KENYA NA TANZANIA WAHAKIKI MPAKA WA KIMATAIFA TANZANIA NA KENYA
Wataalam
wa masuala ya upimaji ardhi pamoja na maafisa mbalimbali kutoka katika
ofisi za Serikali za nchi zote mbili waliojumuika pamoja wilayani Tarime
mkoani Mara kupanga namna ya kutekeleza kazi ya uhakiki na uimarishaji
wa mipaka ya kimataifa kwa pamoja. Wa tatu kutoka kulia (walioketi) ni
Mkuu wa Msafara wa wataalam kutoka Tanzania Bw. Huruma Lugala na kulia
kwake ni Mkuu wa Msafara kutoka Kenya Bw. Julius Rotich.
Mkuu
wa zoezi la Uhamasihaji katika kazi ya kuhakiki na kuimarisha mipaka ya
Kimataifa kati ya Tanzania na Kenya Bw. Raymond Bagenda kutoka Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza wakati wa kikao cha
pamoja cha wataalam wa masuala ya upimaji ardhi kutoka katika ofisi za
Serikali za nchi zote mbili. Kikao hiko kilichofanyika wilayani Tarime
mkoani Mara kinapanga namna ya kutekeleza kazi hiyo kwa pamoja. Kushoto
ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais nchini Kenya inayohusika na
Usimamizi wa Mipaka ya Kimataifa (KIBO) Bw. Joseph Rotich.
Baadhi
ya Wataalam wa masuala ya upimaji ardhi pamoja na maafisa mbalimbali
kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na katika ofisi
zingine za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakifuatilia
mazungumzo kuhusu namna ya kutekeleza kazi ya uhakiki na uimarishaji wa
mipaka ya kimataifa kati ya Kenya na Tanzania.
…………………………………………………………………….
Na Rehema Isango, Tarime, Mara
Timu
za watalaamu wa upimaji ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Tanzania na taasisi za usimamizi wa Ardhi nchini
Kenya zimekutana wilayani Tarime mkoani Mara kwa ajili ya kuanza
utekelezaji wa kazi ya kuhakiki na kuimarisha mpaka wa Kimataifa baina
ya nchi hizi mbili.
Mapema
mwezi Machi, Naibu Waziri wa Adhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.
Angeline Mabula alitangaza azma ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuanza kuimarisha mipaka yake kwa nchi jirani za Kenya na
Uganda baada ya ziara yake ya kukagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika
Mbuga ya Wanyama ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara.
Hatua
ya uhakiki na uimarishaji wa alama za mipaka ya mikataifa inatokana na
mpaka huu kuwa wa siku nyingi na haukuwa wazi katika maeneo mengi pia
baadhi ya alama hizo kuharibiwa, kung’olewa au kuchakaa na hivyo
kusababisha Serikali pande zote kushindwa kusimamia kwa ufanisi shughuli
za mipakani, rasilimali za nchi pamoja na ulinzi na usalama.
Katika
uimarishaji wa alama hizo za mipaka hivi sasa, kutaongezwa alama mpya
ndogo zinazoonana kwa umbali wa mita 100 pamoja na kubainisha eneo la
ardhi huru kwa kila upande wa nchi (buffer zone).
Mpaka
kati ya Tanzania na Kenya una jumla ya urefu wa Kilommita 760 kuelekea
bahari ya Hindi ambapo awamu ya kwanza ya kazi ya uimarishaji mpaka
inayofanyika hivi sasa itahusisha urefu wa Kilomita 238 kutoka kando ya
Ziwa Victoria mkoani Mara hadi Ziwa Natron mkoani Arusha.
Baadaye,
kazi ya uhakiki na uimarishaji wa mipaka itaendelea katika mikoa ya
Kilimanjaro na Tanga na kisha itafanyika katika maeneo yote yanayohusika
na mipaka ya kimataifa nchini.
Uimarishaji
wa mipaka ya kimataifa nchini umefanyika mara ya mwisho mwaka 1975 kwa
kurudishia alama ambazo ziliondolewa na kuongeza nyingine mpya kwa
kuzingatia alama zilizopo.
Mbali
na Kenya nchi nyingine zinazopakana na Tanzania ni; Msumbiji, Malawi,
Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda pamoja
na visiwa vya Komoro na Shelisheli.
KENYA NA TANZANIA WAHAKIKI MPAKA WA KIMATAIFA TANZANIA NA KENYA
Reviewed by crispaseve
on
05:54
Rating:
Post a Comment