Viongozi watakiwa kutomlilia Mandela
……………………………………………………………………………..
Dar
es Salaam. Wasomi na watu mbalimbali wamesema katika kumwenzi Rais wa
Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela ni kutekeleza
yote aliyofanya kwa vitendo siyo kuomboleza kwa kulia.
Pia, walisema viongozi wa Bara
la Afrika wanatakiwa kutambua kuwa uongozi ni dhamana ya wananchi na
hawana budi kuepuka kutumia madaraka kujineemesha wao na familia zao.
Hayo yalisemwa jana wakati
kumbukumbu ya Mandela, iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo wasomi, wanasiasa na
mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini.
Kada wa CCM, Kingunge Ngombale–Mwiru alisema wanatakiwa kumuenzi Mandela kwa kufanya kwa vitendo mema aliyoyaacha,.
Kingunge alisema viongozi hawatakiwi kuhuzunika na kulia, kwani aliyofanya Mandela yanatosha kusherehekea siyo kuhuzunika.
Alisema baada ya kifo cha
Mwalimu Julius Nyerere kila mtu alihuzunika na kuongea mambo mengi,
lakini hakuna aliyetekeleza kwa vitendo aliyofanya.
“Ukiangalia viongozi wa zamani
na sasa wana tofauti kubwa. Viongozi wetu wa sasa wakipata madaraka
wanajifikiria wao kwanza badala ya wananchi,” alisema.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu,
Fredrick Sumaye alisema tatizo lililopo bara la Afrika, ni suala la
Uongozi na Utawala Bora vitu ambavyo vikifuatwa na kuzingatiwa vitasadia
maendeleo.
“Ukishakuwa na uongozi na
utawala bora, yale mambo ya kienyeji hayatakuwapo hivyo kila mmoja
anatakiwa kuiga aliyofanya Mandela na Nyerere, tutaibadili Afrika,”
alisema Sumaye.
Balozi
wa Palestina nchini, Dk Nasri Abu Jaish alisema kifo cha Mandela siyo
pigo kwa wananchi wa Afrika Kusini na Afrika pekee, bali dunia nzima
kwa sababu ni mwalimu wa dunia. “Alikuwa mwalimu kwa viongozi,
hakuwabagua watu, aliwaunganisha na kusaidia nchi zingine,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
Viongozi watakiwa kutomlilia Mandela
Reviewed by crispaseve
on
00:36
Rating:

Post a Comment