Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda Apongeza Uhusiona Uliopo Kati Japan na Tanzania,Ahaidi Kuimarisha Uhusiano wa Kibunge
Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda akimshukuru mwenyeji wake Spika wa Bunge la Japan Mhe. Takahiro Yokomichi na Ujumbe wake wa Wabunge wanaounda kamati inayoshughulikia Maswala ya Afrika kwa mwaliko waliompatia yeye na Ujumbe wa wabunge Kutoka Bunge la Tanzania kuja Japan kubadilishana uzoefu katika maswala ya Kibunge pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya mabunge haya mawili. Kulia kwa Mhe. Makinda ni Mhe. Godfrey Zambi na Mhe. James Lembeli walioambatana Na Mhe. Spika katika Ziara hiyo. Picha na Owen Mwandumbya
--
Na Mwandishi wetu, Tokyo Japan
Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda amesema, Tanzania inajivunia uhusiano mzuri kati yake na Japan. Akizungumza katika majumuisho ya ziara yake nchini Japan, Mhe. Makinda amesema, Bunge la Tanzania linaishukuru Serikali ya Japan na Bunge lake kwa kumwalika yeye na Ujumbe wa Wabunge kutoka Tanzania kuja kujifunza maswala Mabalimbali ya Kibunge ikiwa ni pamoja na kukuza demokrasia ya kibunge baina ya nchi hizi Mbili.
Amesema, Pamoja na Japan kupitia katika hali ngumu ya kulipuliwa kwa miji yake miwili ya Hiroshima na Nagasaki wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia, Matetemeko ya mara kwa mara na mafuriko ya Tsunami, lakaini bado uchumi wake haujayumba kiasi kwamba sasa waJapan wameweza kusima imara kuijenga nchi yao.
Mhe. Makinda amesema Demokrasia safi na Siasa imara za Japan ni mfano tosha na fundisho kwa Tanzania ambapo hivi sasa katika kuimarisha uhusiano huu wa Kibunge, mabunge haya mawili yatabadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi wa Bunge la Tanzania.
“ Nchini yenu mmekomaa sana katika Demokrasia, ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa shughuli za Kibunge, sisi kama watanzania tuna mengi sana tungependa kujifunza kutoka kwenu, leo mmenialika na ujumbe wangu kutembelea Bunge lenu, lakini napenda kusema huu uwe ndio mwanzo wa kuimarisha uhusiano wetu, ikiwezekana hata kamati zetu za Bunge zipate fursa ya kujifunza kutoka kwenu. Ziara za namna hii zitatusaidia kupanua uelewa wetu katika maswala ya Kibunge“ alisema Mhe. Makinda.
Katika kuhakikisha kuwa Bunge la Tanzania linaimarisha uhusiano wake na Bunge la Japan, Spika Makinda ametoa Mwaliko maalum kwa Spika wa Bunge la Japan Mhe. Takahiro Yokomichi kuja kutembelea Tanzania ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na wabunge wengine kutoka Bunge la Tanzania.
Mhe. Makinda amesema, Bunge la Tanzania linayo kamati ya Bunge inayoshughulikia maswala ya mambo ya Nje na uhusiano wa Kimataifa, hivyo ni fursa pekee ya kamati hii na wenzao kutoka Bunge la japan kushrikiana kwa karibu kuhakikisha ushirikano huu unakuwa imara na endelevu.
Akimshukuru Mhe. Makinda kwa kukubali mwaliko wake, Spika wa Bunge la Japan Mhe. Takahiro Yokomichi, amesema nchi yake iliichagua Tanzania miongoni mwa nchi za Afrika hususani Africa Mashariki kutembelea Bunge la Japan kwa kuwa ni nchi yenye demokrasia safi na siasa zake zinaimarika kila kukich na kuifanya Japan kuvutiwa na maendeleo hayo katika Bunge la Tanzania.
Mhe. Yokomichi amesema huu ni mwanzo wa ushirikiano muhimu baina ya Mabunge haya mawili ambapo Bunge la Japan pamoja na kuwa na kamati maalum inayoshughulikia maswala ya Afrika, bado kuna haja kwa kamati hiyo kufanya kazi kwa ukaribu na Bunge la Tanzania kwa lengo la kuangalia maeneo muhimu ambayo Japan itaisaidia Tanzania.
Hata hivyo Mhe. Yokomichi ameaidi kuishawishi Serikali yake ya Japan ili iendelee kutenga fungu kubwa zaidi kwa lengo la kusaidia sekta mbalimbali za maendeleo nchini Tanzania. Tarari Japan ni mchangiaji Mkubwa katika sekta mbalimbali za maendelo kwa kiasi kikubwa.
Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda na Ujumbe wa wabunge 5 kutoka Bunge la Tanzania upo Japan kwa mwaliko maalum na Bunge la Japan kujadili na kuimarisha ushirikiano baina ya Mabunge haya mawili, ambapo kabla ya kuonana na Mwenyeji wake, Ujumbe huo wa Tanzania ulipata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali ya utalii nchi Japan ikiwa ni pamoja na eneo la Mji wa Natori lililokumbwa na mafuriko yaliotokea machi mwaka jana na Mji wa Hiroshima uliosambaratishwa na Bomu la Atomic wakati wa vita kuu ya dunia mwaka 1945. Spika na Ujumbe wake wanatarajia kurudi nchini jumanne wiki hii.
Reviewed by crispaseve
on
08:14
Rating:
Post a Comment