NHIF kwa kuwa Mwenyekiti wa
Mkutano huo ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa watayarishaji wa
vipindi vya elimu kwa umma.
“Tunaishukuru
sana NHIF kwani mmewezesha kwa kiwango kikubwa kufanikiwa kwa mkutano
huu na kwa ushirikiano mkubwa mlioutoa na kwa upande wetu kama TBC
tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu ili elimu ama kazi mnazozifanya
ziweze kutambulika kwa jamii,” alisema.
Mafunzo
hayo ya siku kumi yalihitimishwa rasmi jana ambapo washiriki wa mafunzo
hayo walitoka katika Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali nchini.
TUTAELIMISHA UJINGA NA MARADHI-MDEE
Reviewed by crispaseve
on
23:36
Rating:

Post a Comment