Header AD

ZITTO KABWE:NISIHUSISHWE NA MATAMSHI NA MAKANUSHO WA WABUNGE WALIOKUWA KIGOMA

 
Mbunge wa kigoma kaskazini, Naibu katibu Mkuu (CHADEMA) Zitto Kabwe.
Katika gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Julai 2012, kulikuwa na habari yenye kusomeka 'Wabunge wamsafishia Zitto njia ya Urais 2015'. Habari hii imeleta mjadala mara baada ya kutoka na kusomwa. Mjadala umekuzwa zaidi baada ya Wabunge ndugu Halima Mdee na ndugu Joshua Nassari kukanusha maneno waliyonukuliwa kusema. Napenda kusema masuala yafuatayo.
Moja, Waheshimiwa Wabunge Halima Mdee, Joshua Nassari, Kangi Lugola, Esther Bulaya, Deo Filikunjombe, Raya Ibrahim, Amina Mwidau na David Kafulila walihudhuria tamasha la vijana wa Kigoma All Stars kwa kualikwa na Mratibu wa kundi hilo Mwasiti Almasi.
Wabunge wengine walialikwa lakini hawakutokea wakiwemo Joseph Mbilinyi, David Silinde, Amos Makala, Vicky Kamata na Peter Serukamba. Wabunge hawa hawakualikwa na mimi na wala sikufanya mazungumzo nao yeyote ya awali au kuwaambia au kukubaliana nini cha kuzungumza au hapana. Tamasha lilikuwa la muziki na halikuhusika kabisa na siasa.

Waheshimiwa wote walipewa nafasi ya kusalimia na wote walizungumza. Wabunge waliozungumza kwa muda mrefu kidogo ni ndugu Halima Mdee, Joshua Nassari, Deo Filikunjombe na Kangi Lugola.

Hotuba za Wabunge wote zilirekodiwa kwenye video neno kwa neno na Video hizo zitawekwa wazi kwenye blogu yangu kama sehemu ya documentary ya tamasha lile la kihistoria.

Pili, sikuhusika kwa namna yeyote ile na kuandikwa kwa habari hii iliyozusha mjadala. Wala sikujua kama habari hii ingeandikwa maana katika ziara ile sikuita mwandishi hata mmoja maana nilitaka liwe tukio la Kigoma tu.

Kama mwandishi kaandika ambayo wabunge hawa hawakuyasema basi itaonekana kwenye videos hizo. Wabunge wenyewe wanajua kwenye nafsi zao nini walisema Kigoma na kipi kiliwasukuma kusema walioyasema Kigoma. Nisingependa kuhusishwa kwa njia yeyote ile na matamshi yao, habari iliyowanukuu na hata makanusho yao. Maana mwisho wa siku ukweli ndio utasimama.

Suala la Urais lisitupotezee muda kwani kuna mambo mengi sana ya kujadili kuhusu nchi yetu. Taharuki ambazo watu wanazipata masuala ya urais yanapotajwa zinashangaza sana.

Chama changu bado hakijatangaza rasmi mchakato wa kupata mgombea Urais. Hivi sasa chama hakina mgombea Urais mpaka hapo mchakato utakapotangazwa ambapo wanachama wataruhusiwa kuomba kupeperusha bendera ya chama. Mwanachama wa chama chetu atakaye kubalika na jamii na wajumbe wa mkutano wa uteuzi ndiye atakuwa mgombea wetu. Kwa sasa hayupo na hivyo tusipoteze muda kujadili jambo hili.

Mzee Thabiti Kombo alituachia usia tunapokuwa tunazungumza. Alisema 'weka akiba' sio akiba ya fedha, bali ya akiba ya maneno. Tuweke akiba ya maneno. Tusimalize yote.

Zitto Kabwe(MB)
Reviewed by crispaseve on 06:22 Rating: 5

No comments

Post AD